ASKOFU MOKIWA CHUPUCHUPU KUPATA KIPIGO...

Waumini wakianza kutofautiana mbele ya Askofu Mkuu, Dk. Valentino Mokiwa (kulia).
Mgogoro uliolikumba Kanisa la Watakatifu Wote la Anglikana mjini Sumbawanga na kudumu kwa zaidi ya miaka mitatu, umeshindwa kupata ufumbuzi wa kudumu baada ya Askofu Mkuu wa Kanisa hilo la Anglikana Tanzania, Dk Valentino Mokiwa jana kujikuta katika wakati mgumu baada ya kunusurika kupata kipigo katika vurugu zilizoibuka kanisani.
Vurugu ziliibuka baada ya kusomwa tamko lililothibitisha kuwa nyumba ya maaskofu inamtambua Askofu Mathias Kasagara kuwa ni kiongozi wao halali wa kanisa la Anglikana la Watakatifu Wote Jimbo la Ziwa Rukwa mjini Sumbawanga.
Katibu Mkuu wa Anglikana, Dk Dickson Chilongani ndiye aliyesoma tamko hilo mara baada ya kumalizika kwa ibada iliyoongozwa na Dk Mokiwa.
Dk Chilongani alisema Kasagara ni askofu wao halali kwa kuwa sehemu ya hoja za msingi za kamati ya usimamizi wa kanisa hilo zilidai kuwa uchaguzi uliomweka madarakani Askofu Kasagara uligubikwa na rushwa, si za kweli na nyumba ya maaskofu imeshindwa kuthibitisha.
Baada ya kauli hizo waumini walianza kupiga kelele ya kupinga maelezo hayo, hali iliyosababisha mjumbe wa Kamati ya kusimamia kanisa hilo, Fulgence Lusunzu kushika kinasa sauti na kueleza kuwa wanao ushahidi wa kutosha kuwa rushwa ilitumika kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi huo uliofanyika zaidi ya miaka miwili iliyopita.
Alisema uamuzi wa nyumba ya maaskofu haukuwapa fursa ya kusikiliza upande wa walalamikaji, ilihali ushahidi upo wazi, kutokana kauli hiyo zilianza fujo zilizosababisha Askofu Mokiwa kutolewa lugha chafu, kuvuliwa kofia yake ya kiaskofu, huku wengine wakirusha viti ambavyo alivikwepa hadi alipoondolewa akiwa chini ya polisi waliokuwa wamevalia kiraia.
Pamoja na kuondolewa kwa Askofu Mokiwa, kanisa hilo liliendelea kuwa uwanja wa vita huku waumini wakisikika wakidai kuwa ni heri kanisa hilo lifungwe kuliko Askofu Kasagara kuliongoza.
Awali tangu asubuhi, polisi waliovaa kiraia walitanda katika viunga vya kanisa hilo ambapo Askofu Mokiwa aliwasili na kulakiwa vizuri na waumini wake waliokuwa wakishangilia kwa nyimbo.
Hata hivyo, tayari waumini wa kanisa hilo walionya kwamba Askofu Kasagara asikanyage kwenye eneo hilo, kwani kufanya hivyo kungehatarisha amani, onyo ambalo upande wa Askofu Kasagara walitii hivyo askofu huyo mwenye makazi yake wilayani Mpanda alibaki katika nyumba moja ya kulala wageni alikokuwa amefikia.
Mmoja wa waumini, Julius Michael alisema kwa kuwa waumini wa Jimbo la Rukwa hawamtaki Askofu Kasagara, hakuna sababu ya kuwalazimisha isipokuwa nyumba ya maaskofu inapaswa kuangalia uwezekano wa kuligawa jimbo hilo.
Alisema Serikali imegawa mkoa wa Rukwa na kuzaa Katavi, na kwamba hakuna umuhimu wa kuwalazimisha waumini kumpokea mtu wasiyemtaka.
Mgogoro katika kanisa hilo umedumu kwa zaidi ya miaka miwili sasa, ambapo siku za nyuma waumini hao walimzuia Askofu Mkuu Dk Valentino Mokiwa kumsimika Askofu huyo na badala yake alisimikwa Juni 16 mwaka jana, mjini Mpanda.
Kutokana na mgogoro huo, ilifunguliwa kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Sumbawanga na waumini wa Anglikana wakiongozwa na Fulgence Rusunzu na Rojas Bendera na wenzao 191 yenye namba 11/2011 wakipinga kuchaguliwa kwa askofu Kasagara kuwa kiongozi wa Dayosisi hiyo.
Kesi hiyo iliondolewa baada ya pande mbili zinazovutana kukubaliana kuwa baraza la maaskofu ndilo lenye dhamana ya kutatua mgogoro huo.

No comments: