Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Didas Masaburi
Utaratibu mpya wa CCM kufanya uchaguzi wake wilayani badala ya taifani ilivyokuwa awali, umeanza kuonesha mabadiliko makubwa na athari mbaya kwa vigogo wakiwamo mawaziri.Hali hiyo imejitokeza pale ambapo baadhi ya vigogo ambao katika utaratibu wa awali wasingetarajia kuangushwa katika kinyang’anyiro cha uongozi, wamejikuta ‘wakiangukia pua’.
Baada ya juzi Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye kuangushwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Uwezeshaji, Mary Nagu, Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Makongoro Mahanga naye ameangushwa na mfanyabiashara maarufu Ramesh Patel katika kinyang’anyiro cha ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).
Kana kwamba haitoshi, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Didas Masaburi naye ameambulia patupu katika kinyang’anyiro cha ujumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa. Juzi Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Amos Makala alibwagwa na Mbunge wa zamani Suleiman Saddiq Murad.
Mahanga alikuwa akigombea ujumbe wa NEC wilaya ya Ilala na kuangushwa kwa kupata kura 411 huku mpinzani wake Patel akizoa kura 664 kati ya 1,273; wengine ni Agathon Ulanga (135) na Tahadhari Ditopile (46).
Wakati Mahanga akishindwa wilayani kwake, Masaburi aliyegombea nafasi moja kati ya tano za ujumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa Ilala, alishindwa kwa kupata kura 418 kati ya 1,273.
Kwa mujibu wa Katibu wa CCM wa Wilaya ya Ilala, Ernest Chale, wagombea watano walioshinda nafasi hiyo ni Athuman Chila (689), Aisha Sururu (635), Bonah Kaluwa (516), Yona Mwasuka (461) na Patel (442).
Alisema katika uchaguzi huo nafasi ya Mwenyekiti wa Wilaya ilitwaliwa na Asaa Haroun ambaye alipata kura 1,071 kati ya 1,273 huku wapinzani wake Seleman Karanje akiambulia 190 na Vistus Stambuli tisa.
Katika nafasi mbili za ujumbe wa Mkutano Mkuu wa Mkoa walioshinda ni Ramadhan Mhagama (554) na Pili Ndimanya (434) huku wapinzani wao ambao ni Jamila Simba (419), Jumanne Pembe (285), Ayoub Msalika (274) na Yahya Dihenga (268).
Chale alisema katika nafasi nne zinazowaniwa za NEC Wanawake (UWT) wilaya, walioshinda ni Halima Kinabo (625), Siza Mazongela (579), Fatuma Masawila (561) na Situ Mwasa (475) kati ya kura 1,245 zilizopigwa wilayani hapo.
Kwa upande NEC Wazazi, Ahmada Batenga alishinda kwa kupata kura 320 na Omar Bushiri (319). Walioshindwa ni Sudi Sudi (302), Abdallah Chitanda (268), Mohammed Kapilima (250), Musa Tawaleni (233), Haruna Alphonce (179) na Dk Hussein Hassan (147).
Aidha Chale alisema katika ujumbe wa NEC Vijana, walioshinda ni Yusuph Lima (547), Asia Mponda (546), Asha Maulid (523) na Mwantumu Ditopile (507). Walioshindwa ni Frank Mangati (495), Amos Kabisa (428), Neema Kumba 408 na Shafi Mpenda 157.
Temeke Katibu wa Wilaya, Robert Kerenge, alisema nafasi ya Mwenyekiti wa Wilaya hiyo ilishikwa na Sikunjema Shaban ( 944) huku wapinzani wakiambulia kura 421 za Mbonde Mitandi na Haroun Othman (94) kati ya 1,759 zilizopigwa.
Alisema Magesa Phares alishinda ujumbe wa NEC kwa kura 623 huku wenzake waliomfuatia ambao ni Mangungu Mohamed (580), Mbwana Bauj (409) na Bulimba Bulimba (47).
Kuhusu Katibu wa Siasa na Uenezi wa Wilaya, Chisumo Masunu alipata kura 100 wapinzani wake ambao ni Kisinga Salum (48) na Licheku Ahmed (8) walishindwa na katika nafasi moja ya Katibu wa Uchumi na Fedha mshindi ni Hazal Issa aliyepata kura 132.
Kerenge alisema kwa nafasi 10 zinazowaniwa za ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM wilaya walioshinda ni Mwandishi wa Habari Mwandamizi wa Radio Uhuru, Angela Akilimali (728), Chicago Mwanakombo (742), Hazal Issa (535), Kuchilingulo Mindim (573) na Mangalia Abdallah (1,018).
Wengine ni Dora Mwamkinga kupitia UWT(985), Myovela Elimina (918), Shirafu John (927), Mangwela Fortunatus (296) na Makele Mohamed (257).
Katika nafasi mbili zinazowaniwa za ujumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa walioshinda ni Chikwindo Abdallah (595) na Sijaona Selema (355).
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa walioshinda ni Mlawa Amiri (487), Maganga Hadija (472), Kanyopa Joachim (445), Zahoro Hemed (444) na Mpanjila Aisha (437).
Kutoka Monduli Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa alishinda ujumbe wa NEC kwa kupata kura 709 kati ya 760. Katika kinyang’anyiro hicho, Dk Salash Toure alijitoa, na kumwachia Nanai Konina aliyepata kura 44 lakini Dk toure alipigiwa kura saba.
Msimamizi wa uchaguzi huo Athuman Sheshe alisema kwa mujibu wa taratibu, hata kama mgombea ametangaza kujitoa jina lake linapigiwa kura.
Kutoka Nzega, Ofisa Mtendaji Mkuu wa New Habari Coperation, Hussein Bashe alitoa machozi baada ya mtu aliyekuwa anataka apite katika nafasi ya uenyekiti kuanguka na kulazimika kuondoka bila kusubiri matokeo yaliyochukua zaidi ya saa 20 hadi kutangazwa matokeo.
Hali hiyo iliyotokea baada ya Bashe kupata habari kutoka chumba cha kuhesabia kura kwamba Mwenyekiti Francis Shija alipata kura 588 kitendo ambacho kilimkasirisha na kuondoka bila kusubiri matokeo yake ingawa alipita katika ujumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa.
Kutokana na kambi hiyo kushindwa wananchi wa kijiji anachotoka Mwenyekiti aliyeangushwa, wananchi wa kata ya Itobo walishusha bendera za Chadema na kupandisha za CCM
Msimamizi wa uchaguzi huo Emmanuel Gembe alimtangaza Amosi Kanuda kuwa mwenyekiti mpya baada ya kupata kura 1,486. Kwa upande wa NEC, Yassin Memba alipita. Bashe alizoa kura 1,459, Ahmed Nassoro (824), Paul Kabalele (734), Sakina Bundala (719) na Paschal Manyanda (502).
Katika wilaya ya Tabora Manispaa aliyechaguliwa kuwa Mwenyekiti ni Moshi Konkota
na mjumbe wa NEC ni John Mchele.
Kutoka Lindi, Mke Rais, Mama Salma Kikwete alipita bila kupingwa katika ujumbe wa NEC.
Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi Lindi Mjini Katibu wa CCM wa Mkoa wa Lindi, Adolina Gesi alimtangaza Mama Salma kuwa alikubaliwa na wajumbe 655.
Vuta nikuvute ilikuwa katika uenyekiti wa wilaya ikiwakutanisha Rafii Muhsin, Manyanya Nasibu
na Abdallah Livembe ambapo Gesi alitangaza mshindi kuwa ni Muhsin aliyepata kura
476 akiwabwaga Nasibu (38) na Livembe (138).
Kuhusu wajumbe wa wilaya katika mkutano mkuu CCM Taifa washindi ni Abdallah Pamba na Ali Gwaja miongoni mwa wagombea wanane na katika ujumbe wa mkoa waliochaguliwa ni Mwajuma Amiri na Mwanakombo Abdallah.
Kutoka Kahama, Ofisi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Kahama ilipigwa kufuli na baadhi ya wanachama tangu juzi baada ya uchaguzi kufanyika wakishinikiza kura za wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa zirudiwe.
Baadhi ya wanachama walidai kwamba kura zilizopigwa wakati wa uchaguzi baadhi ya wagombea waliingia katika chumba cha kuhesabia na kuzibadilisha.
Hata hivyo waliotangazwa washindi ni Mwenyekiti Mabala Mlolwa, wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa ni Benson Mpesya, Omary Mziya, Matilda Msoma, Getrude Izengo na Jackson Lutego. Wengine ni Catherine Dalali ujumbe wa NEC, Isaya Simon Katibu wa Uchumi na Fedha na Katibu wa Itikadi na Uenezi ni Masoud Melimeli.
Kutoka Musoma, wilaya za Musoma Mjini na Butiama mkoani Mara zilipata viongozi ambapo kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa jana alfajiri na Msimamizi Amos Sagala, Daud Missango aliibuka mshindi wa uenyekiti wa wilaya kwa kupata kura 225 dhidi ya Isack Chacha (133).
NEC Vedastus Mathayo aliibuka mshindi kwa kupata kura 346, Mkutano Mkuu Taifa nafasi tano zilichukuliwa na Juma Ebambo, Joseph Obeto, Christina Samo, Said Meko na Abdallah Malima.
Ujumbe wa Halmashauri Kuu Wilaya , kundi la Wazazi waliopita ni Edgi Manyama na Dinnah Samanyi; Wanawake ni Samo, Samanyi, Twaiba Mussa na Veronica Kunenge, huku Vijana wakipita Haji Mtete, Mohamed Mussa, Magori Chacha na Idrisa Hussein. Mkutano Mkuu Mkoa ni Godwin Kumila na Samanyi.
Msimamizi wa Uchaguzi wa Wilaya ya Butiama Jackson Mang’ula alimtangaza Yohana Mnema kuwa Mwenyekiti baada ya kumbwaga wa zamani, Nyabukika Nyabukika katika uchaguzi uliokuwa na wajumbe 1,362. NEC ni Christopher Siagi; Mkutano Mkuu wa Mkoa ni Nestory Matiko na Rudia Mazera.
Mkutano Mkuu wa CCM Taifa kupitia wilaya ni Nyabukika, Jerome Masawe, Bracias Chuma, Bhoke Ngurube na Rashid Gewa; Katibu wa Siasa na Uenezi wa Wilaya ni Ntobi Ntobi na Katibu Uchumi na Fedha ni Baraka Imani ‘Obama’.
Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Wilaya kundi la Wazazi wote walipita bila kupingwa, nao ni Fidelis Iginge, Wambura Kishamuri, Hehonyo Hehonyo, John Nyamisana, Ibrahim Makange na James Matongo; Wanawake ni Tabitha Idd, Wegesa Witimu, Mwajuma Magoti na Bhoke Ngurube. Vijana hawakupigiwa kura kutokana na walioomba kukosa sifa kwa kuwa umri wao ulizidi.
No comments:
Post a Comment