Wednesday, November 7, 2012

KATIBU WA MUFTI ZANZIBAR AMWAGIWA TINDIKALI...

Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Soraga akitolewa katika chumba cha huduma ya kwanza katika Kospitali Kuu ya Mnazi Mmoja, Zanzibar baada ya kumwagiwa tindikali na watu wasiojulikana wakati akifanya mazoezi katika Viwanja vya Mwanakwerekwe, Zanzibar jana asubuhi.
Licha ya viongozi wa kitaifa na kimataifa kutaka utulivu na amani visiwani Zanzibar, hali inaonekana kutotengemaa na kuzidisha hofu miongoni mwa wananchi.
Kinachoonekana sasa ni wimbi la kutaka kukomoa baadhi ya viongozi wa dini ya kiislamu wanaopingana na msimamo wa kikundi kingine cha waumini wa dini hiyo na sasa kufikia hatua ya kudhuriana kimwili.
Hali inaonekana kuwa hiyo baada ya Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Fadhil Suleiman Soraga (55), kujeruhiwa usoni, kichwani, kifuani, mgongoni na mikononi kwa kumwagiwa tindikali na mtu asiyefahamika.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar, Aziz Juma Mohammed, alisema jana kwamba Shekhe Soraga, alimwagiwa tindikali hiyo jana asubuhi kwenye viwanja vya Mabata karibu na Msikiti wa Msumbiji akiwa katika mazoezi ya kutembea.
Alifafanua kuwa Shekhe Soraga alikuwa akitoka upande wa uwanja wa Michezo wa Amaan kwenda Mwanakwerekwe na alikutana na mtu ambaye naye alionekana kama mfanya mazoezi mwenzake akitoka upande wa Mwanakwerekwe kwenda Amaan.
Kamanda Mohammed aliyehusisha suala hilo na uhalifu wa kawaida, alisema walipokuwa wakipishana, mtu huyo akiwa na kimiminika hicho kwenye jagi la maji ya kunywa, alimmwagia Soraga usoni.
Alisema baada ya tukio hilo, Shekhe Soraga alikaa chini akiugulia maumivu na baada ya muda wasamaria wema walijitokeza na kumpeleka Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja ambako alipatiwa matibabu ya awali na kisha kusafirishwa kwa ndege ya Serikali kwenda Dar es Salaam ambako amelazwa katika Hospitali ya Aga Khan.
Wakati Polisi wakisisitiza kuwa hawapendi kuhusisha suala hilo na jambo lolote, ndugu wa karibu na baadhi ya viongozi wenzake, wamehusisha suala hilo na kitisho alichopewa baada ya kutoa hotuba ya Iddi el Fitri.
Mkuu wa Shughuli za Dini ya Kiislamu Zanzibar, Thabit Norman Jongo aliliambia gazeti hili akiwa  Aga Khan kuwa kabla ya kufikwa na janga hilo, Shekhe Soraga alipokea vitisho mbalimbali kutoka kwa watu wasiojulikana.
Alisema, alianza kutishwa baada ya kutoa hotuba iliyokemea vitendo vya kuchoma makanisa na kuhatarisha amani visiwani katika Baraza la Iddi el Fitr lililofanyika visiwani humo.
“Lakini pamoja na vitisho hivyo, hatujajua mhusika wa unyama huo ni nani. Hatufahamu kwa kweli na wala hatuhusishi kikundi chochote hadi polisi watakapoweka wazi watakayogundua katika uchunguzi wao,” Jongo alisema.
Mmoja wa ndugu wa familia ambaye hakutaka kutajwa jina gazetini alisema katika hatua za awali inaonekana wazi kwamba hotuba aliyotoa siku ya swala ya Iddi katika Msikiti wa Muembe Shauri, ndicho chanzo cha matatizo hayo.
“Sisi tunajua, kwamba Shekhe Soraga hana maadui...lakini hotuba ya swala ya Iddi ilikera baadhi ya watu wakiwamo wafuasi wa Uamsho,” alisema.
Katika hotuba hiyo, Shekhe Soraga aliitaka Serikali kuwachukulia hatua kali viongozi wa Uamsho ambao wanaonekana wazi wazi kwamba ndio chanzo cha fujo na vurugu visiwani hapa.
Shekhe Soraga alisema vurugu hizo zimetia hasara kubwa Serikali kwa kuharibu miundombinu ya barabara na wananchi wa kawaida wakiwamo mama lishe.
Alitoa mfano wa mfanyabiashara mwanamke muuza matikiti ambayo yalivamiwa na wafanya vurugu na kuharibiwa kwa kukatwa mapanga.
Hotuba ya swala ya Iddi iliyotolewa na Shekhe Soraga ilihudhuriwa na Rais wa Zanzibar,  Dk Ali Mohamed Shein, Makamu wa Kwanza wa Rais, Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi na viongozi waandamizi wa SMZ.
Baada ya hotuba hiyo, Rais Shein  alisema  hakuna mtu aliye juu ya sheria na kusisitiza kuwa viongozi waliohusika na fujo na vurugu watashughulikiwa na vyombo vya Dola.
Naye Mufti wa Zanzibar, Shekhe Salehe Kabi aliwataka wananchi wa Zanzibar  kuacha visa vya kulipizana visasi  ambavyo vinaweza kuleta vurugu na kuzua mtafaruku Zanzibar.
Alitaka watu wote kuwa wamoja na kushirikiana kwa kila jambo na kuonya kwamba tofauti za rangi, kabila, dini na itikadi za kisiasa zisiwe chanzo cha mfarakano wa umoja wa Wazanzibari.
Mke wa Soraga aliyefuatana na mwanawe wa kiume na Jongo, Aga Khan ambaye hakutaka kutajwa jina gazetini, alisema alibaini kudhurika kwa mumewe baada ya kutaarifiwa na wasamaria wema.
“Nilishangaa kuona muda unakwenda na mume wangu harejei mazoezini, ilikuwa kawaida yake kufanya mazoezi ya kutembea au kukimbia alfajiri lakini jana alipitisha zaidi muda. Kumbe alikuwa amemwagiwa tindikali, inaniumiza kwa sababu tunaumizana binadamu wenyewe,” alisema.
Kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Zanzibar akienda Dar es Salaam, Shekhe Soraga alisindikizwa na Balozi Seif, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Abdallah Mwinyi na viongozi wengine wa vyombo vya ulinzi na usalama na mashekhe kadhaa.

No comments: