KATIBA MPYA 'YATOLEA MACHO' NAFASI YA URAIS...

Nafasi ya urais imeelekezewa vidole na wachangiaji maoni juu ya Katiba ijayo wilayani Mbinga, mkoa wa Ruvuma wakitaka ipunguziwe mamlaka ya uteuzi na rais awajibishwe anapofanya makosa katika utendaji wake, hata kabla ya muda wa uchaguzi mkuu.
Aidha katika kumwajibisha, wananchi hao wamependekeza kusiwepo na muda wa kupoteza tangu kumwajibisha hasa kama uwajibishaji wenyewe unahusisha kumuondoa madarakani, mpaka kupatikana kwa kiongozi mwingine.
Innocent Mwitoto (22) anayesoma kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Makatekista iliyopo Kata ya Kigosera wilayani Mbinga, alisema hayo juzi alipokuwa akitoa maoni yake kuhusu Katiba anayoitaka.
Alisema anavyoona kiongozi wa Serikali nchini yuko juu ya sheria na akataka katika Katiba ijayo, Kiongozi wa Serikali awe chini ya sheria na ikitokea anaonesha upungufu, asisubiriwe amalize muda wake kikatiba.
Hoja hiyo iliungwa mkono na Mwalimu Melkioni Mwandumu (59) wa Wilaya ya Mbinga ambaye alitaka Rais akishindwa kazi, aondolewe na kuchaguliwa mwingine mara moja.
Pia Mtawa Betha Shamo (28) wa Mbinga, alipendekeza kiongozi yeyote akishindwa kazi, aondolewe madarakani kabla ya muda wake kuisha, awekwe mwingine.
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha St. Augustine, Tilosi Msigwa (25), alipendekeza katika Katiba ijayo, Rais asiwe sehemu ya Bunge kama ilivyo sasa na asiwe na madaraka ya kuvunja Bunge.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kigosera wilayani Mbinga, Joseph Ngai (45), alipendekeza katika uchaguzi, Rais apatikane baada ya kupata asilimia 50 ya kura zote.
Baadhi ya wananchi wametaka taasisi ya urais, ipunguziwe madaraka ya kuteua viongozi muhimu katika jamii kama Majaji na Jaji Mkuu, wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Gavana wa Benki Kuu (BoT), Msajili wa Vyama vya Siasa na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).
Wengine ambao wananchi wamependekeza wasiteuliwe na Rais ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) na wabunge kumi wa kuteuliwa.
Akizungumza mbele ya sehemu ya wajumbe wa Tume ya Kukusanya Maoni ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Profesa Mwesiga Baregu juzi, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha St. Augustine, Tilosi Msigwa (25), alipendekeza Jaji Mkuu achaguliwe na majaji wenzake.
"Kama ilivyo kwa Spika wa Bunge, ambaye anachaguliwa na wabunge, iwe hivyo pia kwa Jaji Mkuu achaguliwe na majaji wenzake," alisema Msigwa.
Mwalimu wa Shule ya Sekondari Kigosera wilayani Mbinga, Bryceson Mwakyosi (28) alipendekeza DPP ateuliwe na Jaji Mkuu kwa kushauriana na wanasheria au Chama cha Wanasheria Tanganyika.
Pia alipendekeza Mkurugenzi wa Takukuru ateuliwe na Jaji Mkuu na wajumbe wa NEC wawe wawakilishi wa vyama vya siasa na wateuliwe na vyama vyao.
Profesa Baregu alipomuuliza kuwa haoni wawakilishi wa vyama vya siasa watasababisha mvutano na kuzuia Tume kufanya uamuzi, Mwakyosi alisema hata wakivutana, wakikubaliana watazuia mvutano wa vyama vya siasa kwa kuwa watakuwa mashahidi wa kilichotokea.
Hata hivyo, mkulima wa kata hiyo, Galus Mhalo (46) ambaye ana elimu ya darasa la saba, alipendekeza mamlaka ya uteuzi wa wajumbe wa NEC, iwe Bunge.
Baadhi ya wananchi wamependekeza Katiba ijayo itamke idadi kamili ya mawaziri na kuzuia wabunge wasiwe mawaziri huku wakitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, isiingiliwe na siasa.
Mwanafunzi wa kidato cha tatu Shule ya Sekondari ya Makatekista wilayani Mbinga, Innocent Mwitoto (22), alisema wizara hiyo ina umuhimu katika jamii, hivyo itamkwe katika Katiba kuwa waziri hapaswi kubadili mitaala atakavyo.
Mbele ya wajumbe wengine walio katika mkutano huo ni ambao ni Fatma Said Ally, Alli Salehe na Alshaimar Kwegir, Mwalimu wa Shule ya Sekondari Kigosera, Tilosi Msigwa (25), alipendekeza Waziri asiyekuwa na Wizara Maalumu, asiwepo kwa kuwa anaonekana hana kazi, analipwa mshahara wa bure.
Mwalimu Bryceson Mwakyosi (28) wa shule hiyo, alipendekeza nafasi ya Naibu Waziri ifutwe kwa kile alichosema makatibu wakuu wa wizara wanatosha kusaidiana na Waziri.
Alitaka pia iwekwe idadi kamili ya mawaziri na Rais aruhusiwe kupunguza na si kuongeza. Alipotakiwa na Profesa Baregu ataje idadi anayoitaka, alipendekeza wasizidi 20.
Mwanafunzi wa Kidato cha Pili, Shule ya Sekondari ya Makatekista, Marcus Kantambi, alipendekeza mawaziri wasitoke chama kinachotawala pekee bali watoke vyama vya upinzani pia.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kigosera, Edilgot Milinga alipendekeza mawaziri wawe wasomi wa Wizara wanazokabidhiwa. Alitoa mfano wa Wizara ya Kilimo na Chakula, kwamba waziri wake awe msomi wa kilimo.

No comments: