Thursday, August 23, 2012

MKUU WA WILAYA SERENGETI AFARIKI DUNIA..

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Kapteni mstaafu James Yamungu amefariki dunia jana asubuhi kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam alikokuwa amelazwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Tupa, Yamungu alifariki dunia jana asubuhi ikiwa ni siku moja baada ya kufikishwa hapo akitokea katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza.
"Kapteni James Yamungu alianza kuugua tangu Agosti 16 mwaka huu na kulazwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Serengeti. Siku hiyo hiyo tulimsafirisha kwenda Hospitali ya Rufaa ya Bugando Mwanza. Alikaa hapo hadi Agosti 21, mwaka huu tulipomleta katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa uchunguzi na matibabu zaidi, lakini leo asubuhi (jana) akafariki dunia," alisema Tupa alipozungumza na gazeti hili.
Kwa mujibu wa Tupa, DC Yamungu alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa moyo, na anatarajiwa kuzikwa katika mji wake, Kibaha mkoani Pwani kesho, katika maziko yanayotaratibiwa na wakuu wa mikoa ya Pwani na Dar es Salaam kwa ushirikiano na mkuu huyo wa mkoa wa Mara.
Kabla ya kuhamia Serengeti, Mei 16, mwaka huu katika uteuzi uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete, DC Yamungu alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Maswa mkoani Shinyanga, na pia amewahi kuwa DC katika Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani na pia Mbunge katika Jimbo la Kinondoni mkoani Dar es Salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Mara alimsifu DC Yamungu kwa uchapakazi na kukubalika haraka wilayani Serengeti ambako ameiongoza wilaya hiyo kwa miezi mitatu na usheee.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Tupa kuomboleza kifo cha DC Yamungu.
"Nimepokea kwa huzuni na mshituko taarifa za kifo cha Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Kapteni Mstaafu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, Mheshimiwa James Yamungu," alisema Rais Kikwete na kuongeza:
"Kifo cha Kapteni Yamungu kimeinyang’anya nchi yetu na Serikali yetu mtumishi hodari na mwadilifu wa umma ambaye katika utumishi wake wote tangu alipokuwa Jeshi hadi anaingia uongozi wa siasa, alithibitisha uaminifu wake kwa nchi yetu na uongozi wake."
"Kutokana na msiba huu mkubwa, nakutumia wewe Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Tupa, salamu zangu za rambirambi, na kupitia kwako naitumia salamu zangu za dhati kabisa familia ya marehemu, wana-Mara na Wana-Serengeti wote ambako ndiko kwanza alikuwa ameripoti kuanza kazi yake ya ukuu wa wilaya hiyo," alisema Rais Kikwete.

No comments: