Saturday, November 24, 2012

DHARAU ZA MADAKTARI NA MANESI ZASABABISHA KIFO CHA MTOTO...

Mtoto wa kiume amefariki kutokana na maradhi ya uti wa mgongo baada ya madaktari wa hospitali mara mbili kushindwa kugundua dalili na kupuuza mashaka ya mama yake kama 'kupagawa'.
Huku mtoto huyo mdogo akilia kwa maumivu katika chumba cha mapumziko, nesi mmoja badala yake akashauri wazazi wake wamzungushe eneo hilo sababu alikuwa 'akipiga makelele.'
Masaa kadhaa baadaye, mtoto huyo Bobby Bushell mwenye miezi 13 akafariki dunia. Kiwango hicho kibovu cha huduma alichopokea kiliwekwa wazi juzi baada ya wazazi wake kupata fidia kutokana na madhara waliyopata kutoka kwa hospitali hiyo.
Juzi usiku mama wa Bobby, Jane Hooks alisema madaktari wa hospitali walikuwa 'kwa dharau' wakipuuza hoja kwamba alikuwa akisumbuliwa na uti wa mgongo.
"Matibabu kutoka kwa wafanyakazi wa hospitali hiyo yalipungukiwa ubinadamu na madaktari kwa dharau walitupilia mbali hofu yangu kwamba mwanangu alikuwa akisumbuliwa na uti wa mgongo - si mara moja, lakini mara mbili," alisema.
"Mtazamo wao umegharimu maisha yake. Kama wangesikiliza hofu ya mama badala ya kunipuuza kivivu kama kupagawa basi Bobby angekuwa mzima hivi sasa."
Jane alisema kwamba huku hali ya kijana wake kuendelea kudorora na kelele zake kuzidi kukatisha tamaa, nesi alimweleza kumzungusha kwa kutumia kiti cha magurudumu kama njia ya kujaribu kumnyamazisha.
"Alinifuata katika chumba kingine cha wodi ya watoto akiwa na kiti cha kukunja na kusema: "Unaweza kumzungusha kidogo? Anapiga kelele sana".
"Nilipatwa na mshituko lakini nilimweleza alikuwa akiumwa sana kiasi cha kushindwa kusimama au hata kuinua kichwa chake. Ilikuwa ni kitu kogopesha mno kusema. Masaa machache baadaye Bobby akafariki dunia."
Mkasa huo ulianzia Agosti 12, 2007 pale Bobby alipougua nyumbani kwao karibu na Doncaster.
Mama yake aliwasiliana NHS baada ya saa za kazi na kumpeleka kwenye sehemu ya upasuaji ya eneo hilo ambako daktari wake binafsi alimpima majira ya Saa 10:40 jioni.
Ingawa hakugundua maradhi ya uti wa mgongo, Daktari alimshauri Jane na mpenzi wake Craig Bushell kumpeleka Bobby katika Zahanati ya Doncaster Royal.
Waliwasili majira ya Saa 11:20 jioni na alishughulikiwa na daktari.
Licha ya kijana huyo mdogo kuwa na vipele vitatu katika mguu wake na kifuani - ambazo ni dalili za uti wa mgongo - daktari huyo aliamua tu kufuatilia hali yake.
Jane mwenye miaka 29, mfanyakazi wa zamani wa vibarua alisema: "Alisema ameathirika kidogo. Hapohapo nikamuulizia maoni ya pili. Alinieleza hata daktari wa pili atakubaliana tu na alichogundua yeye."
Jane alisema daktari wa pili, msajili, alimwona Bobby majira ya Saa 12:45 jioni na licha ya ukurutu kusambaa katika maeneo manne tofauti, pia alishindwa kugundua maradhi ya uti wa mgongo.
Alisema: "Alikuwa na dharau na mwenye kukatisha tamaa. Alikataa kumpima kama kuvunjika kiuno ambako kungeweza kugundua maradhi ya uti wa mgongo."
Ilichukua masaa mengine manne kabla Jane hajamwendea daktari mwingine kwa ajili ya msaada. "Katika kuchanganyikiwa nikamkokota daktari wa kike kwenye mkono. Alisema: "Mtoto wako anaumwa sana, tena sana"."
Bobby wakati huo alikuwa akipatiwa dawa za kupunguza maumivu lakini haikuwa kabla ya majira ya Saa 9 alfajiri ndipo daktari alipomchunguza.
Mihangaiko ikaanza kumuhamishia Hospitali ya Watoto ya Sheffield lakini walikuwa wamechelewa na akafariki Saa 12:50 asubuhi ya Agosti 13.
Familia hiyo iliishitaki hospitali hiyo lakini imekataa kuwajibika na kupinga madai hayo hadi katika mahakama kadhaa.
Mwezi uliopita Jaji alitupilia mbali pingamizi la hospitali hiyo na kuipa haki familia katika Mahakama ya Sheffield County. Iliamriwa walipwe fidia ambayo haikuwekwa hadharani lakini zaidi ya Pauni laki kadhaa.
Sewa Singh, mkurugenzi wa tiba katika hospitali hiyo alisema: "Tunatoa pole zetu na kuomba radhi kwa Jane, Craig na familia zao kwa mapungufu katika huduma na uangalizi uliotolewa kwa Bobby."

No comments: