ABDULRAHMAN KINANA AJIWEKA KANDO CCM...

Abdulrahman Kinana.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Abraham Kinana, amesema hatogombea tena nafasi za vikao vya juu kwa kuwa muda wa miaka 25 aliyotumikia katika nafasi hizo unatosha.
Kinana aliyasema hayo mjini Dodoma na kubainisha kuwa anaamini kitendo cha kung’atuka kwake ni kizuri na kitatoa nafasi kwa wanaCCM wengine wazuri nao watoe mchango wao kwa chama hicho.
"Sijagombea kwa kuwa miaka 25 ya kushiriki katika vikao vya juu inatosha na ni vizuri kung’atuka, naamini kuna wana CCM wengi wenye sifa na uwezo wa kuongoza chama," alisema Kinana.
Alisema suala la uongozi ni la kupokezana vijiti hivyo kwa sasa ni wakati wake kukabidhi vijiti alivyo navyo kwa wengine.
Wakati Kinana akitoa kauli hiyo, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alimsifu Kinana kwa uamuzi huo na kuuita kuwa ni uzalendo.
"Tunashukuru kwa uzalendo, ujuzi na uzoefu alioonesha katika kipindi chote alichoshika nyadhifa mbalimbali ndani ya chama, hata hivyo, napenda nisisitize kutokana na sifa alizonazo bado chama chetu kinamhitaji," alisema Nnauye.
Alisema kung’atuka kwake kuwania nafasi za vikao vya juu ndani ya chama hicho hakumaanishi kuwa chama hicho hakitoendelea kumtumia pale kitakapomhitaji, kwa kuwa uzoefu wake na utendaji wake ni mtaji ndani ya chama.
Alisema pamoja na kuamua kuachia ngazi, Kinana anaendelea kushika nyadhifa nyingine ndani ya chama hicho, ikiwamo ya Uenyekiti wa Bodi ya vyombo vya habari vya CCM vya Uhuru na Mzalendo.

No comments: