![]() |
| Spika wa Bunge, Anne Makinda. |
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi wameonywa na Spika wa Bunge, Anne Makinda kwa kitendo cha kulidhalilisha na kulifedhehesha Bunge kwa kuzusha tuhuma za uongo dhidi ya baadhi ya wabunge ambazo hata hivyo zimebainika hazina ukweli wowote.
Licha ya kuwataka kutorudia tena kuibua uzushi, Spika pia amewaonya wabunge watano akiwemo Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki kwa kitendo cha 'kushabikia’ na kuzungumza maneno ambayo hawakuwa na ushahidi nayo.
Wabunge hao waliotiwa hatiani na Kamati hiyo ndogo ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge iliyokuwa ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Hassan Ngwilizi ni wawili kutoka CCM, Mbunge wa Mwibara, Alphaxard Kangi Lugola na Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Kessy na watatu wa Chadema ambao ni Lissu, Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika.
Alitoa onyo hili bungeni jana alipokuwa anasoma ripoti ya 'Kamati ya Ngwilizi’ iliyokuwa inachunguza tuhuma za baadhi ya wabunge na wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini kujihusisha na vitendo vya rushwa katika kutekeleza kazi zao za Kibunge.
Waliokuwa wanahusishwa ni pamoja na Mbunge wa Viti Maalumu, Sarah Msafiri Ally (CCM), Suleiman Zedi ambaye ni Mbunge wa Bukene kwa tiketi ya CCM, Munde Tambwe wa Viti Maalumu na Christopher Ole Sendeka, mbunge wa Simanjiro kwa tiketi ya CCM.
Katika ripoti yake aliyoisoma kwa saa moja, wabunge wote waliotumiwa kwa vitendo vya rushwa hawakupatikana na hatia.
Kutokana na ukweli huo, alisema suala hilo limetoa somo na mfano mzuri juu ya mazoea yasiyofaa ya wabunge kuzungumza mambo bungeni bila kufanya utafiti, na badala yake kujikuta wakiingia katika mtego wa kutuhumu watu au taasisi.
“Kwa haya yaliyotokea, kuna umuhimu wa wabunge kujizuia kusema mambo ambayo ni tetesi, na pia ni lazima wabunge wajizuie na tabia ya kutaka kusema tu kuhusu jambo lolote ili wasikie, bila ya kuwa na ukweli wa jambo lenyewe,” alisema.
Ndipo, kutokana na uchunguzi wa kuonesha kuwa tuhuma hazikuweza kuthibitishwa, na pia kwa kuwa tuhuma zenyewe zimeathiri kwa kiasi kikubwa hadhi na heshima ya Bunge kama taasisi, na pia hadhi na heshima ya wabunge waliohusishwa, aliamua kutoa uamuzi kwa mujibu wa utaratibu wa kibunge.
Alianza kwa kumkuta Maswi na hatia, akisema amelidhalilisha na kulifedhehesha Bunge kwa kuzusha tuhumza za uongo na kufanya umma wa Watanzania kuamini baadhi ya wabunge wa Kamati ya Nishati na Madini wanajihusisha na vitendo vya rushwa.
“Na kwa kufanya hivyo, ametenda kosa la kuvunja haki za Bunge, na anastahili adhabu,” alisema huku akimtaka asirudie tena kosa la kuzua tuhuma dhidi ya Bunge na Wabunge.
Onyo kama hilo lilitolewa kwa Kessy, Lugola, Mnyika na Selasini, wakionywa kutorudia kosa la kuzungumzia bungeni jambo wasilokuwa na uhakika nalo.
Lakini kwa licha ya kutakiwa kutorudia kuzungumza jambo asilokuwa na uhakika nalo, alionekana kuvunja Kanuni za Bunge kwa kulisemea nje ya Bunge suala la mgongano wa maslahi kwa wabunge waliotuhumiwa kujinufaisha kwa kufanya biashara na Tanesco, akiwataja kwa majina tena kwa ushahidi wa kuambiwa.
Hata hivyo, Spika alimuombea Lissu msamaha kwa wabunge Sarah Msafiri na Munde Tambwe waliokuwa wanatuhumiwa kwa rushwa na pia kujinufaisha kibiashara ndani ya Tanesco.
Naye Profesa Muhongo, amepatikana na hatia baada ya kushindwa kuthibitisha kauli yake aliyowahi kuitoa bungeni kuwa, ana ushahidi usio na shaka wa baadhi ya wabunge na wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini kufanya biashara na Tanesco, akisema baadhi wameingia mkataba wa kuiuzia matairi huku wakipaisha bei tofauti na ile ya kwenye mkataba.
“Kwa kuwa kauli hii aliitoa bunge tena kwa kutangaza anao ushahidi, lakini ukweli wake haukuweza kuthibitishwa, namtaka Waziri Muhongo awe mwangalifu anapotoa kauli bungeni kwa sababu kauli za mawaziri huchukuliwa kuwa ni kali za Serikali, hivyo anapotoa kauli yoyote bungeni ahakikishe ana uhakika wa jambo analolisema,” alisema.
Spika Makinda alilazimika kuunda tume aliyoipa hadidu moja tu ya rejea ambayo ni kuchunguza na kumshauri Spika iwapo tuhuma kwa baadhi ya wajumbe wa Kamai ya Nishati na Madini kujihusisha na vitendo vya rushwa ni za kweli au hapana.
Alifanya hivyo baada ya Maswi kuandika barua yenye Kumbukumbu SBA. 88/223/01/28 aliyoandika kwa Katibu wa Bunge Julai 31 mwaka huu akimtuhumu Msafiri kwamba alikwenda ofisini kwake na kuomba rushwa ya Sh milioni 50 aweze kuwagawia baadhi ya wabunge na wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini waweze 'kukingia kifua’ kile walichodai utendaji wake usioridhisha katika wizara hiyo.
Aidha, Maswi alimtuhumu Zedi kuomba rushwa ya Sh milioni 2 kwa kila mjumbe wa Kamati.
Wabunge wengine, Tambwe na Ole Sendeka, walihusishwa na rushwa baada ya kuonekana kuwa tishio kwa Katibu Mkuu huyo waliyembana na kumweleza lazima aachia nafasi hiyo kwa kuwajibika, kutokana na utendaji usioridhisha.
Kutokana na tuhuma hizo zilizoanza kama uvumi baadaye kuibua hoja nzito bungeni, Spika alilazimika kuvunja kamati ya nishati na madini na kuunda kamati ya kuchunguza tuhuma.
Lakini baada ya kukabidhiwa matokeo ya uchunguzi, Spika alilieleza bunge kuwa, Kamati imebaini Maswi aliibua tuhuma hizo kama njia ya kujihami dhidi ya tishio la Wabunge hao kutaka kumkwamisha ili ang’oke katika nafasi hiyo.
Sendeka aliingizwa katika tuhuma za rushwa kutokana na kuongoza `vita’ dhidi ya viongozi wakuu wa Wizara ya Nishati na Madini, akitaka hatua zichukuliwe dhidi yao kutokana na kukiuka sheria ya manunuzi, kwa kuamuru kununuliwa kwa lita milioni kumi kutoka kampuni ya Puma Energy (T) Ltd ili kuendeshea mitambo ya IPTL, wakati Tanesco ilishaingia mikataba na makampuni mengine kwa ajili hiyo pia.
Ndipo baadhi ya wabunge wakiwemo, Kessy na Kangi Lugola wakaanza kutilia shaka msimamo wake, wakiamini amehongwa na makampuni ya mafuta.
Lakini baada ya kubanwa, hakuna aliyeweza kutoa ushahidi, kama ilivyokuwa kwa Mnyika ambaye katika hotuba yake ya Kambi ya Upinzani Bungeni alisema kuwa kuna kampeni inafanywa ndani ya nje ya Bunge ili uamuzi wa Katibu Mkuu Maswi ubatilishwe kwa maslahi ya makampuni yaliyokosa Zabuni, naye alishindwa kuthibitisha.
Pamoja na uchunguzi kuisafisha Kamati ya Nishati na Madini, mara baada ya kuahirisha Bunge Spika alisema hajairudisha kamati hiyo na badala yake itaundwa kamati nyingine katika mkutano ujao wa Bunge.

No comments:
Post a Comment