HAKIMU MKAZI ILALA KIZIMBANI KWA KUOMBA RUSHWA...

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, Pamela Kalala amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu, kujibu mashitaka ya kuomba rushwa Sh milioni 3 na kupokea Sh 900,000.
Kalala alipandishwa kizimbani jana mbele ya Hakimu Aloyce Katemana na kusomewa mashitaka yanayomkabili.
Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Allen Kasamala alidai kuwa mshitakiwa anakabiliwa na mashitaka matatu.
Kwa mujibu wa Kasamala katika tarehe tofauti Februari mwaka huu mshitakiwa akiwa katika Manispaa ya Ilala aliomba rushwa ya Sh milioni 3 kutoka kwa Josephine Wage.
Wage ni mke wa mshitakiwa katika kesi namba 703 ya mwaka 2008, dhidi ya Aboubakar Hamis na wenzake, na alitaka kumshawishi ili atoe uamuzi wa kumpendelea mumewe katika kesi inayomkabili.
Katika mashitaka la pili, Kalala anatuhumiwa kupokea rushwa ya Sh 800,000 kutoka kwa Wage, ikiwa ni ushawishi wa kutoa uamuzi wa kumpendelea mume wake huyo.
Hata hivyo, Kasamala alidai kuwa katika mashitaka ya tatu, hakimu huyo anatuhumiwa kupokea rushwa ya Sh 100,000 kutoka kwa Wage Februari 6, ukiwa ni ushawishi wa kutoa uamuzi wa upendeleo.
Mshitakiwa alikana mashitaka yote na Kasamala kudai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na upande wa Jamhuri hauna pingamizi juu ya dhamana.
Katemana alisema ili mshitakiwa aweze kuwa nje kwa dhamana, anatakiwa asaini hati ya dhamana ya Sh milioni moja na mdhamini mmoja wa kuaminika atakayesaini hati ya dhamana ya kiasi hicho cha fedha.
Mshitakiwa alikidhi masharti ya dhamana na kuwa nje hadi Oktoba 23 kesi hiyo itakapotajwa.
Baada ya kutimiza mashari hayo, Kalala akifuatana na mtu anayedaiwa kuwa mumewe, walitoka mahakamani hapo kwa kupitia mlango wa nyuma kwa lengo la kukwepa wapiga picha waliokuwa wakisubiri picha yake.
Hata hivyo, wapiga picha hao walimwona na kumkimbilia ili kumpiga picha, hata hivyo waliendelea kupata ugumu baada ya mumewe kumkumbatia huku akicheka kwa dharau na kuwataka wapige picha kadri wawezavyo.

No comments: