Saturday, August 11, 2012

WALIONASWA WAKISAFIRISHA KILO 92 ZA HEROIN WAFUNGWA MIAKA 25 JELA...


Watu watano kati ya sita walionaswa wakisafirisha pakiti 95 sawa na kilo 92.2 za heroin wametupwa jela miaka 25 kila mmoja baada ya kupatikana na hatia.
Watu hao ambao kati yao wamo Watanzania wanne na raia mmoja wa Iran  pia wanatakiwa kulipa faini ya Sh trilioni 1.4.
Aidha katika hukumu hiyo mahakama hiyo imemwachia huru mshitakiwa wa sita Bakari Kileo Mambo na imetaifisha magari mawili madogo.
Watuhumiwa waliotiwa jela ni Kileo Bakari Kileo, Yahaya Zumo Makame, Mohamed Pourgad (Muiran), Salumu Mohamed Mparakasi na Said Ibrahim Hamisi. 
Akisoma hukumu hiyo jana kwa lugha ya Kiswahili  baada ya mshitakiwa wa tatu kuridhia, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanga Mussa Kipenka alisema upande wa mashitaka uliweza kuthibitisha kesi dhidi ya watuhumiwa watano na yeye amewatia hatiani.
Watuhumiwa sita walifikishwa Mahakama Kuu wakikabiliwa na makosa mawili ambayo ni kula njama ya kutenda kosa na kusafirisha dawa hizo katika miji ya Dar es Salaam, Tanga na Jamhuri ya Nchi ya Iran kwenye tarehe mosi hadi nane ya Machi 2010.
Dawa  hizo za kulevya zilikuwa na thamani ya zaidi ya Sh bilioni 2.3 kwa mwaka 2010.
“Kutokana na kosa hilo la kwanza ambalo ni washitakiwa wote sita kula njama ya kusafirisha dawa hizo za kulevya kwa kuzingatia ushahidi wa pande zote mbili za mashitaka na utetezi, mazingira na mlolongo wa matukio nimesita kuwahusisha washitakiwa wote sita kwa sababu shitaka hili limeletwa na uwepo wa shitaka la kusafirisha dawa.”
Akizungumzia kosa la pili ambalo ndilo lililowatia hatiani washitakiwa watano na kumwacha huru Mambo alisema mnamo Machi 8,2010 majira ya mchana katika eneo la Kabuku kwa pamoja walikamatwa washitakiwa hao sita wakiwa kwenye msafara wa kusafirisha dawa hizo.
“Kosa la pili lilikuwa washitakiwa kukamatwa Kabuku wakisafirisha dawa zenyewe ambazo zilifungwa katika pakiti 95 ndani ya mabegi matatu katika gari lililokuwa likiendeshwa na mshitakiwa wa kwanza ambapo hata hivyo wote walikana shitaka.
“ Upande wa mashitaka uliita mashahidi 20 na kutoa vielelezo 25 huku utetezi nao wakileta mashahidi 17 na vielelezo 15 na katika kusikiliza pande zote hizo Mahakama ilibaini kwamba hapakuwa na maelezo zaidi ya kuendelea kubishaniwa kuhusu uraia wa washitakiwa wote” alisema.
Akitoa ufafanuzi zaidi kuhusu kosa hilo Kipenka alisema ushahidi na vielelezo vilivyowasilishwa wakati wa shauri hilo ulizingatia matukio makuu manne ambayo ni namna mshitakiwa wa tatu (Pourgad) alivyoombewa VISA ya kuingia nchini kwa ushirikiano wa mshitakiwa wa kwanza na wa pili.
“Tukio jingine madai ya baadhi ya mashahidi akiwemo wa tisa kwamba washitakiwa wote sita walifika kwenye Hoteli ya Nyinda Classic jijini Tanga na kupanga vyumba, tukio la tatu ni la Machi 8,2010 washitakiwa kukamatwa Kabuku na nne ni tukio la dawa zilizokutwa zikisafirishwa na washitakiwa kufanyiwa uchunguzi na uthamini wa kitaalamu kwenye maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na kusababisha wahusika hao wote kufikishwa hapo mahakamani ingawa wote walikana shitaka hilo,” alifafanua Kipenka.
Hata hivyo Kipenka aliongeza kwamba anakubaliana kabisa na ushahidi ulioletwa na mashahidi namba 14 na 16 kwamba washitakiwa namba 1 na 2 walishiriki kumwombea VISA mshitakiwa wa 3, magari mawili yaliyotajwa kufika Nyinda Classic yalikuwa yakishabihiana sana na yale yaliyokamatwa Kabuku.
Magari hayo ni namba T. 650 BAT aina ya Suzuki Grand Vitara yenye rangi ya 'silver' na T.457 BCQ Toyota Rav4 yenye rangi ya kijani ambayo yalitumiwa katika matukio na kwa nyakati tofauti mkoani Tanga na Dar es Salaam kusafirisha dawa hizo kabla ya kukamatwa Machi 8, 2010 katika kizuizi cha askari cha Kabuku kilichopo kwenye barabara kuu ya Segera – Chalinze wilayani Handeni yametaifishwa.
Kwa upande wao mawakili wa utetezi waliokuwa wakiwatetea washitakiwa hao 1- 5, akiwemo Mbando, Chuwa na Akaro, pamoja na kuridhia uamuzi wa Mahakama walimuomba Jaji kuangalia uwezekano wa kuwapunguzia adhabu washitakiwa hao hasa kutokana na kusota rumande kwa miezi 29 sasa.
Akisoma hukumu Jaji Kipenka alisema kulingana na kifungu cha 16 kifungu kidogo cha kwanza b,(i) cha sheria ya kuzuia na kudhibiti dawa za kulevya pamoja na kifungu cha 73 cha tafsiri ya sheria washitakiwa wangeweza kujikusanyia kiasi cha Sh 7,191,822,000.00 kiasi ambacho ni mara tatu ya thamani ya dawa hizo zote.
“Hivyo basi Mahakama inawahukumu wote watano kila mmoja kulipa faini ya Sh  1,438,364,400.00 pamoja na kifungo cha miaka 25 jela kwa kila mmoja pia nafasi ya kukata rufaa iko wazi,” alitangaza Jaji huyo.

No comments: