Wednesday, August 15, 2012

TANESCO YAWACHIMBA MKWARA MZITO WEZI WA UMEME...

Meneja Uhusiano wa Tanesco, Badra Masoud.
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limetoa onyo kwa wadaiwa sugu na wezi wa umeme nchini, kuwa baada ya wiki mbili, operesheni maalumu ya nyumba kwa nyumba itaendeshwa nchi nzima na watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Aidha, jana liliikatia umeme Shule ya Green Acres ya Salasala, Dar es Salaam baada ya kubaini kuwa imejiunganishia umeme na kuutumia kinyemela na kukwepa kuulipia.
Kwa mujibu wa Shirika hilo baadhi ya adhabu watakazopewa wahujumu hao wa umeme mbali na kuripotiwa Polisi na kupandishwa kizimbani, Sheria ya Mwenendo wa Madai Sura ya 33 itatumika na nyumba zao kutangazwa kwenye vyombo vya habari na kupigwa mnada.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu operesheni hiyo Dar es Salaam jana, Meneja Uhusiano wa Tanesco, Badra Masoud alisema hatua hiyo ni moja ya mikakati ya shirika hilo kudhibiti wahujumu wake.
"Mtu atakayebainika kutumia mita zetu kinyume cha sheria, kuzichezea, kukata lakiri, kutumia ‘vishoka’, kujirudishia umeme baada ya kukatiwa au kujiunganishia umeme kwa njia haramu, bila kujali cheo au umaarufu wake ‘tutamwanika’ na kumchukulia hatua," alisema Masoud.
Alisema operesheni hiyo itakuwa ya uwazi, kwa kuwa watakutanishwa na vyombo vya habari na Dola ili kudhibiti vitendo vyote viovu dhidi ya shirika hilo vinavyokwamisha maendeleo yake na kulikosesha mapato.
Masoud alisema Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Proches Mramba ametoa wiki mbili za wateja wenye wasiwasi na matatizo ya mita zao au wanaodhani kuwa wanatumia umeme usio wa halali kujisalimisha.
Masoud alisema ifikapo mwisho wa mwezi wanaoiba umeme au wenye wasiwasi kuhusu utendajikazi wa mita zao, watatakiwa kujisalimisha kwa mameneja wa mikoa vinginevyo sheria itachukua mkondo wake.
"Utaratibu huu pia unahuisha watumiaji umeme wanaoununua kwenye mifumo isiyotambuliwa na shirika, naomba wateja wote wahakiki stakabadhi zao na kujiridhisha kuwa umeme wanaotumia ni halali," alisisitiza.
Alisema wadaiwa sugu, wanatakiwa wajisalimishe kwenye ofisi za shirika na kulipa madeni yao kabla ya mwisho wa mwezi, kwani baada ya hapo nyumba zitapigwa mnada kufidia deni na tayari utaratibu wa kunadi nyumba za wadaiwa sugu umeanza katika baadhi ya mikoa.
Aidha, alisema Tanesco imebaini kuwa vituo vingi vya mafuta vinaiba umeme na kuvihadharisha ikivitaka kuacha ‘mchezo huo’ kwa kuwa shirika linajiandaa kukamilisha ushahidi na litakapokamilisha vitatajwa na kushitakiwa.
Akizungumzia suala la Green Acres, Mdhibiti wa Upotevu wa Mapato Tanesco, Stewartness Makiko, alisema shule hizo zimeiba umeme kwa kutumia mita moja iliyofungwa mwaka 2005 kwa nyaya tatu.
Alisema kati ya nyaya hizo mmoja tu ndio uliofungwa moja kwa moja kutoka Tanesco na ulikuwa ukitumika katika takriban maeneo yote ya shule bila gharama kuifikia Tanesco wakati nyaya zingine ziliunganishwa na mita ambayo mara ya mwisho ililipiwa Februari.
Mkurugenzi wa Shule hizo, Julian Bujugo alipoulizwa kuhusu sakata hilo aligoma kuzungumza na waandishi wa habari na kutaka kuzungumza na chombo kimoja tu cha habari.
Shirika hilo huingiza takriban Sh milioni 70 hadi 80 kwa mwezi kama mapato na pia asilimia 21 ya umeme hupotea kutokana na wizi na matatizo ya kiufundi huku kimataifa ikitakiwa umeme huo angalau upotee bila kuzidi asilimia 12.

No comments: