Sunday, November 11, 2012

CCM YAANZA VIKAO VYAKE VYA MWISHO DODOMA LEO...

Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete.

CCM leo imeanza vikao vyake vya mwisho kuelekea katika Mkutano Mkuu wa Nane wa chama hicho ambao mwishoni utahitimisha kupanga safu za viongozi  watakaokiongoza kwa miaka mitano ijayo.
Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete alitua hapa jana saa 8.40 mchana, tayari kuongoza vikao hivyo vinavyoanza leo kwa kutanguliwa na Kamati Kuu asubuhi na baadaye Halmashauri Kuu ya Taifa.
Kazi kubwa ya leo ya Kamati Kuu na NEC ni kupokea taarifa ya maandalizi ya Mkutano Mkuu utakaoanza kesho na pia kufanya uteuzi wa jina la atakayegombea uenyekiti na mawili ya Makamu Mwenyekiti kwa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.
Kwa mujibu wa Katibu wa Itikadi na Uenezi ya NEC, Nape Nnauye, majina hayo ndiyo yatakayopelekwa katika Mkutano Mkuu kwa ajili ya kupigiwa kura.
“Kesho (leo) kutakuwa na vikao vya Kamati Kuu asubuhi na kufuatiwa na Halmashauri Kuu ya Taifa. Kazi yao kubwa itakuwa kupokea taarifa ya maandalizi ya Mkutano Mkuu na uteuzi wa wagombea wa uenyekiti na makamu wake,” alisema Nape.
Alisema Mkutano Mkuu utakaofanyika kwa siku tatu kuanzia kesho ukiwa na kaulimbiu ya “Umoja, Amani na Maendeleo, Tuko imara, tunajenga nchi yetu,” utahudhuriwa na wajumbe 2,214 ambao ni wajumbe halali na kutakuwa na waalikwa 700.
“Kwa ujumla, ndani ya ukumbi wa Mkutano Mkuu tunategemea kuwa na watu zaidi ya 3,000, na nje kutakuwa na watu zaidi ya 4,000.
“Hawa wanajumuisha waalikwa wa ndani na nje, watu maarufu na pia nje ya ukumbi kutakuwa na burudani na mamalishe wengi. Pia kutakuwa na luninga kubwa ya kuonesha matukio yote ya ndani ya ukumbi,” alisema.
Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi, alisema mkutano huo unatarajiwa kuoneshwa moja kwa moja katika vituo vya televisheni vya Star TV na TBC na kwa watu wa nje ya nchi, wataufuatilia kupitia mitandao ya kijamii ambako CCM itaweka mkutano huo.
Alisema kabla ya kuanza kwa Mkutano Mkuu kesho kwenye Ukumbi wa Kizota, asubuhi Mwenyekiti Rais Jakaya Kikwete ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa Ukumbi wa mikutano wa chama hicho utakaojengwa eneo la Makulu katika Manispaa ya Dodoma.
Tayari wajumbe wamekwisha anza kuwasili mjini Dodoma na maandalizi yanaonekana kwa mji huu mkuu wa Tanzania kupambwa na bendera za kijani na Makao Makuu ya CCM katika Barabara ya Nyerere yalikuwa yakisafishwa kwa kupakwa rangi mpya.
Rais Kikwete anayetarajiwa kupewa nafasi nyingine ya kuongoza chama hicho, aliwasili akitokea Dar es Salaam akiwa na mkewe Mama Salma Kikwete.
Akiwa amevalia nguo rasmi za chama hicho tawala, suruali nyeusi, shati la kijani na kofia ya kijani, alilakikiwa na Makamu wake Bara, Pius Msekwa, Nape, Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Adam Kimbisa na Mkuu wa Mkoa, Dk Rehema Nchimbi.
Akizungumzia kuhusu taarifa za kuwapo mpango wa kutaka Kikwete asiendelee kushika kofia mbili, urais na uenyekiti wa CCM, Nape alisema taarifa hizo zitakuwa za ovyo kwa demokrasia ndani ya chama.
“Hata sisi tunayasikia hayo, lakini hoja hizo zitakuwa za ovyo kwa demokrasia ya chama chetu. Hazina mashiko na ni hoja zinazosukumwa na watu wenye uroho na uchu wa madaraka,” alisema Nape.
Zimekuwapo taarifa na kudaiwa pia kusambazwa kwa vipeperushi hapa kutoka kwa baadhi ya wanachama wa CCM wakitaka Rais Kikwete asiendelee na wadhifa wa uenyekiti wa chama, wakidai apate muda wa kuisimamia vyema Serikali kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho.
Wanadai kwa vuguvugu la sasa la upinzani nchini, mwanachama mwingine apewe jukumu la kuongoza chama hicho na kukabiliana na upinzani; hoja inayopingwa na wanachama wengi. 
Katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti, kwa Bara Msekwa atakuwa anaandoka katika wadhifa huo kwa sababu atakuwa mmoja wa watu watakaounda Baraza la Wazee la chama hicho tawala.
Wengine ni marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, Salmin Amour Juma na Abeid Amaan Karume. Pia yumo John Malecela.
Nafasi ya Msekwa inatajwa baadhi ya watu wanaoweza kuishika akiwamo kada maarufu Abdulrahaman Kinana aliyeng’atuka hivi karibuni.
Kwa Zanzibar, Rais Dk Ali Mohamed Shein hakuna shaka sasa atakamata umakamu mwenyekiti baada ya kuwa Karume ‘ameung’ang’ania’ tangu alipoondoka madarakani mwaka 2010.
Lakini uhondo mwingine katika Mkutano Mkuu utakuwa katika nafasi za ujumbe wa NEC ambako kwa Bara, vigogo 31 wanawania nafasi 10.
Miongoni mwao wamo mawaziri kadhaa na wajumbe wanaounda Sekretarieti ya sasa  wakiongozwa na Katibu Mkuu Wilson Mukama.
Wengine ni John Chiligati (Naibu Katibu Mkuu), Mwigulu Nchemba (Fedha na Uchumi), January Makamba (Siasa na Uhusiano wa Kimataifa).
Pia wamo Bernard Membe, Shy-Rose Bhanji, William Lukuvi, Dk Mathayo David, William Malecela, Hiza Tambwe, Stephen Wasira, Ruth Msafiri, Martine Shigella, Assumpta Mshama, Dk Fenella Mukangara.
Katika Kundi la Zanzibar, wamo vigogo kama Kidawa Hamid Saleh, Samia Suluhu Hassan, Abdisalam Issa Khatib, Muhammed Seif Khatib, Dk Hussein Ali Mwinyi, Omar Yussuf Mzee, Mouldine Castico, Shamsi Vuai Nahodha, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa.
Nape ambaye hakuwania nafasi yoyote katika uchaguzi huo wa ndani ulioanza mapema mwaka huu, ameelezea sababu za kufanya hivyo.
“Niliona ingekuwa vizuri kama wajumbe wote wa Sekretarieti tusingegombea ili kusimamia vyema mchakato kwani isingekuwa vizuri kuwa mchezaji na refa wakati mmoja,” alisema Nape na kuongeza:
“Niliona ingekuwa vyema niwe sehemu ya wasimamizi na kutumia muda mwingi kwa kazi hii kuliko kuwa mgombea.”
Mwanasiasa huyo machachari kijana anatajwa katika duru za siasa kama mmoja wa wanaoweza kumrithi Mukama wakati Sekretarieti mpya itakapoundwa kati ya Jumanne jioni au Jumatano asubuhi. 

No comments: