WAZEE 500 WAUAWA KWA USHIRIKINA NCHINI...

Baadhi ya wazee wakishiriki moja ya maandamano kuadhimisha Siku za Wazee Duniani mkoani Lindi hivi karibuni.
Zaidi ya wazee 500 wanadaiwa kuuawa kila mwaka nchini kwa kukatwa mapanga kutokana na imani potofu za kishirikina hali inayofanya wazee kushindwa kufurahia amani na kuishi kwa mashaka.
Madai hayo yalitolewa jana na mwakilishi wa wazee wilayani hapa, Salome Nyoni kupitia risala kwa niaba ya wazee katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yaliyofanyika mkoani hapa.
Nyoni alidai kuwa katika mkoa wa Mwanza pekee, wastani wa wazee 138 huuawa kila mwaka kutokana na imani za kishirikina na wengine hufa kwa kukosa huduma za afya, chakula, makazi bora na kutolipwa pensheni.
Alidai kuwa changamoto inayokabili wazee hao na ambayo inachangia umasikini wa wazee hao ni janga la Ukimwi ikiwa ni pamoja na kukosa programu ya takwimu za wazee hali inayofanya wadhalilike kutokana idadi yao kutofahamika vema.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Said Amanzi alitaka wazee hao kuisaidia Serikali kuelimisha jamii kufanya mambo yanayostahili ikiwa ni pamoja na kulifanya Taifa kuwa thabiti kukemea maovu.
Amanzi alisema kwa vijana wengi hawana maadili na wanaishi miongoni mwa wazee hao na wengine ni watoto wao na wamekuwa wakiwaangalia bila kuwakemea na hivyo kulifanya Taifa kuwa na viongozi wasio waadilifu.
Hata hivyo, Mkuu huyo alitaka wazee hao kuhimiza vijana kushika maadili mema ambayo yalikuwapo tangu zamani ambayo yanafaa katika jamii ili kulifanya Taifa kuwa na amani na utulivu.
Pia alitaka wazee hao kutambua kuwa wao ni sikio, midomo na macho ya Serikali, hivyo wanatakiwa kuwa wepesi kufichua maovu kwa kulinganisha mambo yalivyokuwa huko nyuma na yalivyo sasa.
Mbunge mstaafu enzi za utawala wa Awamu ya Kwanza Issa Ramadhani alisema wakati wa uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere, kulikuwa na utaratibu wa Rais kukutana na wazee kila alipokuwa akifanya ziara mikoani.
Alidai kuwa utaratibu huo uliendelea hadi wakati wa Ali Hassani Mwinyi na ukafa wakati Benjamin Mkapa hali inayolifanya Taifa kuingia katika migogoro ya mara kwa mara na wananchi kwa kutoheshimu wazee.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani  ni "Maisha marefu yanaashiria ongezeko la wazee, tuboreshe huduma zao."

No comments: