MCHUJO WA AWALI CCM WAPINDULIWA...

Kamati ya Maadili na Usalama ya CCM imemaliza kupitia majina ya wagombea na kutoa mapendekezo yake ikiwamo kufumua uamuzi wa mchujo wa majina ya wagombea hao uliofanywa na vikao vya chini vya chama hicho.
Kamati hiyo ambayo kwa mujibu wa ratiba ilitakiwa kufanya kazi hiyo na kutoa mapendekezo kwa siku moja, ilikamilisha rasmi kazi hiyo saa tisa alfajiri kuamkia jana, baada ya kuifanya kwa siku tatu mfululizo.
Akifungua kikao cha Kamati Kuu ya CCM (CC) mjini hapa jana, Mwenyekiti wa Chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, alisema Kamati hiyo imefanya kazi kubwa, kupitia jina la kila mgombea wakiwamo waliopendekezwa kuenguliwa na vikao vingine vya chini.
"Tunaomba radhi kwa kuchelewa kuanza kikao hiki cha CC ambacho kilitakiwa kuanza siku mbili zilizopita, hii ni kutokana na kazi kubwa tuliyoifanya ya kupitia jina moja moja la kila mgombea hadi waliopendekezwa kuenguliwa, na kama mnavyojua idadi ya wagombea ni kubwa," alisema Rais Kikwete.
Alisema idadi ya wagombea waliojitokeza kuwania nafasi ndani ya chama hicho ni zaidi ya 5,000 wakiwamo wa nafasi za ndani za chama 2,853 na wagombea wa jumuiya 2,104.
Alisema kutokana na idadi hiyo kuwa kubwa, Kamati ya Maadili ililazimika kupitia majina yote na sababu zilizotolewa kwa walioenguliwa na waliopendekezwa kupita na kufanya mapendekezo tofauti na yaliyopitishwa na vikao hivyo mikoani.
"Tumechukua muda mrefu kupitia majina haya kutokana na ukweli wa wingi wa wagombea waliojitokeza, tumefurahi kwani wasomi wengi sana wamejitokeza, na ndiyo maana hata mapendekezo yetu ni tofauti kabisa na yaliyotolewa mikoani," alisisitiza.
Alisema kutokana na wingi wa wagombea, ni wazi chama bado kinafanya vizuri. "Nasikia kuna watu wanasema eti CCM inakufa, watakufa wao na kuiacha," alisema.
Rais Kikwete alisema anatarajia kazi ya CC ya kupitia mapendekezo ya Kamati ya Maadili haitakuwa kubwa kwa kuwa kazi kubwa imeshafanywa na kamati ya maadili na hivyo kikao hicho kilitarajiwa kumaliza jana usiku na leo kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kuanza rasmi. Kikao cha CC kina wajumbe 39 lakini waliohudhuria hadi jana walikuwa 34.

No comments: