FREDERICK SUMAYE ABWAGWA UCHAGUZI WA CCM...


Frederick Sumaye.
Matokeo ya uchaguzi wa ngazi mbalimbali ndani ya Chama Cha Mapinduzi yameanza kutoka huku baadhi ya mikoa majina maarufu yakipoteza nafasi kwa wagombea wasiokuwa na majina.
Taarifa kutoka kwa waandishi wetu mbalimbali, wanasiasa wengine walioingia baada ya kukaa nje kwa muda nao wameonesha ushindani mkubwa..
Baadhi ya majina makubwa yaliyopoteza  uchaguzi ni Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye, Naibu Waziri wa Habari Vijana Utamaduni na Michezo Amos Makalla  na Mbunge wa Jimbo la Igalula Dk Athumani Mfutakamba aliyeambulia kura 231 akiangushwa na Mtendaji wa Kata.
Aidha Mbunge wa zamani wa Jimbo la Nyamagana, Lawrence Masha, amepata ushindi wa kishindo na kuivaa nafasi Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC).Pia mtoto wa mwanasiasa mkongwe nchini John Malecela ameukwaa Ujumbe wa NEC Wilaya ya Chamwino
Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Uwezeshaji Dk Mary Nagu ambaye pia ni Mbunge wa Wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara ameibuka kidedea na kumshinda mpinzani wake Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye.
Msimamizi wa uchaguzi huo Elaston Mbwilo alisema kuwa  Dk Nagu aliibuka kidedea kwa kupata   kura 648  ambapo mpinzani wake Frederick Sumaye  aliambulia kura 481 kati ya kura 1129 zilizopigwa ambapo kura 41 ziliharibika. 
Wajumbe wa Mkutano Mkuu  wa Halmashauri Kuu ya Wilaya ya Hanang’  ni  Mkuu wa Wilaya ya Hanang’ Christina Mndeme, Anju Mang’ola, Mateo Darema na Hawa Hussein. 
Mwenyekiti wa (CCM) Wilaya ya Hanang’  atakuwa Michael Bayo baada ya kuwashinda wapinzani wake Goma Gwaltu  na Hassan Hilbagroy. 
Mtoto wa mwanasiasa mkongwe nchini John Malecela ameukwaa Ujumbe wa NEC Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.
Akitangaza matokeo hayo Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma Mjini Albert Mgumba alisema kuwa,  Mussa Abdi alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa kwa  Wilaya ya Kongwa, kwa kupata kura 836 na nafasi ya NEC ilikwenda kwa Godwin Mkanwa.
Katika Wilaya ya Chamwino nafasi ya Mwenyekiti wa Wilaya ilitwaliwa na Ulanga Benjamini  kwa kura 776 na nafasi ya Ujumbe NEC  ilikwenda kwa Malecela Samweli John aliyepata kura 727 .
Wilaya ya Mpwapwa ,John Chigwile alichaguliwa kuwa Mwenyekiti huku nafasi ya NEC Mpwapwa ikienda kwa Mbunge wa zamani George Lubeleje .
Katika Wilaya ya Chemba Mwenyekiti ni Alhaji Issa Mlalo aliyepata kura  867 huku Juma Nkamia akichukua nafasi ya NEC kwa kura 602.
Katika Wilaya ya Kondoa kura zilipigwa mara mbili ambapo Athuman Gola alipata kura 639 na kumshinda  Mohamed Kova aliyepata kura 533 , nafasi ya NEC, ilikwenda kwa Mohamed Lujuo aliyepata kura 893 .
Mbunge wa zamani wa Jimbo la Nyamagana, Lawrence Masha, amepata ushindi wa kishindo na kuivaa nafasi Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), wilayani Nyamagana, mkoani Mwanza. 
Sambamba na Masha, wanahabari Raphael Shilatu, Flora Mgabe na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga, pia wameibuka na ushindi mnono katika Uchaguzi Mkuu wa CCM wa Wilaya hiyo, uliofanyika jana katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu Butimba huku Shilatu akichaguliwa kuwa Mwenyekiti wake mpya.
Katika Wilaya ya  Ilemela, Nelson Mesha aliibuka na ushindi mnono wa kura 352 na kuwa Mwenyekiti mpya wa Wilaya nafasi ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu CCM Taifa  wa Ilemela ilichukuliwa na Israel Mtambalike kwa kura 584, huku Musa Magabe akichaguliwa tena kuwa Katibu Mwenezi kwa kura 43 dhidi ya Mwashumu Ismail (14) na Athuman Mfungo kura moja.  
Naye Mbunge wa zamani wa Jimbo la Morogoro, Suleiman Saddiq Murad  amechaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa kumshinda  Naibu wa Waziri wa Habari ,Vijana, Utamaduni na Michezo Amos Makalla ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mvomero. Katika uchaguzi huo, Murad alipata kura 648  wakati  kwa Makalla alijipatia 371 .
Mkutano huo ambao ulihudhuriwa na wajumbe 1,030, pia walimchagua Abdallah Mtiga kwa kura 674 kuwa Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya hiyo.
Kwa upande wa Wilaya ya Morogoro mjini Kichama , Mbunge wa Jimbo hilo,  Abdulaziz Abood aliweza kutetea nafasi ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa baada ya kuwashinda wapinzani wake Amina Mhina na Kevin Njunwa.
Katika Wilaya ya Ulanga, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Furaha Lilongeri,alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM.
Wakati nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ikinyakuliwa na Halid Nalyioto.
Huko Tabora, Dk Athumani Mfutakamba jana ameangukia pua Uyui baada ya kushindwa katika uchaguzi wa CCM , nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu  ya Taifa (NEC)  anaripoti Lucas Raphael. Nafasi hiyo imetwaliwa na Mlolwa Beatus ambaye alipata kura 769 wakati Athumani Mvutakamba alipata kura 231.
Katika Jimbo la Urambo Mashariki aliyekuwa Waziri wa Wanawake , Jinsia na Watoto Margaret  Sitta aliibuka kidedea nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa. Na Urambo Magharibi UNEC ulienda kwa Profesa Juma Kapuya . 
Katika uchaguzi wa Tarime mkoani Mara, Mwita Gachuma alimbwaga mpinzani wake Mairo Marwa Wansaku kwa Gachuma  kupata kura 1,091 katika nafasi ya NEC Tarime, Mairo alipata kura 180  anaripoti Samson Chacha.
Katika Wilaya ya Rorya,  Thobias Rayar alipata kura 362 na kuwashinda wapinzani wake Lucio Ambogo na   Kulundege.

No comments: