AMCHINJA NDUGU YAKE MSIKITINI KONDOA AKISWALI...

Kamanda wa Polisi Dodoma, Zelothe Stephen.
Jeshi la Polisi wilayani Kondoa mkoani Dodoma linamtafuta Masuri Bakari Lubuva kwa tuhuma za kumuua ndugu yake kwa kumkata na mundu akiswali msikitini.
Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki katika Msikiti wa Kijiji cha Mlongia.
Akisimulia mkasa huo mjomba wa marehemu, Maulid Kijongo alisema ilikuwa ni kawaida kwa ndugu yake huyo kufanya ibada kila siku, hivyo siku ya tukio akiwa msikitini alifika Lubuva ambaye ni mtoto wa baba yake mkubwa akiwa na mundu na kumkatakata.
"Baada ya kukatwa damu nyingi zilitoka na kusababisha akimbizwe katika Hospitali ya Wilaya ya Kondoa kwa matibabu walipofika njiani alifariki kutokana na kuvuja damu nyingi," alisisitiza Kijongo.
Alisema pamoja na kuwepo kwa matukio kadhaa kama hayo yaliyowahi kutokea katika maeneo hayo lakini tukio hilo ni la aina yake kwani lilitokea ndani ya Msikiti, jambo lililozua mshangao kwani mtuhumiwa angeweza kusubiri atoke msikitini na si wakati akifanya ibada.
Kwa mujibu wa Kijongo mtuhumiwa baada ya kufanya kosa hilo alikamatwa na raia wema kisha kuwekwa chini ya ulinzi, lakini wakati akipelekwa Polisi aliwatoroka.
Jeshi la Polisi mkoani Dodoma limekiri kutokea tukio hilo na kusema jitihada za kumsaka mtuhumiwa zinaendelea.

No comments: