Wednesday, August 15, 2012

KASHFA NZITO YAKIKUMBA CHAMA CHA SKAUTI TANZANIA...

Baadhi ya Maskauti wakiwa katika moja ya mafunzo yao ya kawaida.
Chama cha Skauti Tanzania kimelipuliwa bungeni, kwamba kimeacha majukumu yake na kujihusisha na biashara haramu ya kusafirisha watu nje ya nchi na kuuza dawa za kulevya.
Mbunge wa Viti Maalumu, Susan Lyimo (Chadema) alitoa kauli hiyo jana wakati akichangia Bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iliyowasilishwa juzi na Waziri, Dk Shukuru Kawambwa.  
"Chama cha Skauti Tanzania kimeacha majukumu ya msingi na sasa kufanya biashara haramu kwa nchi yetu," alisema na kuongeza kuwa kimekuwa kikisafirisha watu wasiohusika kwenda nje.
Akionesha barua aliyosema ataiwasilisha kwa Spika Anne Makinda, Lyimo alisema viongozi wa chama hicho wamekuwa wakijihusisha na biashara hiyo.
Akielezea kitendo hicho kuwa ni hatari, Mbunge huyo alisema katika maadhimisho ya Jubilei ya Malkia Elizabeth II wa Ungereza, walipelekwa baadhi ya watu wasio wanachama wa Skauti.
Alisema wamekuwa wakitapeli watu kwa kuwachangisha fedha kwa kigezo cha kuwasafirisha kwenda nje.
Alitoa mfano kwamba kuna Mkurugenzi wa Shule alitoa Sh milioni 45 ili wanafunzi wake wapelekwe nje ya nchi na fedha hizo zikaliwa huku wanafunzi wakitelekezwa.
Alisema hadi sasa Mkurugenzi huyo amerejeshewa Sh milioni 21 na bado anaendelea kudai kiasi kilichosalia.
Mbunge wa Viti Maalumu, Christowaja Mtinda (Chadema) alilalamikia Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kutokana na kumwingiza kwenye orodha ya malipo ya mshahara wakati hajawahi kuajiriwa chuoni hapo.
Mtinda ambaye alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mkwawa, alishawahi kutoa malalamiko kama hayo katika moja ya mikutano ya Bunge siku za nyuma.
Jana aliliambia Bunge, kwamba baada ya malalamiko hayo, OUT  ilimtumia majibu ikimweleza kwamba alipata kuomba kazi chuoni hapo.
"Ukweli uliopo sikupata kuomba kazi Chuo Kikuu Huria kwa namna yoyote ile, nao walikiri kutokuwapo barua ya kuniajiri. Ni uongo na unajidhihirisha kwenye maelezo," alisema na kushutumu watendaji wanaopeleka ripoti zisizo sahihi na kusababisha wizara kufanya vitu visivyo sawa.
Aliomba Ofisa wa Chuo hicho Kanda ya Iringa, Dk Francis Chale atafutwe ili atoe taarifa za uhakika juu ya sababu ya kuingiza jina lake kwenye mshahara.
Aidha, Mbunge huyo alishutumu kitengo cha ununuzi cha Chuo cha Mkwawa kuwa kimefanya ubadhirifu wa fedha za ujenzi wa jengo mojawapo.
Mbunge wa Viti Maalumu, Betty Machangu (CCM) alizungumzia kitengo cha Ukaguzi kwa kutaka kiwezeshwe. Alisema wakaguzi wapo ofisi za wakurugenzi na hawawezeshwi vya kutosha, hawana magari na wala mafuta ya kuwezesha ukaguzi.
Alisema wapo walimu wanaokwepa vipindi  ambao ukaguzi ndio ungeweza kuwanasa kwa kuangalia wanavyoandaa masomo yao.
Lyimo pia alizungumzia kitengo cha ukaguzi na kutoa mfano wa Dodoma kuwa ofisi zimo katika jengo la Kikosi cha Zimamoto.
Mbunge wa Bukoba Vijijini, Jason Rweikiza (CCM) alitaka Serikali kuangalia upya utaratibu wa kuwashusha madaraja wanafunzi wanaoshindwa somo la Hisabati kwa kusema kufanya hivyo ni kutowatendea haki.
Mbunge wa Rungwe Magharibi, Profesa David Mwakyusa (CCM) alipongeza hatua za Serikali katika kuongeza idadi ya walimu. Hata hivyo, alishauri ujenzi wa maabara uzingatiwe.
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) alisema Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inabebeshwa mzigo ambao ulipaswa kubebwa na wizara nyingine miongoni mwao ikiwa ni yenye mamlaka ya Utumishi wa Umma.
Alitaka mjadala kuhusu wizara hiyo uwe fundisho kwao ili ikija Bajeti Kuu ya Serikali waungane kupiga kura ya kuikataa.
Mnyika ambaye hakuunga mkono bajeti hiyo, alisema kilio kikubwa cha wabunge ni bajeti ndogo. Alitaka Serikali katika majumuisho, ieleze utayari wake wa kuleta bajeti ya nyongeza kwa ajili ya wizara hiyo ili kuboresha hali za walimu na mambo mengine.

No comments: