UDINI WATAWALA MAONI YA KATIBA MPYA...


Katika moja ya mapendekezo hayo, wametaka vazi la hijab lipigwe marufuku maofisini.
Uhuru uliotolewa wa kutoa maoni yoyote ili kuunda Katiba ijayo kwa manufaa ya Watanzania wote, umetekwa na viongozi wa makanisa na misikiti, ambao wametuma waumini wao kutoa maoni ya kutetea misimamo ya dini husika iingie au isiingie katika Katiba.
Hali hiyo imejidhihirisha wiki iliyopita mkoani Ruvuma na hasa katika Wilaya ya Songea mjini, ambapo Tume ya Kukusanya Maoni ya Katiba Mpya, ilijikuta ikisikiliza maoni ya aina moja yakijirudia zaidi ya mara kumi katika kila mkutano huku watoaji wa maoni hayo wakionesha kutumwa kuwakilisha maoni waliyotumwa. 
Katika maoni hayo, waliotetea Uislamu na Ukristo walikubaliana katika maoni kuwa Serikali haina dini lakini watu wake wana dini na kusisitiza Serikali isingilie uhuru wa kuabudu wa mwananchi.
Hata hivyo wakati wakisisitiza kuwa Serikali haina dini, waumini hao walijikuta wakitoa maoni kutaka Serikali isiyo na dini itambue dini zao na kutii matakwa yao yanayopinga kinachodaiwa ni maslahi ya dini nyingine.
Waislamu katika matakwa yao, walisisitiza Serikali pamoja na kutokuwa na dini, iajiri watumishi kwa uwiano sawa kwa kuzingatia dini na kugawa maeneo vikiwemo viwanja na majumba yasiyotumika kwa usawa huo huo.
Mbali na kusisitiza madai ya siku nyingi ya Waislamu ya kutaka Mahakama ya Kadhi na Tanzania kujiunga na Umoja wa Nchi za Kiislamu (OIC), pia walipendekeza kufutwa kwa Wimbo wa Taifa na siku ya Ijumaa kuwa ya mapumziko kama Jumapili na Jumamosi, au itafutwe siku nyingine ya mapumziko lakini siyo Ijumaa, Jumamosi na Jumapili.
Kumejitokeza pia madai ya kutaka usawa katika siku za sikukuu za dini, yaani Idd El Fitri na Idd Al Haj zipewe siku za mapumziko zaidi ya tano kwa kila sikukuu na kutambuliwa kwa Mwaka Mpya wa Kiislamu.
Katika kutetea hoja hiyo, mkazi wa Kata ya Lizaboni, Haji Nditi (44), alipendekeza siku za kupumzika za Serikali ziwe katikati ya wiki. 
Nditi alisema pendekezo lake, linalenga kuondoa ubaguzi wa siku za kuabudu kwa madai kuwa Ijumaa ambayo ni Siku ya kuabudu kwa Waislamu, imebaguliwa kwa kuwa siku ya kazi wakati Jumamosi na Jumapili, zimependelewa kuwa za mapumziko.
Hata hivyo mmoja wa Waislamu ambaye hakutaka kutajwa jina, akizungumza na gazeti hili, alifafanua kuwa hoja hiyo si kwa mujibu wa Korani, kwa kuwa kitabu hicho kitakatifu, kimeagiza baada ya Ibada, Waislamu watawanyike kwenda kutafuta riziki.
Mkazi wa Mji Mwema, Salehe Seif alisema Mahakama ya Kadhi inapaswa kutambuliwa na Katiba ili ipate nguvu ya utendaji, ikiwemo kukamata Waislamu wanaokaidi amri zake.
Alisema pia si busara Muislamu kufungishwa ndoa na Abdalah (Shehe msikitini) na kuvunjwa kwa ndoa hiyo, kufanywe na Paulina (Hakimu mahakamani).
Mkazi wa Kata ya Makumbusho, Ally Kumchoma (52), alisema kuwa Kadhi asipotambuliwa na Katiba, akitoa hukumu inaweza isitekelezwe kwa kuwa hatambuliki kiserikali na anaweza hata kushitakiwa.
Kuhusu kujiunga na OIC, Seif alisema kutasaidia Waislamu na wasio Waislamu kupata mikopo bila riba ambayo ni neema kwa wote.
Mkazi wa Kata ya Makumbusho, Yahaya Mpingi (52) alipendekeza Mwaka Mpya wa Kiislamu utambulike na kuwe na mapumziko kama mwaka mpya uliozoeleka na kutaka Serikali iajiri Wakristo nusu na Waislamu nusu.
Mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Chuo Kikuu cha St Augustino, Jasmin Ulambo (22), alipendekeza vazi la Hijab liheshimiwe na katika Sensa ya Watu na Makazi, kipengele cha dini kiwepo.
Mkazi wa Kata ya Majengo, Nahodha Mpaka (76), alipendekeza Serikali isiingilie uhuru wa kuabudu na kutoa mfano wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), kwamba limeundwa na Serikali kudhibiti Waislamu.
Hamisi Njovu (36), mkazi wa Kata ya Majengo, alipendekeza OIC Tanzania ijiunge lasivyo ijitoe Vatican.
Hata hivyo hakufafanua kwa nini Tanzania imuondoe Balozi wa Vatican ambayo ni nchi ya kidini na isimuondoe Balozi wa  Iran ambayo pia ni nchi ya kidini. 
Njovu pia alipendekeza Wimbo wa Taifa ufutwe kwa madai kuwa ni wa dini moja. Alipoulizwa na Profesa Baregu afafanue, alisema Mungu Ibariki Tanzania, ni wimbo unaotumika makanisani wakati wakianza ibada.
 Alitaka pia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya utambue wake wanne na watoto wanaotokana na wake hao kwa kuwa Waislamu wameamrishwa kuoa wake zaidi ya mmoja.
Mkazi wa Kata ya Bomba Mbili, Abdul Ramadhani (74), alisema Sikukuu ya Pasaka, ina siku sita, yaani Jumatano ya Majivu, Alhamisi Kuu, Ijumaa Kuu, Jumamosi, Jumapili na Jumatatu ya Pasaka ambazo Wakristo hupumzika. Alisema Waislamu katika Idd, wamekuwa wakipewa siku moja au mbili na kutaka kuwe na usawa.
Wananchi wengi waliotoa maoni walitaka uhuru wa kuabudu kama ulivyo katika Katiba ya sasa, ubaki hivyo hivyo na kupinga kufutwa kwa Wimbo wa Taifa, Tanzania kujiunga OIC na Mahakama ya Kadhi kuingizwa katika Katiba.
Pia walipinga vazi la Hijab kuvaliwa katika ofisi za Serikali, ajira kwa kuzingatia vigezo vya dini na kupendekeza uchaguzi usifanyike siku za ibada ikiwemo Ijumaa, huku wakifafanua kuwa umekuwa ukifanyika mara nyingi Jumapili.
Hata hivyo hawakufafanua kwa nini wanapinga uchaguzi siku hiyo, wakati ibada za Wakristo Jumapili hufanyia nyingi katika nyakati tofauti kuruhusu watu kuchagua muda wa kuingia ibadani na muda wa kwenda kazini.
 Ayubu Bilal wa Kata ya Majengo, alisema machinjio yameshikwa na dini moja na visu vimeandikwa Bismillah na kupendekeza upande mwingine wa visu uandikwe Kwa jina la Baba, la Mwana na Roho Mtakatifu. 
Hata hivyo tofauti na ilivyo kwa Waislamu, Wakristo hawana mwiko wa kuchinja na hata akichinja Muislamu, Mkristo atakula nyama bila wasiwasi.
Mkazi mwingine wa kata hiyo, Charles Wambura, aliyeanza na salamu ya Bwana Yesu ni Mkombozi wa Dunia, apewe sifa, alipinga suala la OIC, alisema haipaswi kuhusisha nchi, hasa kwa sababu ya misaada, badala yake ijulikane na upande wa pili wa hasara kabla ya kuamua.
Naye Daniel Sanga (27),  alipendekeza Mahakama ya Kadhi isiingizwe katika Katiba na Tanzania isijiunge na OIC. 
Katika Kata ya Majengo, baadhi ya wanawake walichukua fomu za kutoa maoni ya Katiba kwa maandishi na kumpa mtu mmoja, aliyeandika kwa niaba yao maoni yaliyofanana, jambo ambalo Tume ililishtukia na kuziweka sehemu moja ili zitambuliwe kama maoni ya mtu mmoja. 
Tume, katika timu iliyokuwa na wajumbe watatu; Profesa Baregu, Al Shaimar Kwegyir na Alli Saleh, ilikamilisha kazi ya kukusanya maoni mkoani Ruvuma mwishoni mwa wiki ambapo Jumatatu ya wiki ijayo, itaanza kazi hiyo katika mikoa mingine.

No comments: