Thursday, August 16, 2012

MWALIMU ACHUNGUZWA KWA KUWATEMBEZA UCHI WANAFUNZI WALIOFELI JARIBIO...

Polisi mkoa wa Temeke, Dar es Salaam imesema inaandaa jalada kwa ajili ya mwalimu wa Shule ya Msingi Mtakatifu Benedict aliyewavua nguo wanafunzi wanne kutokana na kufeli jaribio alilotoa na kubaki uchi.
Akizungumza jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, David Misime alisema tukio hilo lilifanyika Julai 5 wakati mwalimu huyo akifundisha somo la Historia darasa la nne shuleni hapo.
Alisema baada ya Polisi kuandaa jalada imeliwasilisha kwa wakili wa Serikali ili alisome na kuandaa hati ya mashitaka tayari kufungua kesi mahakamani.
Kuhusu tukio hilo, Kamanda Misime alisema wakati akifundisha, mwalimu huyio ambaye jina lake linahifadhiwa kwa sasa, aliwaambia wanafunzi hao kuwa anatoa jaribio la somo hilo na kwamba atakayefeli, atavuliwa nguo na kutembea uchi darasani.
Baada ya jaribio hilo kumalizika, wanafunzi wanne walifeli na kulazimika kutii amri ya mwalimu ya kutembea uchi na baadhi yao wakibaki na nguo za ndani.
"Baada ya hali hiyo mmoja wa wanafunzi hao hakuridhishwa na kitendo hicho na kwenda kushitaki kwa mzazi ambaye alitoa taarifa kituoni," alisema Misime na kuongeza kuwa baada ya kuchunguza, ndipo Polisi ilipobaini idadi hiyo ya wanafunzi.

No comments: