Friday, November 9, 2012

NDEVU ZA SHEKHE FARID WA UAMSHO ZAZUA NONGWA MAHAKAMANI...

Shekhe Farid Hadi Ahmed.
Mawakili wa viongozi wa Jumuiya ya Uamsho wanaoshitakiwa kwa tuhuma tofauti, wamelalamikia kuvunjwa kwa haki za wateja wao wakiwa rumande ikiwamo kunyolewa ndevu kwa wateja hao akiwamo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar, Shekhe Faridi Hadi Ahmed.
Wengine wanaoshitakiwa katika kesi hiyo mbali na Shekhe Farid ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Uamsho, Shekhe Mselem Ali Mselem, Mussa Juma Issa, Suleiman Juma Suleiman, Azan Khalid Hamdan, Khamis Ali Suleiman, Hassan Bakar Suleiman na  Ghalib Ahmada Omar.
Viongozi hao wako rumande wakishitakiwa kwa kutoa lugha za uchochezi na kusababisha ghasia na vitendo vya uvunjifu wa amani uliosababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara.
Mbele ya Mrajisi wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, George Kazi jana, mawakili hao Salum Toufik na Abdallah Juma Kaka, wakiwasilisha hoja mbalimbali za uvunjifu wa haki za watuhumiwa walidai kuwa wateja wao wamenyolewa ndevu wakiwa rumande.
Mawakili hao walidai kuwa hatua hiyo ya Magereza ni kinyume na uhuru wa kuabudu, kwani ndevu kwa mashekhe ni sehemu ya ibada.
Akijibu hoja hizo, Mwanasheria wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Ramadhani Nasibu, akinukuu vifungu vya sheria kwenye Katiba ya Zanzibar, alidai kama kuna haki zinazovunjwa na chombo chochote au mtumishi wa Serikali, kuna mahala pengine pa kupeleka malalamiko hayo.
Baada ya mabishano hayo, Kazi aliamuru washitakiwa  wote warudishwe rumande hadi Novemba 20, itakapokuja katika Mahakama Kuu ya Zanzibar kutajwa tena.
Viongozi hao kwa mara ya kwanza walifikishwa mahakamani hapo wakiwa wamenyolewa ndevu Oktoba 26 chini ya ulinzi mkali wa Polisi.
Kabla ya hapo, Oktoba 22 viongozi hao walifikishwa mahakamani hapo wakiwa na ndevu nyingi kidevuni mwao, lakini Oktoba 26  walikuwa wamenyolewa na kuwafanya wawe na mwonekano tofauti, jambo ambalo lilizua gumzo kubwa miongoni mwa watu waliofika kusikiliza kesi hiyo.
Naye Flora Mwakasala anaripoti kuwa wakati Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Shekhe Issa Ponda akiendelea kusota rumande kwa kesi ya uchochezi na wizi wa mali zenye thamani ya Sh milioni 59, jana kiongozi mwingine wa taasisi hiyo amepandishwa kizimbani na kusomewa mashitaka hayo.
Mukadam Swalehe (45) alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashitaka manne mbele ya Hakimu Victoria Nongwa.
Hata hivyo, Swalehe alirudishwa rumande, kwa kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) aliwasilisha hati ya kuzuia dhamana kwa mshitakiwa kama ilivyo kwa Shekhe Ponda.
Awali wakili wa Serikali Tumaini Kweka alidai kuwa Oktoba 12 eneo la Chang’ombe Markasi mshitakiwa aliingia kwa nguvu  katika kiwanja kinachomilikiwa na kampuni ya AgriTanzania  Limited kwa nia ya kujimilikisha kiwanja hicho isivyo halali.
Alidai siku hiyo hiyo, bila uhalali mshitakiwa katika hali iliyokuwa ikisababisha uvunjifu wa amani, alijimilikisha  kwa nguvu ardhi  ya  kampuni hiyo na kuiba vifaa na malighafi, matofali 1,500, nondo, tani 36 za kokoto mali zote zina thamani ya Sh milioni 59.7.
Katika mashitaka ya uchochezi, inadaiwa katika eneo hilo la Chang’ombe Markasi kwa maelezo kuwa yeye ni kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu (T), alishawishi wafuasi wake ambao ni washitakiwa hao kutenda makosa hayo.
Wakili Kweka alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na DPP amewasilisha hati ya kuzuia dhamana kwa mshitakiwa.
Hakimu Nongwa aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 15 mshitakiwa atakapounganishwa na washitakiwa 50 akiwamo Shekhe Ponda na kusomewa maelezo ya awali.

No comments: