Friday, November 9, 2012

DK MWAKYEMBE AVUNJA BODI YA MAMLAKA YA BANDARI (TPA)...

Dk Harrison Mwakyembe.
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amevunja Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na kuteua wajumbe wapya wa Bodi hiyo katika jitihada zake za kurejesha ufanisi katika bandari hiyo.
Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari, ilieleza kuwa Dk Mwakyembe amevunja Bodi hiyo  tangu Novemba 6 kwa madaraka aliyopewa na Sheria ya Bandari  ya Mwaka 2004.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wajumbe sita walioondolewa wa Bodi hiyo ni Dustan Mrutu, George Ally, Mtutura Mtutura, Emmanuel Mallya, Mwantumu Malale na Maria Kejo.
Baada ya kuvunja Bodi hiyo, taarifa hiyo ya Wizara ya Uchukuzi, ilieleza kuwa Dk Mwakyembe ameunda Bodi mpya yenye wajumbe wanane ambao walitakiwa kuanza kazi mapema iwezekanavyo.
Walioteuliwa kuingia katika Bodi hiyo ni Dk Jabiri Bakari, John Ulanga, Caroline Temu, Jaffer Machano, Dk  Hildebrand Shayo, Saidi Sauko, Julius Mamiro na Asha Nassoro.
Baada ya kuteua Bodi mpya, Waziri Mwakyembe aliiagiza Menejimenti ya TPA, kuwapa nyaraka zote muhimu wajumbe wapya wa Bodi hiyo mpya, ili wajiandae kabla hawajakutana nao ndani ya siku kumi kuanzia Novemba 6.
Pia aliweka wazi kuwa katika mkutano huo kati ya Bodi mpya na Waziri, Serikali itaingia mkataba wa ufanisi na Bodi hiyo ili wafanikishe bandari ichangie zaidi kwenye pato la Taifa.
Safishasafisha hiyo ya bandari inayofanywa na Mwakyembe ilianzia katika Menejimenti ambapo aliwasimamisha watendaji wa bandari hiyo, akiwamo Mkurugenzi Mkuu, Ephraim Mgawe, naibu wakurugenzi wakuu wawili aliotajwa kwa jina moja moja la Mfuko na Koshuma na Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Cassian Ng’amilo, Meneja wa Kurasini Oil Jet na Mhandisi wa kitengo cha mafuta.
Baada ya kusimamisha kazi vigogo hao, Dk Mwakyembe aliunda kamati ya uchunguzi iliyoongozwa na Bernard Mbakileki ambayo ilifanya kazi na kukabidhi ripoti ambayo Waziri aliahidi kuifanyia kazi.
Mwanzoni mwa wiki hii, Dk Mwakyembe alisema kama kuna watu wanaopanga kuhujumu bandari ya Dar es Salaam ili kukwamisha mabadiliko yaliyoanza, watambue wanajisafishia njia ya kwenda kutumikia kifungo gerezani.
Dk Mwakyembe alisema mabadiliko TPA, lazima yafanyike ili bandari itoe huduma bora kuliko hata ya Mombasa, Kenya,  ili kuleta tija katika pato la Taifa.
Alisema habari anazosoma katika vyombo vya habari zikielezea mipango inayofanyika kuhujumu bandari ya Dar es Salaam kama ni kweli, basi waliopo katika mtandao huo wafahamu watanyofolewa mmoja baada ya mwingine na kushughulikiwa kikamilifu, kwa sababu Serikali sasa imechoka kuchezewa.

No comments: