Watu watatu wamekufa papo hapo na wengine 24 kujeruhiwa baada ya basi la kampuni ya RS Bus Express linalofanya safari zake kutoka Dar es Salaam kwenda Bukoba kugongana na lori la mizigo la kampuni ya Dhaudho (Faw) katika kata ya Ngongwa wilayani hapa.
Ajali hiyo imehusisha basi namba T 495 ATG na lori namba T 513 BNP ambalo likuwa likitoka Ushirombo, Bukombe kwenda Dar es Salaam leo saa 12.20 asubuhi.
Kwa mujibu wa Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama, Emmanuel Andrew mapka saa nne asubuhi alishapokea maiti hao watatu na majeruhi 24.
Alisema baadhi ya majeruhi wamevunjika miguu huku wanne wakiwa mahututi na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza kwa matibabu zaidi.
Mganga huyo alitaja waliokufa kuwa ni Edwin Stephano, Hamidu Yusuph ambaye alikuwa dereva wa lori na Zuraia Tuli (50) na kuongeza kuwa waliopelekwa Bugando ni Chabukana raia wa Uganda, Makame Suliman ambaye ni mwanajeshi, Fred Peter na Shafii Abdallah.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa ajali hiyo, kiini cha ajali ni dereva wa lori kumkwepa mwendesha baiskeli na kusababisha lori kuhamia upande lilipokuwa basi.
Hata hivyo, mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo, Johanes Ndyamukamu alisema kabla ya ajali kutokea, basi hilo lilikuwa likifukuzana na lingine la Sumry na baada ya kulipita ndipo lilipokutana na lori ambalo limemkwepa mwendesha baiskeli.
Kaimu Mganga Andrew alisema taarifa zingine atazitoa baadaye ili kujua kama kuna majeruhi ambao wataruhusiwa baada ya matibabu.
No comments:
Post a Comment