![]() |
| Ndege aina ya ATR 42-600 ya Precision Air ikiwa angani. |
Shirika la Ndege la Precision Air limekuwa shirika la kwanza barani Afrika na duniani kumiliki ndege ya kisasa aina ya ATR 42-600 baada ya kukamilisha mchakato wa kuinunua mapema leo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya ndege ya ATR iliyopo jijini Toulouse, Ufaransa, Filippo Bagnato alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa ununuzi wa ndege hiyo.
Ndege hiyo yenye thamani ya dola za Marekani milioni 16.4 takribani Sh bilioni 26.24, ni bora katika sekta ya usafiri wa anga duniani na imezingatia usalama wa abiria kwa hali ya juu pamoja na kutoa aina mbalimbali za burudani kwa abiria wanaosafiri.
Mkurugenzi Mtendaji wa Precision Air, Alfonse Kioko akipokea ndege hiyo alisema kuwa shirika lake litawekeza zaidi ya dola za Marekani milioni 100 kuongeza uwezo pamoja na kuongeza wigo wa safari za shirika hilo katika miaka michache ijayo.
Kioko alisema kuwa ndege hiyo mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 50, itatumika kuongeza wigo wa safari za shirika hilo kutoka Dar es Salaam na Kilimanjaro. Safari hizo zitaanza rasmi ndani ya wiki mbili zijazo baada ya kuwasili kwa ndege hiyo jijini Dar es Salaam wiki hii.
“Uwekezaji wa dola milioni 100 utatuwezesha kuwa na ndege mpya tano, nne zikiwa ni ATR 42-600 na moja ikiwa ni ATR 72-600 pamoja na injini moja mpya ya dharura katika miaka mitatu ijayo. Ujio wa ndege hizi utaongeza idadi ya ndege zetu za ATR kufikia 14 na kutuwezesha kutoa huduma bora zenye uhakika,” alisema Kioko.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya ATR, Filippo Bagnato alisema kuwa Tanzania itaendelea kuwa soko muhimu la kampuni yake na kuongeza kuwa atafanya kila jitihada kuhakikisha uhusiano baina nchi hizo unaendelea kuimarika.
“Utoaji wa ndege ya kwanza ya ATR 42-600 kwa Shirika la Precision ni suala la kihistoria katika Bara la Afrika na duniani. Baada ya kukabidhi ndege hii, Shirika la Ndege la Precision litakuwa miongoni mwa mashirika mengine yanayotoa huduma bora na zenye uhakika.
“Kwa kutumia ATR 42-600, Shirika la Precision litaendelea kujitanua kibiashara na kukumbana na changamoto zilizopo katika sekta ya usafiri wa anga Afrika na kutoa huduma zenye gharama nafuu,” alisema.
Ofisa Mkuu wa Ukaguzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Abubakar Kiroge wakati wa makabidhiano alisema kuwa uchunguzi katika ndege hiyo umeshakamilika na ndege hiyo inakidhi vigezo na taratibu zote zinazotakiwa nchini Tanzania.
“Ndege hii imekidhi vigezo vya kiusalama vinavyotakiwa. Mamlaka husika sasa ipo tayari kuipatia Precision Air cheti cha kuwezesha ndege hiyo kutumika nchini Tanzania. Ukweli ni kwamba ndege hii imezingatia usalama wa abiria kwa haki ya juu,” alisema.

No comments:
Post a Comment