Kampuni 12 zinazoagiza mafuta kutoka nje ya nchi zimepigwa mweleka baada ya kutupiliwa mbali kwa rufaa zilizoifungua dhidi ya Mamlaka ya Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kutaka kubatilisha uamuzi wa kushusha bei ya nishati hiyo.
Katika uamuzi wa rufaa hiyo uliotolewa Septemba 24 mwaka huu na Baraza la Ushindani wa Haki za Kibiashara (FTC) chini ya uenyekiti wa Jaji Razia Sheikh, zimetakiwa kulipa gharama za kesi baada ya rufaa hiyo kuonekana haina hoja.
Baraza limesema katika shauri hilo la rufaa iliyofunguliwa mwaka jana, Ewura ambayo ni mlalamikiwa, ilifanya mapitio ya kanuni ya bei kwa kuzingatia sheria na taratibu.
Kampuni zilizokata rufaa ni BP Tanzania Limited, Engen Petroleum Tanzania Limited, Camel Oil Tanzania Limited, Oilcom Tanzania Limited, Total Tanzania Limited, Gapco Tanzania Limited na Hass Petroleum Tanzania Limited.
Nyingine ni ORYX Oil Company Limited, MGS International Tanzania Limited, GBP Tanzania Limited, Lake Oil Limited, Moil Tanzania Limited na Acer Petroleum Tanzania Limited ambazo zilitaka uamuzi wa Ewura wa Agosti mwaka jana wa kushusha bei ya mafuta ubatilishwe.
Kwenye rufaa hiyo ambayo kampuni ziliwakilishwa na Wakili Madina Chenge, mbali ya kupinga uamuzi huo wa kushusha bei ya mafuta, pia zilitaka FTC ibatilishe amri ya utii ya kuzitaka kuuza mafuta kwa bei hiyo mpya, iliyotolewa Agosti 9. Ewura iliwakilishwa na Wakili Galeba.
Zilidai kwamba, Ewura ilikiuka sheria kwa kushindwa kuangalia gharama za usambazaji wa mafuta nchini, hivyo uamuzi na amri iliyotolewa na mamlaka hiyo ubatilishwe au walipe gharama.
Hata hivyo katika uamuzi wake, Baraza la Ushindani wa Haki za Kibiashara limesema limeridhishwa kwamba mrufani (kampuni) alipewa nafasi ya kusikilizwa kabla ya marekebisho ya bei.
FTC ilisema kwamba imebaini Ewura ilitumia mamlaka yake kama mdhibiti wakati akitengeneza kanuni ya bei mpya kwa mafuta yanayouzwa na kampuni hizo.
Uamuzi huo wa Baraza ulisema warufani hawakuonesha kwa takwimu ni namna gani bei hiyo mpya iliwaathiri kifedha. Hoja kuhusu hali ya kifedha ilitajwa kuwa haijitoshelezi na si bayana. Baraza limeona Ewura isingeweza kutilia maanani wawekezaji bila kuangalia maslahi ya walaji na uchumi wa taifa.
Imeelezwa pia kwamba wakata rufani walipaswa kupeleka ushahidi kuthibitisha ni namna gani waliathirika na bei hiyo elekezi.
“Hakuna ushahidi kabisa kuonesha hasara iliyoingiwa na warufani,” ilisema sehemu ya hukumu hiyo na kusisitiza kwamba kampuni hizo ziliendelea na biashara na kusambaza bidhaa za petroli.
Ilifafanuliwa pia kwenye uamuzi huo kwamba kwa kuwa bei hiyo ilikuwa ikigusa nchi nzima, Baraza haliwezi kukubaliana na warufani kwamba bei iliathiri ushindani.
“Kama kungekuwepo kanuni tofauti kwa wadau wa biashara hii, hii ingewezekana kusababisha ushindani usio haki,” ilisema sehemu ya uamuzi huo na kufafanua kwamba wasambazaji hao wa mafuta walikuwa na uhuru wa kuuza kwa bei yoyote wanayoipenda ili mradi hawavuki bei elekezi ya Ewura .
Baraza lilisema hoja kwamba kampuni hazikuridhishwa na bei, haimaanishi kwamba Ewura ilifanya uamuzi bila kuzingatia maslahi ya warufani hao. Limesema katika kutekeleza majukumu yake, Ewura haiwezi kumpendezesha kila mdau.
FTC imefafanua kwamba anachofanya mdhibiti ni kutekeleza uamuzi kwa kuzingatia sheria na taratibu na kuwianisha maslahi ya wadau wote katika biashara hiyo ya mafuta.
No comments:
Post a Comment