Monday, July 23, 2012

HOTUBA YA WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA NA WATOTO KWA MWAKA 2012 - 2013...


HOTUBA YA WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA NA WATOTO MHESHIMIWA SOPHIA MNYAMBI SIMBA (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2012/13
A:     UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, kutokana na taarifa iliyowasilishwa leo hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii na kwa kuzingatia taarifa hiyo, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako tukufu lipokee, lijadili na kupitisha Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Wizara yangu kwa mwaka wa 2012/13.
Mheshimiwa Spika,  awali ya yote, napenda kutumia nafasi hii kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii ikiongozwa na Mwenyekiti wake mahiri Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama (Mb.) na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Juma Selemani Nkamia (Mb.) kwa kuchambua na kujadili bajeti ya Wizara yangu. Ushauri na maelekezo ya Kamati hiyo yameiwezesha Wizara kuandaa na kuboresha bajeti yake.
Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa imani yake kwangu na kunipa dhamana ya kuiongoza Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto. Ninaahidi kuwa nitajitahidi kwa kadri ya uwezo wangu kuendelea kutekeleza majukumu niliyopewa kwa kushirikiana na watumishi wenzangu na wadau wengine wote ndani na nje ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, Naomba pia kutumia fursa hii, kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa umahiri wake katika kuongoza nchi yetu kwa amani na utulivu. Chini ya uongozi wake Serikali imetekeleza kwa kiwango kikubwa ahadi alizotoa kwa wananchi wakati wa uchaguzi Mkuu na kama zilivyoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2010. Mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wake yamewezesha kuendelea kukua kwa uchumi wa nchi yetu na kuwavutia wawekezaji kuendelea kuwekeza nchini na washirika wa Maendeleo kuona umuhimu wa kuendelea kuiunga mkono Serikali.
Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Mohammed Gharib Bilal kwa uongozi wake bora. Nampongeza pia Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb.) kwa kusimamia vema shughuli za serikali na utekelezaji wake. Aidha Hotuba aliyoitoa kwenye Bunge lako tukufu wakati akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya mwaka 2012/2013 ni kielelezo cha ukomavu wake katika uongozi na imeonyesha mwelekeo  na dira ya utekelezaji wa shughuli za serikali kwa mwaka 2012/2013. Nampongeza pia Waziri wa Fedha Mheshimiwa Dkt. Willam Augustao Mgimwa (Mb.) kwa Hotuba yake ambayo imeainisha misingi ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2012/2013.  Pia nampongeza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Mhe. Stephen Masato Wasira (Mb.) kwa hotuba yake kuhusu hali ya Uchumi ya mwaka 2011/2012 na Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2012/2013.
Mheshimiwa Spika, napenda kuwapongeza wafuatao kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Mawaziri kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Dkt. William Augustao Mgimwa (Mb.), kuwa Waziri wa Fedha; Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali H. Mwinyi (Mb.) kuwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii; Mheshimiwa Balozi Khamis Sued Kagasheki (Mb.) kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii; Mheshimiwa Prof. Sospeter M. Muhongo (Mb.) kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Mheshimiwa Dkt. Harrison G. Mwakyembe (Mb.) kuwa Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa Dkt. Fenella E. Mukangara (Mb.) kuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Dkt. Abdallah O. Kigoda (Mb.) kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Inj. Christopher K. Chiza (Mb.) kuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika na Mheshimiwa Prof. Mark J. Mwandosya (Mb.) kuwa Waziri asiye na Wizara maalumu.  Halikadhalika nampongeza Mheshimiwa James Mbatia (Mb.) kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Mbunge.
Mheshimiwa Spika, nawapongeza pia Waheshimiwa Alhaj Adam Omar Kimbisa (Mb.), Mheshimiwa Shy-Rose Saddrudin Banji (Mb.), Mheshimiwa Anjela Charless Kizigha (Mb.), Mheshimiwa Maryam Ussi Yahaya (Mb.), Mheshimiwa Ndirakindo Perpetua Kessy (Mb.), Mheshimiwa Dkt. Twaha Issa Taslima (Mb.), Mheshimiwa Abdullah Ali Hassan Mwinyi (Mb.), Mheshimiwa Bernard Musomi Murunyana (Mb.) na Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere (Mb.) kwa kuchaguliwa kuwa Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki. Nawatakia kila la kheri katika kutekeleza majukumu yao ya kuiwakilisha nchi yetu katika Bunge hilo.
Mheshimiwa Spika, nakupongeza wewe binafsi kwa umahiri wako  katika kusimamia na kuratibu shughuli za Bunge kwa ufanisi na umakini mkubwa.  Nawapongeza pia, Mheshimiwa Naibu Spika Job Yustino Ndugai, Mbunge wa Kongwa na Waheshimiwa Wenyeviti wa Bunge kwa kukusaidia kuliongoza Bunge vizuri.
Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa natoa salamu za rambirambi kwa familia ya Marehemu Musa K. Silima aliyekuwa Mbunge mteule kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Jeremiah Solomon Sumari aliyekuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki na Regia Estelatus Mtema aliyekuwa Mbunge Viti Maalumu Morogoro. Michango yao katika Bunge lako Tukufu itakumbukwa daima. Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema peponi, Amina.
Mheshimiwa Spika, hotuba yangu itazungumzia maeneo manne (4) ambayo ni: Mapitio ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2010; Hali halisi ya Sekta ya Maendeleo ya Jamii na changamoto zilizopo; Utekelezaji wa mpango wa Mwaka 2011/12;  Malengo ya mwaka 2012/13 na maombi ya fedha za utekelezaji wa mpango wa mwaka 2012/13.

B: MAFANIKIO YA UTEKELEZAJI WA ILANI YA UCHAGUZI YA CCM YA MWAKA 2010  KWA KIPINDI CHA JANUARI 2011 HADI MACHI 2012
Mheshimiwa Spika, yafuatayo ni mafanikio ya Wizara yangu katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi kwa kipindi cha Januari 2011 hadi Machi 2012. 
Ajira na Uwezeshaji wa Wananchi
Mheshimiwa Spika, Ilani ya CCM, Ibara ya 78 imeelekeza kuimarisha na kupanua mafunzo ya vyuo vya maendeleo ya wananchi ili vipokee vijana wengi zaidi na kuwapatia mafunzo ya maarifa ya kisasa katika fani za kilimo, biashara, ufundi stadi na ujasiriamali.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia vyuo 55 vya  maendeleo ya wananchi imetoa mafunzo ya  maarifa na stadi mbalimbali kwa wananchi 62,702 wakiwemo wanawake 29,764 na wanaume 32,938 ili kuinua viwango vya uzalishaji kwenye kazi zao. Hii ni sawa na asilimia 96.8 ya lengo. Aidha, Wizara ilifanya ukarabati mdogo katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Muhukuru. 
Elimu ya Juu
Mheshimiwa Spika, Ibara ya 85 ya Ilani ya CCM imeelekeza kuongeza udahili wa wanafunzi katika vyuo vya elimu ya juu. Katika kutekeleza azma hii, Wizara kupitia Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru iliendelea kudahili wanafunzi katika shahada ya kwanza ya fani za upangaji na usimamizi shirikishi wa miradi, maendeleo ya jamii, maendeleo ya jinsia na stashahada ya uzamili ya maendeleo ya jamii. Jumla ya wanafunzi 173 wakiwemo wanawake 103 na wanaume 70 walidahiliwa. 
Kuyaendeleza Makundi mbalimbali
Mheshimiwa Spika, katika Ibara za 204 na 205 ya Ilani ya CCM ya Mwaka 2010, imeelekezwa kuwa mikataba ya haki za wanawake na watoto iliyoridhiwa itekelezwe kikamilifu. Katika kutekeleza azma hiyo, Wizara imeandaa rasimu ya tafsiri ya Sheria ya Mtoto Na. 21 ya Mwaka 2009 katika lugha ya Kiswahili, na  kukamilisha Taarifa ya tatu, nne na tano ya Nchi kuhusu Utekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto na kuiwasilisha katika Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Mtoto. 
Mheshimiwa Spika, mafanikio mengine ni pamoja na Wizara kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu kupitia Benki ya Wanawake Tanzania na Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake.  Hadi kufikia mwezi Machi 2012, Benki ya Wanawake Tanzania ilitoa mikopo yenye thamani ya shilingi 1,285,550,000 kwa wanawake 5,270 na wanaume 1,157. Aidha, Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake umetoa mikopo yenye thamani ya shilingi 120,000,000 katika halmashauri 15 zilizofanya marejesho ya mikopo ya awali.
Mheshimiwa Spika, katika kudhibiti ukatili dhidi ya wanawake,  Wizara imeunda na kuzindua Kamati ya Kitaifa ya Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto.  Aidha, imeandaa Mwongozo wa Kudhibiti Ukatili wa Kijinsia na Mkakati wa Kitaifa wa Kuzuia Ukatili wa Kijinsia Nchini  kwa lengo la kutumiwa na kamati za ukatili wa kijinsia, ulinzi na usalama katika ngazi za mikoa,  halmashauri za wilaya pamoja na wadau wengine Nchini. 
Mheshimiwa Spika, Ibara ya 188 ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2010, imeelekeza kuhakikisha kwamba Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) yanajishughulisha na majukumu ambayo yameandikishwa kufanya na kwamba hayapati nafasi ya kujiendesha kinyume na makusudio hayo.  Katika kutekeleza azma hiyo, Wizara iliendelea kuelimisha wananchi kuhusu matakwa ya Sera ya Taifa ya NGOs (2001), Sheria ya NGOs Na. 24 (2002) na Kanuni za Maadili ya NGOs kwa wadau 4,047. Wadau hao walitoka katika taasisi za elimu, taasisi za fedha, taasisi za kiserikali, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na watu binafsi. Fursa zilizotumika kutoa elimu hii ni kupitia Ofisi ya Msajili wa NGOs, mikutano ya Bodi ya Taifa ya Uratibu wa NGOs, Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma na Maonesho ya Sabasaba kwa lengo la kuwawezesha kukidhi matakwa ya sheria, taratibu za usajili na kutoa taarifa kwa Msajili wa NGOs pindi mashirika hayo yanapojiendesha kinyume na taratibu zilizowekwa.

C: HALI HALISI YA SEKTA YA MAENDELEO YA JAMII NA CHANGAMOTO ZILIZOPO
Mheshimiwa Spika, hali ya sekta ya maendeleo ya jamii kwa ujumla imeendelea kuimarika. Kuimarika kwa sekta kumetokana na ushirikiano mzuri tulioupata kutoka kwa wadau wetu katika kutekeleza majukumu ya Wizara. Majukumu yalilenga kufanikisha uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, usawa wa kijinsia, upatikanaji wa haki za mtoto na uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. 
Mheshimiwa Spika, hali ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kupitia vyuo vya maendeleo ya wananchi inaridhisha. Vyuo vimeendelea kutoa mafunzo ya stadi na maarifa yanayowezesha wananchi  kujiajiri na kuajiriwa, hivyo, kuwapunguzia umaskini. Udahili wa wananchi katika vyuo hivi umeongezeka kutoka 31,877 mwaka 2010/11 na kufikia 32,133 mwaka 2011/12. Vyuo hivi kwa sasa vina umuhimu mkubwa kutokana na ukweli kwamba vinadahili idadi kubwa ya vijana waliomaliza elimu ya msingi na sekondari ambao hawakufanikiwa kuendelea na mafunzo ya juu. Pamoja na umuhimu wa vyuo hivi, hali ya majengo na miundombinu yake bado ni chakavu kutokana na ukosefu wa matengenezo ya mara kwa mara. Changamoto nyingine ni uhaba wa vyombo vya usafiri, upungufu mkubwa wa watumishi wa kada mbalimbali, nyumba za watumishi, madarasa, karakana, mabweni, vifaa na mitambo ya kufundishia na kujifunzia. 
Mheshimiwa Spika, idadi ya wataalamu wa maendeleo ya jamii katika ngazi za Taifa, mkoa na halmashauri ni ya kuridhisha. Hali hii imesababisha ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo kuendelea kuimarika. Ushiriki huu umetokana na matumizi ya mbinu shirikishi katika uandaaji na utekelezaji wa programu mbalimbali za maendeleo zinazowezeshwa na wataalamu hawa katika ngazi ya kata na vijiji. Changamoto inayokabili eneo hili ni upungufu wa wataalamu wa maendeleo ya jamii katika ngazi ya kata. Hivi sasa ni kata 1,329 tu kati ya kata 3,321 zenye wataalamu hawa, sawa na upungufu wa asilimia 60. 
Mheshimiwa Spika,  jitihada za kufikia usawa wa kijinsia na kuwapatia uwezo wanawake kupitia programu mbalimbali za maendeleo zimeendelea kuimarika.  Hii inatokana na Serikali kutambua kuwa usawa wa kijinsia na uwezeshwaji wa wanawake ni masuala muhimu kufikia maendeleo. Maeneo ambayo yamezingatia usawa wa kijinsia ni pamoja na nafasi za uongozi katika ngazi mbalimbali, mfano, uwakilishi wa wanawake katika Bunge, halmashauri za Wilaya na taasisi mbalimbali za Serikali. Aidha, udahili wa wanafunzi katika shule za msingi, sekondari na vyuo umezingatia usawa wa kijinsia. Pamoja na mafanikio hayo, bado zipo changamoto ambazo zinakwamisha juhudi za kuleta usawa wa kijinsia. Mpaka sasa bado zipo mila, desturi na imani potofu ambazo zinaendelea kuathiri haki ya wanawake katika masuala ya kutoa maamuzi na kushika nafasi mbalimbali za uongozi. Aidha, suala la mimba na ndoa za utotoni zinachangia katika kudhoofisha maendeleo ya elimu ya wanawake.
Mheshimiwa Spika, jitihada nyingine ambazo Wizara imefanya katika kuleta usawa wa kijinsia ni kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake, mila zenye madhara kwa wanawake na watoto wa kike, ukatili kwa watoto na albino. Aidha, Wizara imeandaa Mwongozo na Mkakati wa Kitaifa wa Kuzuia Ukatili wa Kijinsia Nchini  kwa lengo la kutumiwa na kamati za ukatili wa kijinsia, ulinzi na usalama katika ngazi ya mkoa na halmashauri pamoja na wadau wengine nchini. 
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya Mwaka 2008 na Sheria ya Mtoto Na. 9 ya Mwaka 2009 ili kuleta maendeleo na upatikanaji wa haki za mtoto kote Nchini.  Baadhi ya jitihada ambazo zimefanyika ni pamoja na kuratibu maandalizi ya seti saba (7) za kanuni za utekelezaji wa Sheria ya Mtoto Na. 21 (2009). Seti hizo za kanuni ni pamoja na: Makao ya Watoto; Kuasili; Shule za Maadilisho; Mahabusu ya Watoto; Apprenticiship; Creches; na Kulelea Watoto Mchana. Aidha, seti nne (4) za kanuni zinafanyiwa kazi. Lengo ni kuhakikisha kuwa watoto wanalindwa dhidi ya vitendo mbalimbali vya kikatili na hatimaye kuishi katika mazingira salama. Changamoto iliyopo katika utoaji wa haki za msingi za mtoto ni pamoja na ongezeko la watoto wanaoishi/kufanya kazi mitaani, tatizo la VVU na UKIMWI na kuongezeka kwa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vinavyofanywa na wazazi/walezi. Mmomonyoko wa maadili pamoja na umaskini uliokithiri miongoni mwa jamii ya Watanzania ni kati ya sababu kuu zinazochangia ongezeko la watoto wanaoishi/kufanya kazi mitaani. 
Mheshimiwa Spika, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yamekuwa yakiongezeka na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.  Hivi sasa kuna jumla ya mashirika 6,669 yaliyoandikishwa chini ya Sheria ya NGOs Na. 24 ya Mwaka 2002, kati ya hayo mashirika 5,837 yamepatiwa cheti cha usajili na mengine 832 yalipatiwa cheti ya ukubalifu.  Mashirika haya yanafanya kazi katika ngazi ya wilaya, mkoa, taifa na kimataifa. Aidha, shughuli za mashirika haya zimejikita katika nyanja mbalimbali za maendeleo ikiwemo haki za binadamu, maendeleo ya jinsia, afya, elimu, maendeleo shirikishi, kilimo, mazingira, haki za watoto, ustawi wa jamii na utetezi kuhusu sera mbalimbali. Changamoto zinazokabili NGOs kwa sasa ni utegemezi mkubwa kwa wafadhili na kutokuwepo mfumo madhubuti wa kubainisha michango yao katika maendeleo ya Taifa.

D: UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MWAKA 2011/12 NA MALENGO YA MWAKA 2012/13
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12 Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali iliendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi. Aidha, katika mwaka 2012/13 maeneo matatu (3) yafuatayo yamepewa kipaumbele: 

Kuimarisha utoaji wa mafunzo ya taaluma ya maendeleo ya jamii katika vyuo vya maendeleo ya jamii na mafunzo ya maarifa, ujuzi na stadi katika vyuo vya maendeleo ya wananchi, hususan, kuongeza mafunzo ya ufundi stadi katika vyuo 25 vya maendeleo ya wananchi;

Kuwajengea uwezo wanawake na wanaume ili washiriki katika ngazi zote za utekelezaji wa miradi na mipango mbalimbali ya maendeleo na kufaidika sawa katika maendeleo kwa kuendelea kutambua fursa mpya na muafaka hasa za kiuchumi zinazojitokeza katika maendeleo yao; na

Kusimamia sera na sheria na kuratibu utekelezaji wa mikataba ya kimataifa, kikanda na kimataifa inayohusu ustawi, haki na maendeleo ya wanawake na watoto kwa kutoa miongozo ya kukusanyia takwimu za watoto wanaonyanyaswa na wanaoishi mitaani.
Mheshimiwa Spika, hali ya utekelezaji wa mpango wa mwaka 2011/12 na malengo ya mwaka 2012/13 ni kama ifuatavyo: 
Maendeleo ya Jamii
Mheshimiwa Spika, taaluma ya maendeleo ya jamii ni muhimu katika kuwajengea uwezo na fikra sahihi wananchi na kuimarisha ushiriki wao katika shughuli za maendeleo. Taaluma hii hapa nchini hutolewa katika vyuo vya maendeleo ya jamii ambavyo viko tisa (9) nchini. Katika mwaka 2011/12, Wizara yangu kupitia vyuo hivyo, ilidahili jumla ya wanachuo 3,074 wakiwemo wanaume 830 na wanawake 2,244. Jumla ya wanachuo 173 walidahiliwa katika ngazi ya shahada, wanachuo 385 ngazi ya stashahada na wanachuo 2,516 ngazi ya astashahada. Katika mwaka 2012/13, Wizara yangu itaendelea kudahili wanachuo katika taaluma ya maendeleo ya jamii.
Mheshimiwa Spika, ili kuboresha mazingira ya kufundishia nakujifunzia, Wizara yangu katika mwaka 2011/12 iliyafanyia ukarabati majengo na miundombinu katika vyuo. Chuo cha Maendeleo ya Jamii, Mabughai – Lushoto, Tanga kilifanyiwa ukarabati. Aidha, vyanzo vya maji vya Chuo cha Maendeleo ya Jamii, Mlale – Songea vijijini, mkoani Ruvuma vilijengewa uzio ili kuhifadhi na kulinda mazingira yake. Katika mwaka 2012/13, Wizara yangu inatarajia kuendelea na ukarabati wa majengo na miundombinu katika vyuo vingine, kwa kutegemea rasilimali fedha zitakazopatikana.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12 Wizara yangu iliendesha mkutano mkuu wa mwaka wa sekta ya maendeleo ya jamii.  Mkutano huo uliwapa fursa wataalamu wa sekta ya maendeleo ya jamii na wadau wake kutathmini mwenendo wake na kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto zilizopo katika sekta hiyo hapa nchini.  Jumla ya washiriki 280 kutoka Wizarani, vyuoni, halmashauri, sekretariati za mikoa na sekta nyingine walihudhuria. 
Mheshimiwa Spika, mafunzo ya ujuzi na stadi mbalimbali kwa wananchi yana umuhimu wa pekee kwa sasa kwa sababu yanawawezesha wananchi kujiajiri na kuajiriwa. Katika mwaka 2011/12, Wizara yangu kupitia vyuo 55 vya maendeleo ya wananchi iliwapatia mafunzo ya ujuzi na stadi wananchi 32,133 wakiwemo wanawake 15,632 na wanaume 16,501. Wizara inaendelea kuwashauri wahitimu kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali ili waweze kukopesheka kirahisi. Katika mwaka 2012/13, Wizara yangu itadahili na kutoa mafunzo kwa wananchi 35,820 ndani na nje ya vyuo.
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia vyuo 25 vya maendeleo ya wananchi, itaanzisha rasmi mafunzo ya ufundi stadi yatakayofuata mfumo wa VETA. Jumla ya vijana 1,250 watadahiliwa katika vyuo hivyo kuanzia mwezi Januari 2013. Mfumo huo utawezesha wahitimu kujiajiri, kuajiriwa na pia kujiendeleza kupitia mfumo rasmi wa elimu.
Mheshimiwa Spika, katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, Wizara yangu iliendelea na ukarabati katika chuo cha Maendeleo ya Wananchi Muhukuru kwa mwaka 2012/13, Wizara imeandaa utaratibu wa ukarabati kwenye vyuo 25 vya maendeleo ya wananchi vinavyotarajiwa kuendesha mafunzo ya ufundi stadi kwa mfumo wa VETA. Vilevile, Wizara itajenga karakana zisizopungua tano (5) na kuziwekea vifaa vipya vya mafunzo. 
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Wizara yangu iliandaa programu ya kutoa mafunzo na kusambaza teknolojia sahihi kupitia vyuo vya maendeleo ya wananchi kwa lengo la kuwapunguzia mzigo wa kazi wananchi na kuwaongezea kipato, hivyo, kukuza uchumi wao. Hadi mwezi Machi, 2012 wakufunzi 52 walipatiwa mafunzo hayo. Sambamba na mafunzo hayo, aina sita (6) za teknolojia rahisi zilinunuliwa na kusambazwa vyuoni. Teknolojia hizo ni mashine za kufyatulia tofali, wanyama kazi, mikokoteni, mashine za kuangulia vifaranga, mashine za kukaushia matunda na mboga za majani na meko sanifu. Katika mwaka 2012/13, Wizara itaendelea kusambaza teknolojia hizo ili ziweze kuwafikia wananchi wengi vijijini. 
Maendeleo ya Jinsia
Mheshimiwa Spika, uwezeshaji wanawake kiuchumi ni suala linalopewa kipaumbele katika kutekeleza mikataba na maazimio mbalimbali yanayohusu maendeleo ya wanawake. Ili kuwakwamua wanawake kiuchumi, Wizara yangu iliendelea kuratibu na kusimamia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake kwa kushirikiana na halmashauri. Katika kipindi cha 2011/12, Wizara yangu kupitia mfuko huo ilitoa jumla ya Shilingi 120,000,000 kwa halmashauri 15 zilizokamilisha marejesho ya mikopo kwa ajili ya kuwakopesha wanawake wajasiriamali. Wanawake hao hupewa mikopo yenye masharti nafuu ambayo wanapaswa kuirejesha ndani ya mwaka mmoja, ili wanawake wengine waweze kukopeshwa. Mikopo hii itaendelea kutolewa kwa kipindi cha mwaka 2012/13 ili wanawake waendelee kunufaika na kujikwamua kiuchumi. 
Mheshimiwa Spika, ukosefu wa masoko ni tatizo linalowakabili wanawake wengi wafanyabiashara.  Ili kupunguza tatizo hili, Wizara yangu kwa kushirikiana na Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF) na wadau wengine imekuwa ikiwezesha wafanyabiashara wanawake kupata masoko ndani na nje ya nchi.  Mkakati unaotumika ni kuwapatia mafunzo ya biashara na ujasiriamali na kuwawezesha kushiriki maonesho ya kimataifa ya biashara hapa kwetu na nje ya nchi.  Kwa mwaka wa fedha uliopita jumla ya wanawake 350 walipatiwa mafunzo ya biashara na ujasiriamali na kuwezeshwa kushiriki katika maonesho ya biashara ya kimataifa ya Dar es Salaam.  Aidha, wanawake 20 (15 kutoka bara na 5 kutoka visiwani) waliwezeshwa kushiriki maonesho ya biashara ya kimataifa nchini Rwanda ambako pia mimi mwenyewe nilihudhuria na baadhi ya wataalamu wa Wizara. Kwa mwaka 2012/13 Wizara yangu itaendelea kuratibu na kusimamia ushiriki wa wanawake wajasiriamali katika maonesho mbalimbali ya biashara ya kimataifa.
Mheshimiwa Spika, taarifa za ukatili wa kijinsia zimekuwa zikitolewa kwa wingi sana na vyombo vya habari (TV, redio na magazeti).  Hali hii imetokana na elimu na hamasa kubwa iliyotolewa na Wizara yangu na wadau wengine. Katika kukabiliana na tatizo hili, Wizara yangu katika kipindi cha mwaka 2011/12, iliratibu Mkutano wa Mawaziri wa Maendeleo ya Wanawake na Jinsia kutoka Nchi Wanachama wa Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu uliofanyika Arusha tarehe 04 Novemba, 2011. Lengo la Mkutano huo lilikuwa ni kuandaa mapendekezo kuhusu kutokomeza ukatili wa kijinsia katika Ukanda wa Maziwa Makuu. Mapendekezo hayo yaliwasilishwa na kupitishwa na Wakuu wa Nchi Wanachama katika Mkutano Maalumu uliohusu upigaji vita ukatili wa kijinsia uliofanyika tarehe 16 Desemba, 2011 Kampala Uganda. Katika kipindi cha mwaka 2012/13, Wizara yangu itaendelea kuratibu na kutekeleza mipango na mikakati ya kutokomeza ukatili wa kijinsia.  Aidha, Wizara itatoa elimu zaidi na mbinu thabiti za kuzuia na kukabiliana na tatizo hili.
Mheshimiwa Spika, juhudi nyingine zilizofanyika ili kutokomeza ukatili wa kijinsia nchini, zilikuwa ni uzinduzi wa Kamati ya Kitaifa ya Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake, Watoto na Albino tarehe 19 Desemba, 2011. Aidha, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa pamoja na Umoja wa Afrika, iliandaa tukio la kupanda Mlima Kilimanjaro ambalo kaulimbiu yake ilikuwa “Speak Out-Climb Up”. Jumla ya washiriki 74 kutoka nchi 36 za Afrika, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika walishiriki katika zoezi hilo ambalo lilizinduliwa rasmi na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 05 Machi, 2012. Madhumuni ya kampeni hii yalikuwa ni kuongeza uelewa wa jamii kuhusu madhara ya ukatili dhidi ya wanawake na wasichana katika Afrika na kuziomba Serikali husika ziwajibike katika kupiga vita ukatili kwa wanawake na wasichana. Katika Kipindi cha mwaka 2012/13, Wizara yangu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itaendelea kuhamasisha na kutoa elimu kwa jamii ili kupiga vita ukatili wa kijinsia hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, nchi yetu imesaini na kuridhia mikataba mbalimbali inayohusu maendeleo ya jinsia na wanawake. Ili kuweza kutekeleza mikataba na maazimio hayo, Wizara ilishiriki katika Mkutano wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Hali ya Wanawake, Kikao Maalumu cha Baraza kuu la Umoja wa Mataifa (United Nations General Assembly Special Session - UNGASS) na Mkutano wa Maziwa Makuu Kuhusu Masuala ya Wanawake. Maazimio ya mikutano hiyo pamoja na mambo mengine yalikuwa ni kuinua kiwango cha usawa wa jinsia na uwezeshaji wa wanawake. Katika kipindi cha mwaka 2012/13, Wizara yangu itaendelea kushiriki katika mikutano hiyo na kuratibu utekelezaji wa makubaliano yatakayoafikiwa.
Mheshimiwa Spika, sanjari na kuanzisha madirisha ya taarifa kwa wanawake, Wizara imeanzisha Kituo cha Utafiti na Utunzaji Kumbukumbu za Wanawake katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru. Kituo hicho ni tawi la Kituo cha Kanda cha Utafiti na Utunzaji Kumbukumbu za Wanawake kilichopo Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Kituo hiki kina umuhimu wa pekee wa kuwawezesha Watanzania kupata matokeo ya tafiti mbalimbali zinazohusu jinsia zinazofanywa katika Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu kupitia Maktaba ya Digitali. Aidha, matokeo ya tafiti zitakazofanywa na kituo cha Tengeru yataweza pia, kusambazwa kwa nchi wanachama wa Maziwa Makuu kupitia Maktaba ya Digitali. Kwa mwaka 2012/13, Wizara kwa kushirikiana na wadau (UNESCO) itaendelea kukiimarisha Kituo hicho kwa kukiongezea vitendea kazi.
Mheshimiwa Spika, ili kuweza kutafakari mafanikio na changamoto zinazokabili jamii, hususan wanawake, Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali huratibu maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani tarehe 08 Machi, kila mwaka. Lengo la maadhimisho haya ni kuwakutanisha wanawake ili waweze kubadilishana uzoefu katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazowakabili. Kila mwaka maadhimisho haya huambatana na kaulimbiu kulingana na mazingira na uhitaji wa wakati husika. Kaulimbiu ya mwaka 2012 ilikuwa ni Ushiriki wa Wasichana, Unachochea Maendeleo. Kaulimbiu hii ililenga kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kuwashirikisha wasichana katika mipango mbalimbali ya maendeleo, ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa fursa sawa kati ya wasichana na wavulana katika elimu, mafunzo, uchumi, siasa na utamaduni.  Wizara yangu itaendelea kuratibu maadhimisho haya mwaka 2013.

Maendeleo ya Mtoto
Mheshimiwa Spika, suala la ulinzi na ustawi wa watoto ni mojawapo ya kipaumbele cha Wizara. Ili kutimiza ule msemo kuwa “watoto ni taifa na viongozi wa kesho”, tunapaswa kuwalinda na kuwakinga dhidi ya maambukizi ya magonjwa yakiwemo UKIMWI pamoja na ukatili wa aina yoyote ile. Katika mwaka 2011/12, Wizara kwa kushirikiana na wadau wengine wa masuala ya watoto hapa nchini, iliunda Kikosi Kazi cha Kitaifa ambacho kimeandaa rasimu ya awali ya mpango wa miaka mitano wa utekelezaji wa kutatua tatizo la watoto wanaoishi/kufanya kazi mitaani.  Mwezi Agosti, 2011, Wizara yangu ilizindua Ripoti ya Utafiti wa Ukatili Dhidi ya Watoto Nchini Tanzania. Ripoti hiyo imetoa makadirio ya awali ya ukubwa na sura ya ukatili wa kijinsi, kimwili na kiakili yanayowasibu wavulana na wasichana hapa nchini. Ripoti hiyo imeonesha kwamba, takribani wanawake watatu kati ya 10 na mwanaume mmoja kati ya saba walifanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsi na watu wazima walipokuwa watoto chini ya miaka 18.
Mheshimiwa Spika, matokeo ya utafiti huo yatasaidia kuweka mikakati madhubuti ya kuzuia na kukabiliana na tatizo hili.  Aidha, yatasaidia kuanzisha taratibu za kuboresha huduma kwa wahanga wa ukatili na kuandaa miongozo na kanuni za utekelezaji wa Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009. Katika mwaka 2012/13, Wizara itasambaza kanuni na miongozo hiyo katika halmashauri zote nchini, ili wananchi waweze kuzielewa na kuzizingatia. Pia, Wizara itatayarisha mwongozo wa kukusanya takwimu za watoto wanaonyanyaswa.
Mheshimiwa Spika, moja ya haki za msingi za mtoto, kama zilivyoainishwa katika mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda, ni haki ya kushiriki na kushirikishwa katika masuala yanayomhusu. Katika mwaka 2011/12 Wizara yangu kwa kushirikiana na wadau wa masuala ya watoto hapa nchini, iliandaa Zana za Ushiriki wa Watoto (Child Participation Toolkit) pamoja na Rasimu ya  Mkakati wa Taifa wa Ushiriki wa Watoto. Zana zote hizi zinalenga kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kumshirikisha mtoto katika masuala yanayomhusu kama ilivyobainishwa katika mikataba ya kimataifa na kikanda kuhusu haki na ustawi wa mtoto. Katika mwaka 2012/13, Wizara itaendelea kuimarisha Baraza la Watoto la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na mabaraza ya watoto ya mikoa na wilaya ili yaweze kutoa fursa nzuri za ushiriki wa watoto katika maeneo husika. Vilevile, Wizara itasambaza zana za ushiriki wa watoto kwa wadau wote wa maendeleo ya watoto hapa nchini ili waweze kuzielewa na kuzitumia.
Mheshimiwa Spika, malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya watoto ni muhimu katika kujenga msingi wa taifa lenye watu makini na wanaoweza kukabiliana na changamoto za maendeleo. Mwezi Februari, 2012 Wizara yangu kwa kushirikiana na wadau iliandaa mkutano wa kimataifa uliohusisha wadau wa ndani na nje ya nchi wa masuala ya watoto. Mkutano huu ulizingatia masuala makuu matatu (3) ambayo ni: kuandaa kiunzi (framework) kitakachoonesha namna nzuri ya kutekeleza malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto; kuanzisha namna bora ya ushirikiano wa kiutendaji; na kutoa fursa kwa wadau kubadilishana uzoefu na maarifa katika masuala yanayohusu malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.
Mheshimiwa Spika, mkutano huu pamoja na masuala mengine uliazimia kwa kukubaliana kuwa wadau wote hasa familia na kaya kuwekeza zaidi katika malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto ili kuwa na taifa bora la baadaye kutokana na ukweli kuwa maendeleo na ukuaji wa mtoto (katika maisha yake yote) hutegemea jinsi alivyotunzwa na kulelewa kuanzia umri wa siku 0 hadi 1000. Katika mwaka 2012/13, Wizara yangu itakamilisha uandaaji wa Sera Jumui ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kwa kuzingatia maelekezo tuliyopewa na Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Wizara yangu iliratibu maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ambayo yaliadhimishwa katika ngazi ya mkoa. Kila mkoa ulipata fursa ya kuadhimisha siku hii kulingana na rasilimali zilizopo ikiwa ni pamoja na kushirikiana na Asasi Zisizokuwa za Kiserikali katika mkoa husika.  Kaulimbiu ya mwaka 2012 ilikuwa ni Haki za Watoto Wenye Ulemavu: Ni Jukumu Letu Kuzilinda, Kuziheshimu, Kuzitimiza na Kuzitekeleza. Kaulimbiu hii ilikuwa inatukumbusha kuwa tuna jukumu la kuangalia upya utoaji wa haki za msingi kwa watoto wenye ulemavu na hasa katika miundombinu na utoaji wa huduma za msingi kama vile elimu na matibabu.  Vilevile, Wizara yangu iliratibu maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani yaliyofanyika kimkoa. Kaulimbiu ilikuwa ni Uwajibikaji Sawa katika Majukumu: Msingi wa Familia Bora. Kaulimbiu hii ililenga kuhamasisha na kushawishi wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuwajibika kwa pamoja katika malezi ya familia. Katika mwaka 2012/13, Wizara itaendelea kuratibu maadhimisho ya siku hizo kwa lengo la kuhamasisha jamii kuhusu haki na ustawi wa mtoto na maendeleo ya familia.
Mheshimiwa Spika, suala la kutokomeza mila zenye kuleta madhara kwa jamii ni miongoni mwa masuala yaliyopewa kipaumbele na Wizara yangu. Katika mwaka 2011/12,  Wizara kwa kushirikiana na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ilifanya mkutano na Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka katika halmashauri zote Nchini ili kujadili masuala ya ukeketaji na ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto wa kike. Mkutano huu uliazimia kuendelea kuhamasisha jamii zetu kuhusu madhara yanayowapata watoto wa kike wanapokeketwa. Aidha, kila halmashauri iliandaa mpango kazi wa kutokomeza ukatili dhidi ya watoto. Katika mwaka 2012/13, Wizara yangu imepanga kuendelea kuratibu utekelezaji wa mpango kazi wa kutokomeza ukeketaji na mila nyingine zenye kuleta madhara kwa jamii. 

Mashirika Yasiyo ya Kiserikali
Mheshimiwa Spika, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) yana umuhimu wa pekee katika kutatua changamoto zinazokabili jamii yetu hasa makundi maalumu. Kwa kutambua umuhimu huo, katika kipindi cha mwaka 2011/12, Wizara yangu iliendelea kurasimisha ushiriki wa NGOs katika shughuli za maendeleo Nchini. Jumla ya mashirika 675 yalisajiliwa ambapo kati ya hayo mashirika 646 yalipatiwa Cheti cha Usajili na mashirika 29 yalipatiwa Cheti cha Ukubalifu. Aidha, katika kuimarisha uratibu na ufuatiliaji wa NGOs Nchini, Wizara yangu iliteua rasmi Maafisa Maendeleo ya Jamii wa mikoa na wilaya kuwa Wasajili Wasaidizi wa NGOs katika ngazi husika. Uteuzi huu utaisaidia sana Serikali kuhakikisha kuwa mipango ya kazi ya NGOs inajumuishwa kwenye mipango ya maendeleo ya halmashauri husika ili kuwepo na utumiaji endelevu wa rasilimali fedha na watu. Aidha Bodi ya Taifa ya Uratibu wa NGOs ilizinduliwa rasmi.  Bodi hiyo ilipewa changamoto ya kubuni utaratibu wa kubaini mchango wa sekta ya NGOs nchini ili uingizwe kwenye pato la Taifa. Katika kipindi cha mwaka 2012/13, Wizara yangu itaendelea kusajili na kuratibu mashirika haya ili kuyawezesha kutambulika na kuendesha shughuli zao kisheria.
Mheshimiwa Spika, sekta ya NGOs Nchini inakabiliwa sana na changamato ya kujengewa uwezo wa kiuendeshaji na mbinu za kuibua fursa mbalimbali za kutunisha rasilimali fedha ili iweze kuendesha shughuli zake kwa uendelevu. Katika kipindi cha mwaka 2011/12, Wizara yangu kwa kushirikiana na Mitandao ya Mikoa ya NGOs na Taasisi ya ‘The Foundation for Civil Society’ iliwezesha kufanyika uchaguzi wa wajumbe wa Baraza la Taifa la NGOs katika awamu ya pili. Baraza hili jipya limeazimia kuhakikisha kuwa wadau wote wa sekta ya NGOs Nchini wanatumia Kanuni za Maadili ya NGOs na pia, utaratibu wa sekta yenyewe kujifanyia tathmini ya utendaji wao ili kuongeza uwajibikaji na uwazi miongoni mwao. Aidha, katika kipindi hiki NGOs 433 zilipatiwa rasilimali fedha kiasi cha shilingi 11,227,948,101 ikiwa ni ruzuku kutoka Taasisi ya ‘The Foundation for Civil Society’ ili kuwajengea uwezo wa kushiriki kikamilifu katika uchambuzi wa sera mbalimbali, utetezi, uhamasishaji wa jamii kushiriki katika michakato mbalimbali ya kitaifa kama vile katiba mpya, utawala bora na maendeleo ya kiuchumi kwa ujumla. Aidha, katika kuhakikisha kuwa taarifa mbalimbali kuhusu sekta ya NGOs Nchini zinapatikana kwa wananchi, Wizara yangu iliendelea kuhuisha Tovuti ya Taifa ya Uratibu wa NGOs na Benki ya Takwimu na taarifa za NGOs ambapo wadau 26,000 kutoka sekta binafsi, serikali, wabia wa maendeleo, taasisi za utafiti na elimu ya juu na Asasi za Kiraia (CSOs) walihudumiwa. Kwa mwaka 2012/13, Wizara yangu itaendelea kuhimiza taasisi mbalimbali na wabia wa maendeleo kuzijengea uwezo NGOs ili kuimarisha utendaji wao na pia kuongeza uwajibikaji katika sekta ya NGOs Nchini. 

Sera na Mipango
Mheshimiwa Spika, suala la ufuatiliaji na tathmini ni muhimu katika kuhakikisha kuwa yanakuwepo matumizi mazuri ya rasilimali za umma katika Wizara. Wizara yangu katika mwaka 2011/12 iliendelea kusimamia, kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa miradi na shughuli zingine katika Wizara ikiwa ni pamoja na kuvitembelea Vyuo vya maendeleo ya jamii na vya maendeleo ya wananchi.  Katika ufuatiliaji na tathmini hiyo, Wizara ilibaini kwamba miradi mingi haitakamilika kutokana na upatikanaji mdogo wa rasilimali fedha. Kwa mwaka 2012/13, Wizara yangu itaendelea kuratibu, kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa miradi ya maendeleo na shughuli zingine katika Wizara.
Mheshimiwa Spika, mipango ya maendeleo ni muhimu katika kuleta ufanisi na utaratibu mzuri wa utekelezaji wa majukumu ya Wizara.  Katika mwaka 2011/12, Wizara yangu ilikamilisha uandaaji wa Mpango Mkakati wa Wizara wa Miaka Mitano (2011 – 2016), unaotoa dira na mwongozo wa utumiaji wa rasilimali ili kuiwezesha Wizara kufanikisha malengo yake. Katika mwaka 2012/13, Wizara yangu itaendelea kuratibu utekelezaji wa Mpango Mkakati huo. 
Utawala na Utumishi
Mheshimiwa Spika, watumishi waadilifu na wanaowajibika ni muhimu katika kutekeleza majukumu ya Wizara. Katika mwaka 2011/12, Wizara yangu iliendelea kusimamia utendaji kazi kwa misingi ya haki, usawa, uadilifu, utawala bora na uwazi na kuweka mkazo katika kudhibiti vitendo vya rushwa na uzembe kazini. Masuala haya ni ya msingi katika kuiwezesha Wizara kufanikisha dira na dhima yake na ya Taifa kwa ujumla. Jitihada hizi zitaendelea kutekelezwa katika mwaka 2012/13. 
Mheshimiwa Spika, uwepo wa watumishi wenye uwezo ni nyenzo muhimu katika kuleta tija na ufanisi katika taasisi husika. Kwa mwaka 2011/12, Wizara yangu iliendelea kuwajengea uwezo watumishi wake kwa kuwapatia elimu na maarifa kupitia vyuo vya elimu ya juu vya ndani na nje ya nchi. Jumla ya watumishi 60 walipata mafunzo ya muda mfupi, kati na ya muda mrefu katika nyanja mbalimbali. Katika mwaka 2012/13, Wizara itawezesha watumishi 30 kupata mafunzo mbalimbali ya muda mfupi na mrefu.
Mheshimiwa Spika, katika kuwapatia motisha wafanyakazi, Wizara yangu kwa mwaka 2011/12 iliwapandisha vyeo watumishi 94, iliwabadilisha kazi watumishi saba (7) na kuwathibitisha kazini watumishi 127. Aidha, iliwaingiza kwenye masharti ya kudumu na malipo ya uzeeni watumishi 139 na kuwaingiza katika masharti ya kawaida watumishi 66. Kwa kipindi cha mwaka 2012/13, Wizara itaendelea kupandisha vyeo watumishi kwa mujibu wa Sera ya Menejimenti na Ajira Katika Utumishi wa Umma ili kuongeza tija katika utendaji kazi. 
Mheshimiwa Spika, katika kuboresha mazingira ya utendaji kazi, Wizara yangu imekamilisha ukarabati wa jengo la makao makuu ya Wizara. Katika mwaka 2012/13, Wizara itaendelea kuboresha mazingira ya nje ya ofisi kwa kuweka maegesho ya magari, bustani na njia za kupita kwa miguu. 
Mheshimiwa Spika, katika kutambua umuhimu wa afya kwa wafanyakazi, Wizara iliendelea na juhudi za kuwakinga dhidi ya athari za maradhi hasa UKIMWI. Katika mwaka 2011/12, Wizara yangu iliwezesha watumishi kumi (10) kupata viini lishe, madawa na chakula. Watumishi hao ni wale waliojitokeza kuwa wameathirika na Virusi Vya UKIMWI na UKIMWI. Katika mwaka 2012/13, Wizara itaendelea kutoa elimu na huduma hizo kwa watumishi. 

Mawasiliano Serikalini
Mheshimiwa Spika, suala la kujitangaza ni muhimu kwani linawezesha wadau na umma kwa ujumla kufahamu majukumu yanayotekelezwa na Wizara. Kwa mwaka 2011/12, Wizara yangu ilielimisha na kuhamasisha jamii kuhusu wajibu na majukumu yake kwa kutumia machapisho na matangazo mbalimbali yanayohusu elimu kwa umma. Aidha, ilitumia maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Maonesho ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), Kilimo (Nanenane) na Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara kuelimisha umma. Katika Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru, Wizara ilijitangaza kupitia uzinduzi wa Kitabu cha Mchango wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii katika Maendeleo ya Tanzania (1961–2011); Kitabu cha Mafanikio ya Miaka 50 ya Uhuru Katika Sekta ya Maendeleo ya Jamii; na maonesho ya huduma na bidhaa mbalimbali za wadau wa Wizara. Aidha, mwaka 2011/12 Wizara ilikutana na wanahabari wa vyombo mbalimbali kama vile runinga, radio, magazeti ili kutoa taarifa za masuala yanayohusu Wizara.  Katika mwaka 2012/13, Wizara itaendelea kutoa habari muhimu kwa wananchi kupitia vyombo vya habari, majarida na maonesho mbalimbali.

E: HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, mapitio ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2010 na malengo ya mwaka 2012/13 yanaonesha Wizara yangu ilivyo mtambuka na hivyo kuhitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali katika kuimarisha na kuleta ufanisi katika utendaji wa Wizara. Wizara kwa kushirikiana na wadau itaendelea kutekeleza majukumu yake ya kuiwezesha jamii kushiriki kikamilifu katika maendeleo yao binafsi na Taifa letu kwa ujumla. Lengo letu sote, ikiwa pamoja na Wizara yangu, ni kupunguza umaskini kwa kuboresha maisha ya Watanzania wote.
F: SHUKURANI
Mheshimiwa Spika, napenda sasa kumshukuru sana Naibu Waziri Mheshimiwa Ummy Ally Mwalimu (Mb.), kwa ushirikiano, ushauri na msaada mkubwa anaonipa katika kuongoza Wizara hii.  Vilevile, napenda kutoa shukurani za dhati kwa Katibu Mkuu Bibi Kijakazi Rajabu Mtengwa, Naibu Katibu Mkuu Bibi Anna Tayari Maembe, wakurugenzi, wakuu wa vitengo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Wanawake Tanzania, wakuu wa vyuo pamoja na wafanyakazi wote wa Wizara yangu wa ngazi zote, waliopo kwenye taasisi zetu zote, kwa jitihada zao katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara, ambayo ni pamoja na kuniwezesha mimi kuwasilisha hotuba hii mbele ya Bunge lako tukufu. Juhudi zao na maarifa katika utekelezaji wa majukumu tuliyo nayo umewezesha kuendeleza sekta hii muhimu.
Mheshimiwa Spika, kabla sijamaliza hotuba yangu, sina budi kuwashukuru wale wote tunaofanya nao kazi na wengine ambao kwa namna moja au nyingine tunashirikiana. Peke yetu kama Wizara tusingefikia mafanikio niliyoyataja. Naomba kupitia Bunge lako tukufu, kutoa shukurani zangu za dhati  kwa wafuatao: Asasi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA); Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF); Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP); Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA); Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA); Shirikisho la Vyama vya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (FAWETA); Medical Women Association of Tanzania (MEWATA); White Ribon; Friedrich Ebert Stiftung (FES); Plan International; Save the Children Tanzania; Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu; mashirika mbalimbali yasiyo ya Kiserikali; pamoja na wanaofanya kazi kwa maslahi ya jamii kwa namna moja au nyingine.

Napenda pia, kuzishukuru serikali za nchi rafiki ambazo kwa kupitia mashirika yake zinaendelea kutusaidia. Nchi hizo ni pamoja na Marekani (USAID); Jamhuri ya Korea (KOICA); Denmaki (DANIDA) na Kanada (CIDA). Aidha, Mashirika ya Umoja wa Mataifa ambayo ni: UNICEF; UNDP; UNFPA; UNESCO; ILO; Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo ya Wanawake (UN-WOMEN). Nayashukuru vilevile, mashirika mengine ya ndani na nje kwa misaada yao. Aidha, napenda kuwashukuru Umoja wa Nchi za Ulaya (EU), Ubalozi wa Ayalandi, Ubalozi wa Uingereza na Benki ya Dunia kwa kuwa tayari kushirikiana nasi.

G: MAKADIRIO YA BAJETI YA WIZARA MWAKA 2012/13

Mheshimiwa Spika, ili Wizara yangu iweze kutekeleza majukumu na malengo yake kwa mwaka 2012/13, sasa naliomba Bunge lako tukufu liidhinishe matumizi ya Shilingi 15,616,991,000. Kati ya hizo, Shilingi 12,155,650,000 ni kwa matumizi ya kawaida ambapo mishahara ni Shilingi 8,770,125,000 na matumizi mengineyo (other charges) ni Shilingi 3,385,525,000. Aidha, Shilingi 3,461,341,000 ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ambapo Shilingi 3,000,000,000 ni fedha za ndani na Shilingi 461,341,000 ni fedha za nje.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

1 comment:

Anonymous said...

I truly find this a interesting subject. Never looked at this subject in this manner. If you are planning to create more articles relating to this subject, I definitely will be back in the near future!