Mheshimiwa Samuel Sitta
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja amesema kitendo cha Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta kukisema chama hicho mbele ya wanafunzi wa darasa la saba ni sawa na kutokitendea haki.Mgeja alisema hayo alipozungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana na kuongeza kwamba Waziri Sitta hakuitendea haki CCM kwa kutoa kauli dhidi ya viongozi wa CCM na Serikali, alipokuwa mgeni rasmi katika mahafali ya Shule ya Msingi Kwema juzi mjini hapa.
Alisema Sitta ni kiongozi mkubwa ndani ya CCM na Serikali yake, hivyo hakupaswa kutoa kauli kali dhidi ya chama wakati kuna mikutano na vikao husika vya ndani ambavyo vingeshughulikia suala hilo.
Aidha, alisema kitendo cha kuhutubia wanafunzi wa darasa la saba kuhusu mambo ya ufisadi badala ya kuwaeleza juu ya mfumo wa mtihani wao ulivyobadilika au Watanzania wamejipangaje kuhusu changamoto ya soko la pamoja la Afrika Mashariki, ni kutokitendea haki chama hicho.
Aliongeza kwamba Sitta akiwa mmoja wa viongozi serikalini, ana nafasi ya kupendekeza njia mwafaka za kupambana na ufisadi badala ya kuzungumza majukwaani kwa takribani miaka saba sasa.
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo wa CCM alisema mambo anayoyafanya Waziri huyo ni sawa na kampeni chafu zinazolenga kuwachafua na kuwabeba wagombea wengine katika uchaguzi wa CCM, hususan kwa nafasi ya Mwenyekiti wa Mkoa wa Shinyanga.
Badala ya kuharibu hali ya hewa ndani ya chama, alishauri ni vema akaangalia jinsi ya kukisaidia chama kwa njia zisizoweza kuleta mpasuko.
Aidha, alisema kauli za Sitta zina utata, akitolea mfano alipokuwa ziarani Kagera ambako alikaririwa akisema maisha bora kwa Mtanzania ni ndoto, hali ambayo Mgeja aliielezea kuwa ni sawa na kupinga kauli ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete.
Alisema Sitta sasa anafananishwa na mbogo aliyejeruhiwa ndani ya chama na kumwomba Rais aangalie kwamba anayoyafanya kwa sasa hayajengi chama bali yanakivuruga na ndiyo yanayosababisha baadhi ya wananchi waichukie CCM kwa kipindi hiki.
"Waziri amekosa maneno ya kuwapa matumaini Watanzania na badala yake anayoyaongea yanaweza kuiharibia CCM katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015.
Wakati Mgeja akisema hayo, mmoja wa wananchi ambaye hakuwa tayari kutajwa jina, alisema Sitta ifike mahali sasa ataje kwa majina mafisadi walio ndani ya chama na serikalini, kuliko kila mara kuwazungumzia watu wasiofahamika kwa wananchi wa kawaida.
Aliendelea kusema kuwa Waziri alipaswa kuzumgumzia mambo ya msingi na changamoto zilizopo wilayani Kahama kama vile kuwapo kwa migodi mikubwa ya dhahabu pamoja na kilimo cha mchele na ni jinsi gani atasaidia wana Kahama kukabiliana na soko la ushindani la Afrika Mashariki.
Kauli hizo zimekuja baada ya Waziri huyo kunukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari, akiihadharisha CCM kutokubali kukumbatia mafisadi na mawakala wao katika uchaguzi wa mwaka huu, na badala yake kitumie fursa hiyo kuachana nao ili kizaliwe upya.
Aidha, aliapa kutoacha kukemea vitendo vya rushwa, dhuluma, ufisadi na ubabe vinavyofanywa na baadhi ya viongozi wa CCM na Serikali hata kama kwa kufanya hivyo ataambiwa anaipaka matope Serikali, huku akitamba kuwa tabia ya kusema ukweli imewafanya wapigakura wake kumpachika jina la ‘Chuma cha Pua’.
Waziri huyo ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Tisa linalotajwa kuwa lililokuwa na msisimko mkubwa, alisema wakati umefika sasa Watanzania kutambulika kwa uadilifu na si kwa ufisadi, ubabe, dhuluma na rushwa.
Alisema hayo alipokuwa akihutubia wanafunzi, wazazi na walezi waliohudhuria mahafali ya 11 ya darasa la saba katika shule hiyo ya mchepuo wa Kiingereza ya Kwema iliyopo mjini hapa, katika hafla iliyohudhuriwa pia na Mbunge wa Kahama, James Lembeli ambaye pia amejitosa kuwania Uenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Shinyanga.
No comments:
Post a Comment