Sehemu ya majengo ya Hospitali ya Mwananyamala iliyoko katika Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Siku moja baada ya kuhusishwa na uzembe uliosababisha maiti kuchukuliwa na familia nyingine na kusafirishwa hadi Tanga kwa maziko badala ya Dar es Salaam, uongozi wa hospitali ya Mwananyamala imekana kuhusika na uzembe huo.Badala yake, imedai suala hilo linaliangukia Jeshi la Polisi kwa madai, kwamba vifo vinavyotokana na ajali mara nyingi hushughulikiwa na Jeshi hilo.
Kauli hiyo ilitolewa jana na mmoja wa maofisa wa hospitali hiyo ambaye alikataa kutajwa, akisema vifo wanavyohusika navyo ni vya kawaida vinavyotokea hospitalini hapo.
"Suala lolote linalohusu vifo vilivyotokana na ajali, moja kwa moja Polisi ndio wenye jukumu la kutoa maiti mochari, hivyo suala la mwili uliotolewa kimakosa kwa kweli lilitokana na wao kwa sababu marehemu alikufa kwa ajali," kilieleza chanzo hicho.
Alikuwa anazungumzia mwili wa askari wa kampuni ya ulinzi ya Group 7 Security, Ntimaruki Khenzidyo (25) aliyekufa Jumatatu kwa ajali ya gari eneo la Masaki, Dar es Salaam na mwili wake kuhifadhiwa hospitalini hapo, lakini juzi ikaibuka tafrani baada ya ndugu wa marehemu kufuata mwili na kuelezwa na wahusika kuwa umeshachukuliwa.
Majibu hayo yaliamsha hasira za ndugu waliocharuka na kufanya fujo wakitaka kupewa mwili wa ndugu yao. Polisi walilazimika kuingilia kati kuzima vurugu hizo, zilizodumu kwa zaidi ya saa tatu.
Baadaye ilifahamika, kuwa mwili huo ulichukuliwa kimakosa na wafiwa wengine wa Tanga ambao walishausafirisha, lakini bila kujua kuwa haukuwa mwili wao. Mwili wa Khenzidyo ulikuwa uzikwe makaburi ya Mikocheni, Dar es Salaam jana mchana, lakini shughuli hiyo imeendelea kusitishwa kusubiri mwili urudishwe kutoka Tanga.
Hata hivyo, Kamanda wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alipoulizwa juu ya suala hilo, alikana Polisi kuhusika na uzembe, akisisitiza kuwa Jeshi hilo halitunzi maiti na wala halihusiki na utoaji maiti mochari.
Alisema kazi ya Polisi ni kupima mwili kuangalia kama ulihusiana na uhalifu wa aina yoyote na kisha kuacha ripoti hospitalini ambapo wanaweza kupata maelekezo ya ama uruhusiwe kuchukuliwa au la.
Aliongeza kuwa, tayari ndugu wa Khenzidyo wameshafungua jadala la malalamiko katika kituo cha Polisi cha Oysterbay, Kinondoni, kuhusu suala la kuchukuliwa kwa mwili wa ndugu yao kimakosa.
Katika maelezo yao wanalalamika kupotea kwa mwili wa marehemu wao, huku wakisisitiza kuwa haki na wajibu ni lazima vipewe kipaumbele katika kushughulikia suala hilo.
Kamanda Kenyela alitumia fursa hiyo kusihi ndugu kuwa na subira wakati Polisi ikiendelea kufuatilia suala hilo, huku akiongeza kuwa hana uhakika kama baada ya mwili huo kupelekwa Tanga kimakosa umezikwa au bado.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Costantine Massawe alisema hana taarifa za tukio hilo, na kutoa rai kuwa kama kuna familia inahusika na tukio hilo, iangalie uwezekano wa kuurudisha mwili Dar es Salaam.
"Ninashangaa sana. Iweje watu wachukue mwili usio wao … ilikuwa lazima wautazame kwanza kabla ya kuuchukua hospitalini au kabla ya kuuzika na kwa nini hawakufanya hivyo?" Alihoji Massawe.
Akizungumzia sakata hilo, Thobias Msulwa ambaye ni ndugu wa marehemu, alisema suala hilo linasikitisha kwa kuwa linaonesha bado uzembe unaweza kusababisha vurugu katika jamii.
No comments:
Post a Comment