Tuesday, November 20, 2012

JAJI WARIOBA ASHAMBULIA JUKWAA LA KATIBA...

Jaji Joseph Warioba.
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amelishutumu Jukwaa la Katiba kwa kutokubaliana na mchakato unaofanywa na kujikita kutoa shutuma nyingi na za uongo dhidi ya Tume.
Jaji Warioba pia amemshutumu kiongozi wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba kwa kutoheshimu sheria inayoendesha mchakato huo, ambayo wakati wa utungwaji wake, muda mrefu ulitumika  kuhusisha wadau mbalimbali kabla ya kupitishwa na Bunge.
“Kibamba (Deus) na wenzake wanataka tufanye kazi kwa kufuata mawazo yao na si sheria iliyopo jambo ambalo sisi hatukubaliani nalo,” alisema Jaji Warioba katika mkutano wake na waandishi wa habari Dar es Salaam.
Mwenyekiti huyo alisisitiza kuwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ni sheria pekee iliyojadiliwa ndani ya mwaka mmoja na ilipopitishwa na Bunge, ilifanyiwa marekebisho tena ili kukidhi mahitaji ya wananchi.
“Baada ya sheria hii kujadiliwa na kurekebishwa mara kadhaa, wadau na wananchi wengine wametulia isipokuwa Kibamba, sisi Tume tumeamua tuendelee na kazi yetu, haya ya Jukwaa la Katiba hatutayatekeleza,” alisema Warioba.
Akichambua madai ya jukwaa hilo, Jaji Warioba alisema propaganda zinazofanywa nalo kuwa Tume haiwezi kukamilisha utungaji wa Katiba mpya kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao na kwamba haifikii wananchi wengi, zinadhihirisha kuwa Jukwaa hilo halikubaliani na mchakato huo.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Kibamba alisema Tume ya   Mabadiliko ya Katiba inalipua kazi ya kukusanya maoni ili kuwasafishia njia wanasiasa wanaopigania kwenda Ikulu.
Alidai kuwa mchakato wa mabadiliko ya Katiba utakapofikia ukingoni, ni Watanzania wasiozidi milioni moja tu, watakaokuwa wametoa maoni.
Alishauri mchakato huo usiharakishwe na kuongeza kama ni suala la kuwahisha Katiba mpya kabla ya mwaka 2015, marekebisho yafanyike katika Sheria ya Tume ya Uchaguzi (NEC) pekee.
Jaji Warioba alisema Tume imejipanga vizuri kupata maoni ya kutosha ya wananchi ambayo yatawezesha kupatikana kwa Katiba mpya na kwamba idadi ya watu si hoja, bali cha msingi ni mawazo ya watu.
“Hiki tunachofanya kwa sasa si kura ya maoni bali ni kupokea maoni, hivyo suala la idadi ya watu, si lazima wananchi wote watoe maoni bali baadhi, kwani tunafahamu kuwa wanawakilisha maoni ya wananchi wengine,” alisema Warioba.
Kuhusu kufikia walemavu, Jaji Warioba alisema Tume yake kila sehemu inakokwenda inatambua makundi yote, wanawake, wazee, vijana, wanafunzi na watu wenye ulemavu. Alisema kwa hali hiyo hawajasahau makundi hayo kwani kila kundi linapata uwakilishi.
Kuhusu muda, Jaji Warioba alisisitiza kwamba baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo, Tume ilitambua kuwa muda ni moja ya changamoto kubwa; wakajipa miezi mitatu kujiandaa kuanzia Mei hadi Julai na baada ya hapo waliweka kalenda ambayo alisisitiza kuwa wanaifuata vizuri.
Jaji Warioba alisema wameshapokea maoni kutoka mikoa 24 na sita iliyobaki walianza mchakato huo jana. Mikoa hiyo ni Dar es Salaam, Unguja Magharibi, Arusha, Simiyu, Geita na Mara.
Kutokana na kalenda, Jaji Warioba alisema hadi Oktoba mwakani watakuwa na rasimu ya Katiba mpya kabla ya kupisha Bunge la Katiba Januari na baadaye kura ya maoni ya wananchi.
Alisema wana uhakika Katiba mpya itakamilika mwaka mmoja na nusu kabla ya uchaguzi wa mwaka 2015 ili kutoa nafasi ya kurekebishwa kwa sheria mbalimbali.
Jaji Warioba alisema wao ni wazoefu katika mabadiliko ya Katiba kwani walifanya hivyo mwaka 1984 na 1992.
Akitoa tathmini kuhusu mwitiko wa wananchi wanaotuma maoni kwenye Tume, Jaji Warioba alisema wananchi 27,992 wametembelea ukurasa wa facebook na ujumbe mfupi wa maneno uliotumwa wakati wa mchakato wa awamu ya tatu ulifikia 5,909.
Alisema hadi mchakato wa kupokea maoni utakapokamilika, wanatarajia kuwa wamekutana na wananchi wapatao milioni moja.
Mtandao wa Jinsia kuhusu Katiba (GFC) umeipongeza Tume kwa kutoa nafasi ya kutoa maoni na michango yao kuhusu upatikanaji wa Katiba mpya nchini kwa makundi yote.
Pongezi hizo zilitolewa Makao Makuu ya Tume hiyo Dar es Salaam baada ya wajumbe wa mtandao huo, wakiongozwa na Magdalena Rwebangira kufika afisini hapo kuwasilisha ripoti kuhusu mchakato wa Katiba na mapendekezo yao.
Rwebangira  alisema mapendekezo waliyowasilisha Tume ni muhimu kuwamo ndani ya Katiba mpya ili haki za wanawake na makundi mengine zilindwe.
Alisema uamuzi wa Tume kuweka ratiba kwa asasi zote kuwasilisha maoni yao, utasaidia kukusanya maoni ya kila aina na baadaye kufanyiwa kazi na Tume.
Rwebangira alisisitiza umuhimu wa kuzidisha elimu ya Katiba kwa wananchi hasa vijijini ili wachangie kikamilifu wakati wa vikao vya mabaraza  ya Katiba.
Akipokea ripoti hiyo,  Jaji Warioba  alisema wanawake  hasa  vijijini wametoa maoni  ya msingi  yanayohusu maisha yao.
“Mwanzoni wanawake walikuwa hawajitokezi  sana kuzungumza katika mikutano, lakini idadi yao imekuwa ikiongezeka katika kila awamu,” alisema.
Aliipongeza GFC ambayo iko chini ya uratibu wa Asasi ya Wanawake Wanasheria  (TAWLA) kwa kushiriki kikamilifu katika ukusanyaji maoni na kutoa taarifa bila  upotoshaji.

No comments: