WATAKA KATIBA MPYA IRUHUSU WANAWAKE KUOA...

Nakala ya Katiba ya sasa.
Suala la unyanyasaji wa kijinsia limeibuka katika utoaji maoni ya Katiba mpya, ambapo mmoja wa watoa maoni amependekeza wanawake wapewe fursa ya kulipa mahari na kuoa wanaume.
Mkazi wa Kata ya Kigosera, Edilgot Milinga (54), ambaye elimu yake ni kidato ya cha nne na ni Ofisa Mtendaji wa Kata hiyo wilayani hapa, alisema juzi kuwa wanawake wakiruhusiwa kuoa, huenda tatizo la unyanyasaji wa kijinsia katika jamii likaondoka.
"Hawa wanawake inasemekana tunawanyanyasa mpaka inawachanganya, sasa ili isiwachanganye, kipengele cha ndoa kiwe huru. Kama mwanamke anaweza kuoa, atongoze, alipe mahari ili naye aoe.
"Inaonesha wanachanganyikiwa kwa sababu wanaolewa," alisema Mtendaji huyo na kusababisha wajumbe wa Tume ya Kukusanya Maoni ya Katiba mpya, kuangua kicheko.
Mbali na kupendekeza wanawake waruhusiwe kuoa ili wapate haki alizodai wanazipata wanaume, Mtendaji huyo alitaka Katiba itangaze ukomo wa idadi ya wake wanaopaswa kuolewa na mwanamume na ukomo wa idadi ya watoto.
"Idadi ya wake itamkwe katika Katiba, mwisho iruhusiwe kuoa wake wawili na watoto mwisho watatu … mazingira ya uchumi yamebadilika, tunashindwa kupeleka shule watoto wetu," alisema Milinga.
Mkazi mwingine wa kata hiyo, Ditrick Mwingira, alipendekeza Katiba iruhusu wafungwa kupelekewa wake zao angalau mara mbili kwa wiki, ili kuepuka wanaume kuingiliana kimwili.
Hata hivyo, mkazi wa Kata ya Mkako, Emelda Mkondola, ambaye elimu yake ni darasa la saba na mwalimu wa dini, alisema ingawa wanawake wanafanya kazi sawa na wanaume, lakini wanaume wamekuwa wakitawala mazingira ya nyumbani.
Alipendekeza Katiba itambue usawa wa mwanamke na mwanamume katika kazi za nyumbani, ili kuondoa unyonyaji kwa mwanamke.
"Inatakiwa tukitoka shamba, mimi mama nikibeba mtoto, baba abebe jembe na kuni, tukifika nyumbani nikibandika maji, baba awe anaogesha mtoto," alisema Emelda.
Naye mwanafunzi wa Seminari ya Likonde, Greyson Kibanga (18), aliyejitambulisha kama Padri mtarajiwa, alipendekeza adhabu inayotolewa kwa mwanafunzi wa kiume aliyempa ujauzito wa kike isionee wanafunzi wavulana.
Alipendekeza ili kuwe na usawa, kama adhabu ni jela miaka 30, wagawane, msichana miaka 15 na mvulana miaka 15.
Wajumbe wa Tume ya Maoni ya Mabadiliko ya Katiba walioko Ruvuma ni pamoja na Al Shaymar Kwegyir, Ally Saleh, Fatma Said Ally chini ya Profesa Mwesiga Baregu.

No comments: