Baadhi ya wanakwaya walionusurika kwenye ajali hiyo wakisubiri msaada eneo la tukio.
Wanakwaya 12 wa madhehebu ya Kikristo walikufa papo hapo jana na wengine 14 kujeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyotokea Kijiji cha Makole jirani na Mto Wami iliyohusisha magari manne.
Kufuatilia ajali hiyo Rais wa Kenya, Mwai Kibaki ameagiza ndege ya kuwabeba majeruhi kuwarejesha nchini Kenya kwa matibabu zaidi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Ernest Mangu alisema ajali hiyo ilitokea saa 11 alfajiri jana ambapo lori la mizigo lililokuwa likitokea Tanga kuelekea Dar es Salaam liligonga basi dogo la abiria lililowabeba wanakwaya hao waliokuwa wakitokea Nairobi kwenda Dar es Salaam kwa shughuli za kidini.
Kamanda Mangu alisema lori hilo liligonga basi lililosimama ili kutoa msaada kwa wanakwaya waliokuwa kwenye basi lingine ambalo liliacha njia na kupinduka upande wa kulia wa barabara hiyo.
“Basi hilo lilisimama na abiria waliteremka ili kutoa msaada kwa wenzao ambao basi lao lilikuwa limepinduka upande wa kulia wa barabara ukitokea Tanga. Wakati wakiendelea kufanya uokozi ghafla likaja lori lililokuwa linatoka Tanga kwenda Dar es Salaam likaligonga basi lile dogo lililokuwa limesimama.
“Wakati dereva wa lori anajaribu kulimiliki lori hilo ili litulie barabarani, ghafla alijikuta akigongana uso kwa uso na lori lingine ambalo lilikuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Arusha. Tukio hilo limesababisha wanakwaya 12 ambao ni raia wa Kenya kufa papo hapo na wengine 25, kujeruhiwa vibaya,” alisema Kamanda Mangu.
Kamanda huyo alisema kutokana na ajali hiyo, magari yaliyokuwa yakisafiri kati ya Dar es Salaam na mikoa ya Kaskazini zikiwemo pia nchi jirani za Kenya na Uganda yalishindwa kupita katika eneo hilo kutokana na malori hayo kufunga njia na hadi jana mchana jitihada za kuyaondoa malori hayo zilikuwa zinafanywa.
“Tunaendelea kutafuta ufumbuzi ili kuyaondoa malori hayo na magari yaweze kupita, tuna uhakika wa kukamilisha kazi hiyo mchana huu,” alisema Kamanda Mangu.
Kuhusu waliokufa katika ajali hiyo, Kamanda Mangu alisema walipelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili huku majeruhi wakikimbizwa katika Hospitali ya Tumbi, Kibaha na wengine Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.
Taarifa tulizopata baadaye zilisema kwamba majeruhi waliofikishwa Kibaha nao walipelekwa Muhimbili baada ya kufanyiwa huduma za kwanza.
Alisema dereva wa lori aliyeligonga basi hilo dogo la abiria anashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi.
Wakati huo huo, habari kutoka Kenya, zilizopatikana jana zilisema Rais wa Kenya, Mwai Kibaki ameagiza ndege za nchi hiyo kuja Tanzania kuwabeba majeruhi na kuwakimbiza katika hospitali za Kenya kwa matibabu zaidi.
Hata hivyo habari hizo hazikueleza ni lini ndege hizo zitawasili nchini ili kuwachukua majeruhi hao.
Basi la Ally's Sports likiwa limepinduka huku mbele yake likionekana basi la Sumry nalo likiwa limeingia porini katika ajali zilizosababishwa na utelezi barabarani.
Wakati huo huo, John Nditi anaripoti kutoka Morogoro kwamba abiria 29 kati ya 51 wamelazwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, kutokana na kupata majeraha baada ya kutokea ajali ya mabasi matatu katika eneo la Makunganya , wilayani Morogoro kwenye Barabara Kuu ya Morogoro- Dodoma.
Ajali hizo zilitokea jana kati ya saa 2: 50 asubuhi, ambapo ajali ya kwanza ilihusisha basi la Shabiby lenye namba za usajili T 425 BYS likitokea mkoani Dodoma kwenda jijini Dar es Salaam ambalo lilianguka na kuziba njia.
Wakati Basi hilo likiwa bado limeziba njia kwenye kona muda mfupi baadaye likatokea basi la Sumry lenye namba T 777 BWL aina ya Yutong kutoka jijini Dar es Salaam kwenda Mwanza lilishindwa kusimama na kwenda kujikita korongoni.
Kama haitoshi, basi jingine la Kampuni ya Allys Sports Bus lenye namba za usajili T 692 BKV nalo likifuata nyuma ya Sumry nalo lilishindwa kusimama na kuanguka kiubavu pia katika eneo hilo.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Morogoro, Leonard
Gyindo na timu ya uokoaji walifika asubuhi hiyo eneo la tukio na kuthibitisha kutokea kwa ajali hizo.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa huo, kuwa ajali hizo zilitokana na uzembe wa madereva na mwendo kasi.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Dk Rita Lyamuya, alikiri kupokea majeruhi 51 kati ya hao 29 wamelazwa katika wodi mbili tofauti wakiendelea vizuri na matibabu.
“ Tumepokea majeruhi 51 kati ya hao 22 wametibiwa na kuruhusiwa na wengine 29 tumewalaza wakiwemo wanaume 7 na waliobakia ni wanawake na watoto wadogo, ambao hali zao zinaendelea vizuri , isipokuwa watu wawili ndio wameonekana wameumia kwa kiwango kikubwa," alisema Dk Lyamuya.
Naye mmoja wa mashuhuda wa ajali ya kwanza , Edward Chiutila, alisema huenda ajali hiyo imechangiwa na utelezi kutokana na mvua zilizokuwa
zikinyesha asubuhi hiyo kwa vile dereva wake hakuwa katika mwendo kasi.
“ Nilikuwa mtu wa kwanza kwenda kuwasaidia kuwatoa majeruhi kwenye basi la Shabiby , lilikuwa ni eneo tambalale ...huenda utelezi umechangia kuanguka kwake,” alisema Chitula aliyeshuhudia ajali hiyo.


No comments:
Post a Comment