KLABU YA YANGA HATARINI KUSHUSHWA DARAJA...


Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (Fifa) limelitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)  likazie hukumu yake iliyoitoa kwa Yanga kumlipa mchezaji John Njoroge ambaye mkataba wake ulivunjwa bila kufuata taratibu.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile  Osiah akizungumza Dar es Salaam leo alisema licha ya Fifa kuitaka Yanga imlipe mlinzi huyo ambaye kwa sasa anachezea Sofapaka   kiasi cha Sh milioni 17,159,800, pia imeitaarifu TFF kuhusiana na shitaka lililowasilishwa na kocha wa zamani wa Yanga, Kostadin Papic ambaye anaidai dola za Marekani 12,300  za malimbikizo ya mshahara wake.
Kwa mujibu wa Osiah , Yanga inatakiwa  kutekeleza uamuzi huo wa kumlipa Njoroge kiasi hicho cha fedha ikiwa ni fidia ya kuvunja mkataba wake kinyume cha taratibu ambao ulitolewa Desemba mwaka jana na kufika TFF  Januari mwaka huu haraka iwezekanavyo  ili kuepuka adhabu ambazo inaweza kupewa na Fifa endapo itashindwa kutekeleza adhabu hiyo.
Osiah alibainisha kuwa endapo Yanga watashindwa kutekeleza adhabu hiyo waliyopewa na Fifa inaweza kushushwa daraja, kunyang’anywa pointi kwenye mechi zake za ligi au kupigwa faini. 
“ TFF tunaitaka Yanga kutekeleza  hukumu hiyo mapema ili kuepuka adhabu ambazo inaweza kukubaliana nazo endapo itakaidi kutekeleza hukumu, hivyo kutulazimu kufanya kile ambacho Fifa itaamua dhidi yao,” alisema Osiah.
“Ushindi wa Njoroge unamaanisha kuwa iwapo Yanga itashindwa kutekeleza kumlipa mchezaji huyo kasi cha Sh milioni 17, inaweza kujikuta katika adhabu ambayo itatulazimisha tuishushe daraja; kuinyang’anya pointi kwa kiwango kitakachotajwa na Fifa, kuipiga faini au adhabu zote kwenda kwa pamoja. Tunaiomba Yanga itekeleze hukumu hiyo kwa wakati uliotajwa kwenye barua ya FIFA ili kuepuka hatua hizo,”alisema Osiah.
Kuhusiana na suala la Papic, Osiah alisema TFF imepokea barua kutoka Kitengo cha Sheria cha Fifa likiwataka waitaarifu Yanga kuhusu mashitaka yaliyowasilishwa na Papic ambaye anadai kuwa hajalipwa malimbikizo ya mshahara wake yanayofikia kiasi cha dola 12,300 za Kimarekani na kwamba kocha huyo anadai alikuwa akiwasiliana na maofisa na viongozi wa Yanga, lakini hakupata ushirikiano na hivyo kuamua kwenda Fifa.
“TFF ilifanya juhudi za kuwasiliana na Yanga kuhusu malalamiko hayo ili kujaribu kumzuia kocha huyo asishtaki Fifa, lakini juhudi hizo hazikuzaa matunda. TFF imesikitishwa na habari hizo na inaiomba Klabu ya Yanga kufanya kila jitihada kuhakikisha inawasilisha taarifa zote muhimu na nyaraka zinazohusiana na stahiki za kocha huyo ili kama ilishamalizana naye, sifa ya Klabu ya Yanga isafishwe. 
“Tayari barua imeshaandikwa kwa Klabu ya Yanga kuitaka itekeleze utashi huo mapema iwezekanavyo. Tukio hilo, si tu linachafua sifa ya Klabu ya Yanga, bali soka ya Tanzania kwa ujumla kutokana na ukweli kwamba ikishadhihirika kuwa kuna tatizo la malipo ya makocha nchini, ni dhahiri kuwa itakuwa ni vigumu kwa klabu zetu na hata timu za taifa kupata makocha wazuri kutoka nje kwa kuwa watakuwa wamejengeka hofu ya kufanya kazi nchini,” alisema Osiah.
Pia Osiah alizungumzia suala la Yanga kutimua Sekretarieti ya Yanga na kueleza kuwa TFF bado haijapata rasmi taarifa hizo na kueleza kuwa inasubiri ijulishwe kwa barua na Yanga kuhusiana na jambo hilo.
“Kama itakuwa imeitimua Sekretarieti nzima, basi TFF inapokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa. Si nia ya TFF kutetea watendaji wazembe, lakini klabu hazina budi kufuatilia kwa karibu utendaji wa Sekretarieti zao ili isije ikafikia wakati Sekretarieti nzima inaondolewa kwa makosa ambayo yangeweza kusahihishwa kama kungekuwa na ufuatiliaji wa karibu,” alisema.
Pamoja na hayo Osiah amezitaka klabu za soka nchini kujenga utaratibu wa kuhakikisha taratibu za kuvunjwa mikataba ya wachezaji, makocha ama wafanyakazi wengine wa klabu hizo zinafuatwa ili kuepuka masuala hayo kufikishwa mbali kwenye vyombo vya juu.
 “TFF haizuii makocha kufukuzwa kazi endapo wanakiuka makubaliano ama wameshindwa kuonesha kiwango  lakini suala hilo lifanyike kwa kufuata utaratibu ili  kuepuka ukiukwaji wa taratibu za kuvunja mikataba inayofanywa na klabu zetu.” 

No comments: