Sunday, November 11, 2012

KIAMA CHA VIGOGO WANAOFICHA FEDHA USWISI KIMEWADIA...

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.

Serikali imeahidi itatumia vyombo vyake vya ndani na nje katika kufuatilia hoja ya Mbunge wa  Kigoma Kaskazini (Chadema), Kabwe Zitto juu ya tuhuma za kuwepo kwa Watanzania walioficha fedha haramu katika benki za nje.
Uamuzi huo wa Serikali umetokana na hoja ya mbunge huyo kuwa, baadhi ya Watanzania, wakiwemo viongozi wastaafu wa Serikali, wameficha fedha nyingi haramu nje ya nchi na kwamba anayo orodha ya majina yao na ya benki walikohifadhi fedha hizo
Akijadili hoja hiyo bungeni jana, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema alisema kwa vile tayari serikali kupitia vyombo vyake vya usalama na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeshaanza kuzifanyia uchunguzi tuhuma hizo, baadhi ya hoja zilizowasilishwa na Zitto zinakosa mashiko.
Alisema mapendekezo mengine yaliyotolewa na Zitto yanapingana na sheria za nchi, ikiwa ni pamoja na kutoruhusiwa kwa mtu yeyote kutoa siri za benki kuhusu wateja wake na kwamba sheria hiyo imetungwa na bunge.
Werema alisisitiza kuwa, majina ya wanaotuhumiwa kuficha fedha nje ni muhimu kwa vile yanatoa nafasi kwa vyombo husika kupata mahali pa kuanzia. Alimtaka Zitto na wabunge wengine wenye ushahidi wa suala hilo kuuwasilisha kwake ama kwa Spika wa Bunge.
Werema alisema kwa kuwa Serikali imeshaanza kufanya uchunguzi wa tuhuma hizo kupitia kwenye vyombo vyake vya usalama, ni vyema iachwe iendelee na kutoa taarifa kwa bunge kuhusu matokeo ya uchunguzi huo katika kikao chake cha 11 kitakachofanyika Aprili mwakani.
Akichangia hoja hiyo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliunga mkono mapendekezo yaliyotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kutaka vyombo vinavyohusika viachwe viendelee kufanya uchunguzi kabla ya kutoa taarifa kwa Bunge.
Pinda alisema licha ya Zitto kutoa hoja hiyo, amekuwa mwangalifu na anasita kutaja majina ya wahusika kwa sababu za msingi kwa vile anafahamu vyema ukweli na uhalali wa yaliyofanywa na watuhumiwa unahitaji ushahidi wa kutosha ili asionekane amezua jambo, ambalo hana hakika nalo.
"Tunachopaswa  kujua ni kina nani hawa Watanzania, ambao wamekwenda kuweka pesa nje ya nchi kinyume cha sheria. Kuweka pesa nje si tatizo, lakini lazima iwe ni kinyume cha sheria na huo ndio msingi wa mjadala uliopo bungeni," alisema.
Pinda alisema hana ugomvi na hoja iliyotolewa na Zitto bungeni na kuongeza kuwa, ushauri wa Mwanasheria Mkuu umelenga kuiwezesha serikali kuwa sehemu ya yale yanayohitajika kufanywa katika kupeleleza tuhuma hizo.
"Napenda kukubaliana na Mwanasheria Mkuu lakini lazima bunge lijisikie kwamba wote tumeridhika, hakuna kwamba likienda kule tutaficha, hakuna sababu za kuficha kwa sababu mtu kama ameiba ni mwizi tu," alisema.
Pinda alimtaka Zitto aisaidie serikali kwa kutaja majina ya watuhumiwa na mtu mwingine anayeweza kutoa taarifa zitakazoisaidia serikali katika uchunguzi wake na kusisitiza kuwa, kamwe majina hayo hayawezi kuchakachuliwa.
"Tukifanya hivyo, tutakuwa tumefanya jambo zuri na hatutaweza kuilaumu serikali wala bunge," alisema.
Akihitimisha mjadala huo, Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema kwa mujibu wa kanuni za Bunge, hoja iliyowasilishwa na Zitto haiwezeshi kuundwa kwa kamati teule kwa ajili ya kujadili tuhuma hizo.
Makinda alisema hiyo haina maana kwamba hoja ya Zitto imetupwa, isipokuwa serikali imeamua kuzifanyia kazi kwa kuendeleza uchunguzi wake na kutoa taarifa kwa bunge katika kikao chake cha 11.
Katika hoja yake, Zitto alisema viongozi mbali mbali wastaafu wa serikali wanahusika kuficha mabilioni ya pesa katika benki za nje, hasa Uswisi na kutaka wachunguzwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Mbali na hilo, Zitto alipendekeza iwe marufuku kwa kiongozi yeyote wa umma au mume au mke wake au mtoto wake kuwa na akaunti nje ya nchi isipokuwa kwa sababu maalumu na kwa kibali rasmi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Zitto pia alitaka serikali kuwasiliana na Benki ya Dunia kupitia kitengo cha ‘Assets Recovery Unit’ ili mabilioni ya fedha na mali ambazo zimetoroshwa nje ya nchi kwenda Uswisi, Dubai, Mauritius na maeneo mengine ziweze kurejeshwa.
Wakichangia hoja hiyo juzi, Werema na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu, William Lukuvi walimtaka Zitto awataje kwa majina Watanzania wanaotuhumiwa kuficha fedha haramu nje ya nchi ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Kwa upande wake, Lukuvi alisema kama Zitto anayo majina, anapaswa kuyaweka hadharani ili serikali iweze kuendesha uchunguzi wa uhakika na hatimaye kuwabaini wahusika na kuwachukulia hatua.
Akijadili hoja hiyo, Luhaga Mpina (Kisesa -CCM) alisema hoja hiyo imeletwa kwa wakati mwafaka, lakini alimtaka Zitto aache kuzunguka, badala yake ayaweke hadharani majina ya watuhumiwa ili sheria  ichukue mkondo wake.
Alisema hoja ya Zitto kutaka iundwe tume maalumu kwa ajili ya kuchunguza tuhuma hizo, haina maana iwapo ataendelea kuficha majina yao. Alisema jambo la msingi ni taasisi husika kuanza kuwachunguza mara moja wahusika wa tuhuma hizo wanaofahamika kwa majina.
"Ningekuwa Zitto, ningekabidhi leo hii hii hati zote kuhusu wahusika wa tuhuma hizo ili hatua zianze kuchukuliwa," alisema Mpina na kumtaka Zitto akabidhi hati hizo kwenye meza ya Spika iwapo anazo.
Naye Christopher Ole Sendeka (Simanjiro-CCM) alisema wapo wafanyabiashara halali wanaohifadhi fedha zao nje ya nchi kihalali, lakini wengine ni mafisadi na wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria.
Alisema haiwezekani ziwepo tuhuma kubwa na nzito kwa watu wenye dhamana kubwa ya nchi halafu Serikali ikakaa kimya. Alisema aliwahi kutoa hoja bungeni kutaka watu hao watajwe majina, lakini anashangaa kuona hadi sasa kimya.
Ole Sendeka alitaka hoja iliyowasilishwa na Zitto isifanyiwe marekebisho kama alivyopendekeza Mwanasheria Mkuu, badala yake iungwe mkono kwa bunge kuunda kamati teule kwa ajili ya kuchunguza tuhuma hizo.
Alisema haiwezekani watu waendelee kutajirika ghafla baada ya kuwa hohehahe kwa miaka mingi na iwapo viongozi wa zamani na wa sasa wa serikali ama watoto wa vigogo wanahusika, hatua zichukuliwe bila kujali nyadhifa zao.
Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema) aliomba mwongozo wa mwenyekiti na kusema haoni sababu kwa nini Zitto ashinikizwe kutaka majina kwa sasa wakati ameeleza wazi kwenye hoja yake kuwa, atakuwa tayari kufanya hivyo baada ya kuundwa kwa kamati teule kwa ajili ya kuchunguza tuhuma hizo.
Naye Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugora (CCM) alisema bunge halipaswi kumng'ang'ania Zitto ataje majina ya watuhumiwa, badala yake iundwe kamati teule kwa ajili ya kuchunguza tuhuma hizo na wahusika wachukuliwe hatua kali.
"Zitto kaleta ufunguo wa kuanzia. Akaunti zinajulikana zilipo, wanaozimiliki wanajulikana. Waziri Membe (Benard Membe-Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa) alishatamka wazi kwamba, anayajua majina ya watu hao, awataje," alisema.
Wakati Lugora alipotaja jina la Membe, waziri huyo alionekana akigonga meza kuunga mkono hoja hiyo huku akitingisha kichwa kuonyesha kwamba anaiafiki hoja hiyo.
Mbunge huyo alisema kwa sasa wananchi wamechoka kuendelea kusikiliza wimbo wa mafisadi kwa sababu hawawezi kuondoka kwa kuimbiwa wimbo huo.
Alisema katika hatua za awali, uchunguzi unaweza kufanyika bila ya wahusika kutajwa majina.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda wiki iliyopita alisema tayari serikali imeshaanza kuchunguza tuhuma hizo na kuongeza kuwa, uchunguzi huo hauwezi kufanyika kwa kipindi kifupi. Alisema uchunguzi
utakapokamilika, serikali itatoa taarifa.

No comments: