KIAMA CHA KUNGURU WEUSI CHAANZA RASMI LEO...

Wizara ya Maliasili na Utalii, imetangaza kuendesha kampeni ya kuangamiza kunguru weusi katika mikoa ya Tanga na Pwani kuanzia leo hadi Novemba mosi kwa kutumia sumu tulivu aina ya DRC 1339.
Taarifa ya Wizara ya Maliasili na Utalii iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana, ilieleza kuwa tangu mradi wa kudhibiti kunguru hao uanze Julai 2010 hadi Septemba 2012, kunguru 807,961 wameuawa kwa sumu hiyo na mitego katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Pwani na Tanga.
Kampeni hiyo imehamia mikoa hiyo, baada ya kukamilika Dar es Salaam ambako taarifa hiyo ilieleza kuwa kampeni hiyo iliendeshwa kwa mwezi mmoja tangu Agosti 27 hadi Septemba 25. Katika kampeni hiyo kunguru 41,487 waliuawa.
"Ingawa sumu hiyo haina madhara makubwa kwa binadamu, wananchi hasa watoto, wanatakiwa kutochezea mizoga ya kunguru. Endapo mtu atakuwa ameshika mizoga hiyo anatakiwa anawe kwa sabuni," ilieleza taarifa hiyo iliyotumwa na Msemaji wa Wizara hiyo, George Matiko.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa kunguru weusi wanauawa kwa lengo la kupunguza idadi yao, ili wasiendelee kusababisha kero kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Wizara hiyo, kunguru hao mbali na kupora vyakula na vitu vingine, wamekuwa pia wakieneza vimelea vya magonjwa mbalimbali kwa binadamu na kuku.
"Wananchi wanaombwa kutoa ushirikiano kwa vikosi vitakavyokuwa vikiokota mizoga ya kunguru, kwa kuonesha iliko. Pia wanaombwa kutoa taarifa pale watakapogundua idadi kubwa ya ndege hao sehemu yoyote ili hatua za kuwaangamiza zichukuliwe.
"Taarifa zipelekwe katika ofisi za Maliasili za mikoa, wilaya na manispaa. Pia wananchi wanaweza kupiga simu 0716 129120 kwa mkoa wa Pwani na 0757 585358 Tanga," alisema Matiko katika taarifa hiyo.
Alifafanua kuwa kampeni hiyo itahamia Morogoro Novemba 5, ambako itaendeshwa kwa mwezi mmoja pia.
Baada ya kumalizika kwa kampeni hiyo, katika mkoa huo, Matiko alisema Wizara itafanya tathmini ili kuona mafanikio ya operesheni hiyo katika mikoa yote minne ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga na Morogoro kwa kunguru wanaoonekana Dar es Salaam, ndio walewale ambao huzungukia mikoa inayopakana nao.

No comments: