Friday, October 19, 2012

SHEKHE PONDA NA WENZAKE 46 WAFIKISHWA KORTINI KWA UCHOCHEZI...

Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Shekhe Ponda Issa Ponda (wa pili kushoto) na wafuasi wake 49 wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana ambako wameshitakiwa kwa tuhuma za uvamizi wa kiwanja cha Kampuni ya Agritanza kilichopo Chang’ombe, kufanya vurugu, kuharibu mali na uchochezi uliosababisha uvunjifu wa amani. Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa jumla ya vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 56 viliibwa.
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Shekhe Ponda Issa Ponda na wafuasi wake 49 akiwamo bibi wa miaka 100, Zaida Yusufu, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashitaka matano yakiwamo ya uchochezi na wizi.
Walifikishwa jana mahakamani hapo na baada ya kusomewa mashitaka na kukana,  walirudishwa rumande kwa sababu hakimu aliyepangiwa kusikiliza kesi hiyo, hakuwapo na hivyo ikasomwa mbele ya   ambaye alisema hana mamlaka.
Kwa upande wa Shekhe Ponda, Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) aliwasilisha hati ya kuzuia dhamana yake  kwa madai kuwa ni kwa usalama wake na kwa maslahi ya Jamhuri.
Wafuasi hao 49 walifikishwa mahakamani hapo saa 5.15 asubuhi huku wakiimba ‘Takbir… Allah Akbar (Mungu mkubwa) ’ na walipokuwa wakishushwa kwenye gari la Polisi wengine walibebwa wakionekana kuwa na maumivu.
Ilipofika saa 6.20 mchana huku wanahabari wakiwa wametanda kila mahali kupata picha, Shekhe Ponda aliletwa akiwa katika msafara wa magari ya Polisi baadhi yakiwa na ving’ora likiwamo gari la maji ya kuwasha.  
Baada ya kushushwa, Ponda alipelekwa moja kwa moja katika chumba cha mahakama na kuunganishwa na washitakiwa wenzake.  
Wafuasi  hao pamoja na Shekhe Ponda walisomewa mashitaka na Wakili wa Serikali, Jumanne Kweka mbele ya Hakimu Stewart Sanga. 
Katika mashitaka hayo, wote kwa pamoja walidaiwa kuwa Oktoba 12 walikula njama ya kutenda kosa  eneo la Chang’ombe Markasi wilayani Temeke, Dar es Salaam. 
Ilidaiwa wakiwa Chang’ombe, walivamia kwa nguvu katika kiwanja kinachomilikiwa na kampuni ya Agritanza kwa nia ya kujimilikisha isivyo halali.  
Kweka alidai Shekhe Ponda na wenzake katika hali ya uvunjifu wa amani na isivyo halali, walijimilikisha mali hiyo halali ya Agritanza. 
Katika mashitaka ya nne ambayo ni ya wizi, ilidaiwa kuwa kati ya Oktoba 12 na 16, washitakiwa waliiba vifaa vya ujenzi katika kiwanja hicho vyenye thamani ya Sh  milioni 59.6 ambavyo ni kokoto, nondo na saruji mali ya kampuni hiyo.
Katika mashitaka yanayomkabili Shekhe Ponda peke yake, ilidaiwa kuwa katika maeneo tofauti kati ya Oktoba 12 na 16 akiwa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Temeke eneo la Chang’ombe alihamasisha waumini wake watende kosa. 
Kesi hiyo itatajwa Novemba mosi na upelelezi haujakamilika. Aidha, washitakiwa walirudishwa rumande akiwamo bibi huyo wa miaka 100 na vijana wadogo.
Pamoja na jitihada za wakili wao Juma Nasoro kuwaombea dhamana wateja wake, jitihada hizo ziligonga mwamba.  
Baada ya kumalizika, msafara wa zaidi ya magari kumi uliondoka na washitakiwa hao likiwemo gari la maji ya kuwasha huku Shekhe Ponda akiwekwa katika gari la vioo vya giza kama alivyoletwa.

No comments: