Friday, October 19, 2012

KIKUNDI CHA UAMSHO ZANZIBAR CHADAIWA KUUA POLISI...

Kamanda Mussa Ali Mussa.
Wakati Watanzania wakiwa bado na majonzi ya kuuawa kwa aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, mauaji mengine ya polisi yametokea Zanzibar.
Safari hii katika tukio la juzi usiku, askari F2105 Koplo Said Abdul-rahman Juma (41) wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Mkoa wa Mjini Magharibi, ameuawa kwa kukatwa mapanga kichwani na mikononi wakati akiwa njiani kurudi nyumbani kwake eneo la Bububu.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Ziwani jana, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema mauaji hayo yaliyofanyika saa 6.30 usiku yalisababishwa na fujo za wafuasi wa Jumuiya ya Uamsho baada ya kuenea uvumi wa kutekwa kwa Msemaji Mkuu wa Jumuiya hiyo, Shekhe Farid Hadi usiku wa kuamkia juzi.
Kamishna Mussa alisema Polisi inaendelea na msako dhidi ya watu waliofanya mauaji hayo ili kuwakamata na kuwafikisha mahakamani.  
Alisema hadi jana, watu 10 walikuwa wamekamatwa kwa tuhuma mbalimbali zilizotokana na vurugu za juzi na upelelezi wa kujua ukweli juu ya uvumi wa kutekwa Shekhe Farid unaendelea.
Kamishna Mussa alisema taarifa za kutekwa kwa Shekhe Farid zinatia shaka kutokana na mazingira ya kutoweka kwake, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mdogo wake, Said Omar Said ambaye alikuwa dereva wake kabla ya kutoweka maeneo ya Mazizini walikokwenda kununua umeme.
“Shekhe Farid alimtaka Said amwache eneo hilo na apeleke umeme nyumbani huku yeye akibaki  kuzungumza na watu wengine waliokuwa ndani ya gari lingine aina ya Noah ambalo namba zake hazijajulikana, lakini aliporudi kumchukua hakumkuta,” alisema Kamishna Mussa.
Alisema fujo hizo zilisababisha hasara kubwa kwa Serikali, CCM na wananchi ikiwamo kuchoma na kuharibu miundombinu ya barabara na kuchoma maskani za CCM za Kisonge na Mwembeladu. Pia baadhi ya magari yalivunjwa vioo, pia duka la pombe lilivunjwa na mali iliyokuwa ndani kuibwa.
Hata hivyo, Kamishna Mussa alisema hali ya Zanzibar jana ilikuwa shwari na wananchi walikuwa wakiendelea na shughuli zao kama kawaida. Aliahidi kuwa Polisi kwa kushirikiana na vikosi vingine vya ulinzi na usalama, wataendelea kuhakikisha amani inadumu muda wote.
Alitaka wananchi kuendelea kuwa wavumilivu na kudumisha amani na utulivu katika maeneo yao na kutoa taarifa za watu waliohusika na vurugu na mauaji ya Koplo Said.
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa CCM, wameitaka Serikali kulipa fidia mali zote zilizoharibiwa na wafuasi wa Jumuiya ya Uamsho na kuruhusu vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuweka ulinzi na usalama ili maafa zaidi yasitokee.
Pia wametaka mamlaka inayohusika ndani ya Serikali kuifuta Jumuiya hiyo kwa vile inakwenda kinyume na malengo na dhamira ya kuanzishwa kwake.
Akizungumza jana Mbweni katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Mwakilishi Hamza Hassan Juma kwa niaba ya wawakilishi wa CCM, alisema Jumuiya ya Uamsho si chama cha siasa, ni jumuiya ya kidini lakini imeonekana kukosa mwelekeo.
Alisema kwa sasa jumuiya hiyo inafanya vitendo vinavyofarakanisha waumini wa dini hiyo, kuwagawa na kuidhalilisha dini yenyewe ya Kiislamu.
Juma alisema waliunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuondoa  kasoro zilizokuwapo na kusababisha wananchi kuishi kwa amani na usalama na kuondoa tofauti zao za kisiasa.
Alisema hawakutarajia kufika mahali Zanzibar iwe sawa na nchi zenye machafuko na kufanya wananchi washindwe kuishi kwa amani na salama na kuonya kuwa Serikali haitakaa kimya kwani itasababisha sura mbaya kwa wananchi.
Kutokana na hali hiyo, wajumbe hao waliitaka Serikali mara moja kuwachukulia hatua waliohusika na ghasia hizo na kuwafikisha katika vyombo vya sheria na kumtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi  Nchini (IGP), Said Mwema na makamanda wake kuwajibika  moja kwa moja katika suala hilo ili kukomesha mambo hayo.
Imeripotiwa kwamba matukio ya kuvamiwa makanisa na kufanyika uharibifu yameendelea kujitokeza Dar es Salaam, baada ya jana kuvamiwa mawili na kufanyika uharibifu wa mali na mtu kujeruhiwa na wavamizi hao.
Katika tukio la kwanza watu wanane wasiofahamika, walivamia Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Yombo Kuu,  saa nane usiku na kutaka kwenda madhabahuni, lakini kabla ya  kutenda uhalifu waliodhamiria walizuiwa na mlinzi wa Kanisa hilo, Daniel Nkya.
Baada ya kuzuiwa, wanne waliruka ukuta na kuingia kanisani humo na wengine kuingilia getini, na kumvamia mlinzi huyo mwenye umri wa miaka 52 na kumpiga rungu kichwani na mkononi na kumjeruhi.
Tukio hilo lilishuhudiwa na mlinzi mwingine wa Kanisa hilo, Richard Temba ambaye alikimbia na kwenda kupiga kengele ya Kanisa, jambo ambalo lilifanya wavamizi hao kutimua mbio na kutokomea.
Akizungumza na gazeti hili kanisani hapo jana, Mchungaji Kiongozi wa Usharika huo wa Yombo Kuu, Joshua Jaha alisema baada ya kupewa taarifa ya tukio hilo alitoa taarifa Polisi na askari walifika na kufanya uchunguzi wa awali na kuondoka na baadhi ya vitu ambavyo vinaweza kusaidia uchunguzi mbali na kumhoji Nkya.
Baada ya hapo Nkya alipelekwa katika hospitali ya Amana ambako alipatiwa matibabu na kuruhusiwa  na kwa mujibu wa Mchungaji Jaha, hali yake inaendelea vizuri.
“Katika hali kama hii iliyopo hivi sasa ya matukio ya uchomaji makanisa kama ilivyotokea Mbagala, ni vigumu kubaini  nani anahusika na tukio hili ingawa naweza kusema wavamizi hawa hawakuwa vibaka, kwani wangekuwa vibaka wangekwenda moja kwa moja ofisini ambako ndiko vitu mbalimbali hutunzwa,” alisema.
Hadi Saa 10 jioni askari Polisi saba walikuwa wanaendelea kuimarisha ulinzi kanisani hapo.
Katika tukio la pili, Kanisa la Faraja International Gospel lililopo Yombo Makangarawe vifaa vyake vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni tano viliungua, baada ya moto kuibuka saa saba usiku wa kuamkia jana.
Kwa mujibu wa Mchungaji wa Kanisa hilo, Yohana Kusaga,  moto huo ambao chanzo chake hakijulikani haujulikani ulianza saa saba usiku na majirani waliubaini na kupiga simu kumjulisha kuwa Kanisa lake limeshika moto na akafika na kuijulisha Polisi ambao walifika na watu wa Zimamoto na Tanesco.
Mchungaji Kusaga alisema moto huo ulizimwa na majirani ambao walivunja sehemu ya ukuta na kutupa mchanga sehemu ulikokuwa na kuuzima ingawa vitu vilivyokuwa juu ya meza hiyo ambavyo ni mixer, amplifaya na vipaza sauti 10 viliteketea.
Kwa mujibu wa Mchungaji Kusaga, Tanesco walifika eneo la tukio na kubainisha kuwa moto huo haujasababishwa na hitilafu ya umeme, hivyo kufanya tukio hilo kugubikwa na utata na Polisi walichukua mabaki ya vifaa hivyo kwa uchunguzi zaidi.

No comments: