Aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba (pichani) amekana kuhusika kuleta nchini kampuni ya kukagua madini ya Alex Stewart, na kudai alifanya kazi baada ya kampuni hiyo kufika kwa maelekezo ya Rais wa wakati huo, Benjamin Mkapa.
Akijitetea jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwenye kesi inayomkabili ya matumizi mabaya ya ofisi na kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 11.7, Mramba alidai kutohusika kutafuta kampuni hiyo wala kuiingiza nchini.
Katika kesi hiyo, Mramba na wenzake wanadaiwa kutoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo, jambo lililosababisha hasara hiyo kwa Serikali.
Ili kuthibitisha kutohusika kwake, Mramba akiongozwa na Wakili Hurbert Nyange, alitaja baadhi ya mashahidi atakaoleta katika kesi hiyo kuwa ni pamoja na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Andrew Chenge.
Mbali na Chenge ambaye sasa ni Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), wengine ambao alidai atawaita kama mashahidi wake ni Gavana wa Benki Kuu (BoT) au mwakilishi, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali, John Cheyo (UDP) na mtaalamu wa masuala ya kodi, Florian Busigara.
Pia alidai pia atamwita mwakilishi wa kampuni ya Alex Stewart na shahidi mwingine ambaye alidai hajathibitisha ujio wake, hivyo atatajwa wakati wakiendelea kujitetea.
Mramba alidai kuwa chimbuko la kesi hiyo ni malalamiko ya wabunge, wananchi na vyombo vya habari kuwa nchi yetu ina migodi kadhaa lakini wananchi hawanufaiki nayo na kwamba migodi hiyo ilikuwa ikidanganya juu ya uzalishaji na uuzaji wake wa madini nje ya nchi.
"Serikali iliiteua BoT kumtafuta mkandarasi anayefaa kufanya kazi hiyo … ilifanya hivyo na kuingia mkataba na kampuni hiyo, baada ya kutangaza nafasi hiyo kwenye mtandao na kupata wazabuni," alifafanua Mramba katika madai yake.
Aliendelea kudai kuwa BoT ilifanya kazi hiyo kwa maelekezo ya Rais Mkapa ambapo yeye kama Waziri wa Fedha wa wakati huo, alipewa jukumu la kumlipa mshauri huyo kwa kutumia fedha kutoka ndani ya Serikali au BoT au kwa kushirikiana.
Baada ya ushahidi wa Mramba, Mahakama ikiongozwa na mahakimu wanaosikiliza kesi hiyo, John Utamwa, Saul Kinemela na Sam Rumanyika, iliahirisha kesi hiyo hadi leo saa 7 mchana, ushahidi utakapoendelea kutolewa.
Leo pia mahakama itatoa uamuzi juu ya barua kivuli ambayo Mramba alitaka kuitoa kama kielelezo, lakini upande wa mashitaka ulipinga isipokewe bila saini ya mtoa barua hiyo.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini katika Awamu ya Tatu, Daniel Yona na Katibu Mkuu mstaafu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Gray Mgonja.
Endapo mahakama itaamua kumwita Mkapa kutoa ushahidi katika kesi hiyo, itakuwa ni mara ya pili katika kipindi kifupi kwa kiongozi huyo mstaafu kutinga kizimbani kutoa ushahidi.
Hivi karibuni, Mkapa alitinga katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumtetea aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Coster Mahalu katika kesi iliyokuwa ikimkabili ya kuisababishia Serikali hasara ya mabilioni ya fedha. Mahalu alishinda kesi hiyo.

No comments:
Post a Comment