Thursday, August 16, 2012

SEKONDARI KUSIMAMIA MITIHANI SHULE ZA MSINGI...

Baadhi ya wanafunzi katika moja ya Shule za Msingi hapa nchini wakiwa darasani.
Katika kukabiliana na wimbi la udanganyifu katika mitihani, Serikali imetangaza kuchukua hatua kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuanzisha utaratibu wa walimu wa sekondari kusimamia mitihani ya shule za msingi.
Aidha, kuanzia mwaka huu, idadi ya wanafunzi katika chumba cha mtihani itapunguzwa kutoka 30 hadi 25 kwa shule za msingi na sekondari, lengo likiwa kupunguza msongamano unaosababisha wanafunzi kutazamiana katika majibu yao.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alipotoa kauli ya Serikali kuhusu hatua zilizochukuliwa kwa waliohusika na udanganyifu wa mitihani ya darasa la saba na ya kidato cha nne mwaka jana.
Dk Kawambwa alisema Serikali haitasita kuzifutia usajili shule zinatakazobainika kuhusika na vitendo vya udanganyifu kwenye mitihani.
"Pamoja na hayo tutazielekeza kamati za mitihani za mkoa na halmashauri kuteua mapema walimu waadiilifu kwa ajili ya usimamizi wa mitihani na majina yao kuhakikiwa na vyombo vya usalama kabla ya kusimamia mitihani," alisema.
Waziri alitumia fursa hiyo kuliarifu Bunge kuwa mitihani ya kumaliza elimu ya msingi itafanyika kote nchini Septemba 19 na 20.
Alitaka maofisa elimu wa mikoa na wilaya kushirikiana na kamati za uendeshaji mitihani za mikoa na wilaya kuhakikisha taratibu za uendeshaji zinazingatiwa ipasavyo.
"Napenda pia kuasa wasimamizi wote wa mitihani, walimu wakuu na wakuu wa shule kuhakikisha wanazingatia kikamilifu taratibu za usimamizi na uendeshaji mitihani, kwani wizara haitasita kuchukua hatua kali kwa watakaobainika kufanya udanganyifu katika mitihani," alisema.
Katika mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi mwaka jana, watahiniwa 9,736 kati ya 983,545 walibainika kudanganya. Na uchunguzi ulibaini walimu 422 kushiriki, kama ilivyokuwa kwa walimu na wasimamizi 250. Wamiliki na mameneja wa shule pia walibainika kuhusika.
Kutokana na makosa hayo, wanafunzi hao walifutiwa matokeo, walimu wakuu 176 walivuliwa madaraka, huku walimu wakuu 246 na wasimamizi 312 waliohusika wakizuiwa kusimamia mitihani kwa kati ya miaka mitatu na mitano.
Kwa upande wa sekondari, wanafunzi 3,303 kutoka shule 91, kati ya hizo 75 zikiwa za Serikali walibainika kujihusisha na udanganyifu katika mitihani ya kidato cha nne. Walimu 140, wakuu wa shule 48 na wasimamizi 92 nao walihusishwa.
Mwaka huo, wanafunzi 339,330 walifanya mtihani, huku 180,216 wakifaulu, idadi ambayo ni sawa na asilimia 53.2 ya watahiniwa wote.
Pamoja na adhabu za aina tofauti kwa wahusika, ikiwa ni pamoja na wanafunzi kufutiwa mitihani, Serikali imewaandikia wamiliki wa shule 13 barua za kusudio la kuzuia udahili wa kidato cha kwanza kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia mwaka 2013.
Aidha, wameagizwa kuwachukulia hatua wakuu wao wa shule na walimu waliohusika katika udanganyifu.

No comments: