Thursday, August 23, 2012

MAKARANI WATISHIA KUGOMEA ZOEZI LA SENSA...

Zikiwa zimesalia siku chache kabla ya kufanyika kwa Sensa ya Watu na Makazi, makarani ambao watafanya kazi hiyo mkoani Dar es Salaam wametishia kugoma mpaka watakapolipwa malipo yote ya posho ya mafunzo na ya kuanza kazi.
Hali hiyo imejitokeza baada ya kuibuka mkanganyiko kuhusu malipo hayo kwa makarani waliokuwa wakipata mafunzo ya uendeshaji wa sensa hiyo na kulipwa viwango tofauti.
Utata huo tayari umeripotiwa katika wilaya zote za mkoa wa Dar es Salaam na kufanya makarani hao kugoma kula kiapo cha utii na kutunza siri katika kazi hiyo itakayofanyika Agosti 26, wakitaka walipwe kwanza fedha wanazodai kabla ya kuapa na kuanza kazi rasmi.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mmoja wa makarani hao, Glady Theonest wa Kinondoni alisema wamekuwa wakizungushwa malipo yao kwa watakaotumia dodoso refu na fupi, huku malipo ya siku yakikatwa bila maelezo yoyote.
Theonest alidai kuwa pamoja na kutakiwa kupewa malipo hayo tangu juzi, wamekuwa wakifika kwenye vituo walivyoelekezwa bila mafanikio na jana walipaji walifika lakini kabla ya kulipa, waliwataka wale kiapo kwanza jambo lililozua zogo.
Alidai kituo chao cha malipo katika Sekondari ya Mtakuja, Kunduchi, kinajumuisha kata za Kawe, Bunju, Mbweni, Wazo, Makongo Juu, Mbezi na Kunduchi ambazo zina zaidi ya makarani 1,500 wanaodai malipo ya siku sita ya Sh 210,000 kila mmoja, kwa wa dodoso refu.
"Haya ni madai ya ambao tunahusika na dodoso refu, wenzetu wa dodoso fupi nao wana madai yao ambayo kwa kiasi yanafanana na yetu, lakini kutokana na ubabaishaji wa malipo ya mafunzo, yale ya dodoso la jamii yameshindikana kufanyika," alisema.
Malalamiko mengine yanatoka kwa makarani ambao walitakiwa kukusanyika katika sekondari ya Turiani, Magomeni tangu juzi ili kulipwa na kuapishwa, lakini kazi hiyo haikufanyika na kuingiwa na wasiwasi kuwa huenda wasipate malipo hayo.
Hali hiyo ilisababisha vurugu na kusababisha Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana kwenda kuwatuliza na kuwaelezea sababu iliyochangia kuchelewa kwa malipo yao ambapo alibainisha tatizo hilo lilitokana na masuala ya kibenki.
Alipotafutwa na gazeti hili kuzungumzia suala hilo, Rugimbana ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Sensa wa Wilaya hiyo, alikiri kuwapo tatizo hilo na kuahidi kuwa hadi leo wote watakuwa wamelipwa, kwa kuwa malipo hayo yalianza jana kwa makarani wote wa Kinondoni ambao wamegawanywa katika kata saba.
Rugimbana alisema maandalizi ya sensa yanaendelea vizuri na vifaa vyote kwa ajili ya kazi hiyo vilitarajiwa kukabidhiwa kwa wahusika jana, ikiwa ni pamoja na makarani wote kuapishwa.
Hali kama hiyo nayo ilitokea kwa makarani ambao wamekuwa wakikusanyika katika shule ya msingi Buguruni wilayani Ilala kuanzia saa moja asubuhi hadi wakati mwingine saa 4 usiku bila kulipwa stahiki yao.
Ofisa kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Said Ameir alikiri kuwapo ucheleweshaji wa malipo hayo na kubainisha kuwa tatizo hilo linatokana na kuchelewa kufika kwa fedha za malipo hayo ambazo hutakiwa kupelekwa katika akaunti za halmashauri husika kupitia benki mbalimbali.
Akizungumzia tatizo hilo kwa upande wa Dar es Salaam, Ameir alisema tatizo lingine mbali na masuala ya kibenki, ni idadi kubwa ya makarani ambao wanakadiriwa kuwa zaidi ya 18,900 wakati watoa malipo ni wachache.
Aliwatoa hofu makarani hao na kuwataka kuwa wavumilivu kwani fedha za malipo yao yote zipo na hakuna mtu atakayedhulumiwa fedha yake aliyostahili kulipwa.

No comments: