Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Vallentino Mokiwa. |
Kamati ya Usimamizi wa Kanisa na waumini wa madhehebu ya Anglikana, Kanisa la Watakatifu Wote la hapa imesisitiza kuwa waumini wake wataendelea kutomtambua na kumzuia Askofu Mathayo Kasagara kuingia kanisani humo.
Huku wakitahadharisha kuwa hawatarajii nguvu ya namna yoyote ile kutumika dhidi ya waumini hao kwani kufanya hivyo kutafanya Nyumba hiyo ya Maaskofu wa Kanisa hilo la Anglikana Tanzania kulaumiwa na dunia nzima.
Kwamba waumini hawako tayari kulazimishwa kumkubali Askofu Kasagara kuwa kiongozi wao wa kiroho na Nyumba ya Maaskofu wa Kanisa hilo Tanzania.
Waumini hao kupitia kamati yao hiyo wameweka wazi kuwa hawako tayari na hawatarejesha mali zozote za Kanisa kwa maaskofu kwa kuwa wenye mali hiyo ni waumini na si Nyumba ya Maaskofu kwani wao ni wadhamini.
Pia waliomba waumini wenzao wa makanisa mengine duniani wawaombee waumini wa Kanisa hilo katika vita hiyo ya kiroho mabayo wana uhakika kwa maombi ya pamoja, Mungu wa Amani ataleta ufumbuzi wa kweli.
Hayo yalielezwa jana na Mwenyekiti wa Kamati hiyo na waumini wa Kanisa, John Mahinya kwa mwandishi wa habari hizi baada ya Kamati kukutana kanisani hapo kujibu tamko lililotolewa na Katibu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania, Dk Dickson Chilongani kwa vyombo vya habari Dodoma wiki iliyopita .
Katika tamko hilo kutokana na mgogoro huo wa Kanisa uliodumu kwa miaka mitatu sasa, maaskofu katika mkutano wa Dodoma waliridhia Askofu Kasagara aendelee kutoa huduma, huku ‘likiwageuzia kibao’ waumini wanaompinga.
Pia waumini hao walitakiwa kurejesha mali zote za Kanisa na wakishindwa kufanya hivyo, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Kwa mujibu wa Dk Chilongani mali zinazopaswa kurudishwa na kukabidhiwa kwa Dayosisi ya Ziwa Rukwa ni pamoja na Kanisa la Watakatifu Wote, ofisi ya Mchungaji, nyumba mbili za wachungaji, uwanja wa Kantalamba iliko nyumba ya Askofu na Kanisa dogo la Askofu.
Mali nyingine ni jengo la ofisi ambalo halijakamilika, viwanja 14 vya Kanisa eneo la Majumba Sita na shule ya msingi ya mtaala wa Kiingereza ya Mtakatifu Mathias.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Mwenyekiti Mahinya waumini wa Kanisa hilo kupitia kamati hiyo waliweka wazi msimamo wao juu ya kukabidhi mali zinazoitwa za Dayosisi ya Ziwa Rukwa.
"Tumetambua na kuendelea kutambua, kuwa vita kubwa tuliyonayo na viongozi wetu wa kiroho ni juu ya mali tuliochuma sisi waumini wa Kanisa hili kwa jasho letu wenyewe … Nyumba ya Maaskofu ni wadhamini tu wala si wenye mali …. Mali inakabidhiwa kwa mdhamini kama mwenye mali hayupo sasa wenye mali tupo ni sisi waumini wa Kanisa la Watakatifu Wote mjini hapa
"Hii ndiyo sababu mali hii iko mikononi mwetu na sisis wenye mali ndiyo wenye haki ya kumkabidhi tunayemtaka…mali mnazitaka lakini mwenye mali halisi mnamwambia ni hiyari kuwa Mwanglikana au la, basi kama hamtaki mwenye mali basi mwacheni na mali zake," alisisitiza Mwenyekiti Mahinya.
"Hatutarajii kurudi mahakamani lakini pia hatutarajii nguvu ya namna yoyote kutumika dhidi yetu kwa kufanya hiyo mtalaumiwa (Nyumba ya Maaskofu) na dunia nzima. Huu ni ushauri tu mnaweza kuupokea au kuukataa lakini pia tunashauri kuwa achaneni na suala la mali, takeni sana kuokoa roho za watu ili waweze kumwona Mungu baada ya maisha haya ya tabu za dunia," alisema.
Kikao cha maaskofu Septemba 26 Dodoma kwa mujibu wa Dk Chilongani kilitafakari kwa kina juu ya fujo katika Kanisa Septemba 23 zikisababishwa na kundi lisilomtambua Askofu Kasagara.
Katika vurugu hizo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Valentino Mokiwa aliripotiwa kunusurika kipigo wakati wa vurugu.
No comments:
Post a Comment