Ufukwe wa Ziwa Nyasa.
Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kukutana na Rais wa Malawi, Joyce Banda, kuzungumzia mgogoro unaofukuta wa umiliki wa Ziwa Nyasa ambalo Malawi inalitambua kama Ziwa Malawi.Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, John Haule amethibitisha kuwapo kwa mkutano huo unaotarajiwa kufanyika jijini Maputo, Msumbiji wakati viongozi hao wakihudhuria mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
"Ni kweli marais hawa wanatarajia kukutana, mimi tayari nipo Maputo kwa ajili ya mkutano huo na wa SADC, lakini siwezi kukwambia watakutana lini na maelezo zaidi wasiliana na Ikulu ndio wahusika," alisema Haule.
Kwa mujibu wa gazeti la Malawi, Nyasa Times, tayari Banda ameondoka nchini humo kwenda Msumbiji kuhudhuria mkutano wa SADC, lakini pia akiwa nchini humo atakutana na Rais Kikwete kuzungumzia mgogoro huo.
Msumbiji ndio mwenyeji wa mkutano wa SADC wa 32 unaokutanisha wakuu wa nchi wanachama utakaofanyika Agosti 17 na 18.
Kwa mujibu wa gazeti hilo marais hao wakiwa kwenye mkutano huo watapata fursa ya kukutana na kikubwa watakachojadili ni namna ya kupunguza wasiwasi ulioibuka baina ya Watanzania na Wamalawi kutokana na mgogoro huo.
Wakati mkutano huo ukitarajiwa kufanyika, tayari mawaziri wa mambo ya nje wa Tanzania na Malawi, wanatarajiwa kukutana Agosti 27, kwa ajili ya kujadili mustakabali wa mgogoro huo.
Aidha, mkutano wa Kamati ya Wataalamu wa nchi hizo mbili umepangwa kufanyika Agosti 20 ukiongozwa na Haule na wajumbe takribani 20 wa Tanzania na unatarajiwa kufanyika Mzuzu, Malawi.
Mazungumzo ya mikutano yote miwili ya wataalamu na mawaziri yatahusu suluhu ya mgogoro huo ambao Malawi inadai Ziwa lote ni mali yake na kuanza kufanya utafiti wa mafuta na gesi hadi upande wa Tanzania.
Tanzania nayo imebainisha wazi na kutumia ramani na taarifa za kihistoria kuhusu umiliki wa Ziwa hilo na kusisitiza kuwa asilimia 50 ya Ziwa ni mali yake na kuitaka Malawi isimamishe mara moja utafiti wa nishati hiyo unaofanya katika eneo hilo na kwamba iko tayari kwa lolote katika kutetea haki yake.
Nchi wanachama wa SADC ni pamoja na Angola ambao sasa ndio wanashikilia nafasi ya uenyekiti, Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Lesotho, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini, Swaziland, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.
No comments:
Post a Comment