Mbunge wa Bahi mkoani Dodoma, Omary Badwel (43) alipandishwa kizimbani leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashitaka ya kushawishi na kupokea rushwa ya Sh milioni moja.
Kwa mujibu wa madai yaliyowasilishwa mahakamani hapo dhidi ya Mbunge huyo, lengo la kupokea fedha hizo lilikuwa ili apitishe bajeti ya Halmashauri ya Manispaa ya Mkuranga.
Badwell alisomewa mashitaka hayo na Mwendesha Mashitaka kutokaTaasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Janneth Machullya akisaidiana na Ben Linkolin mbele ya Hakimu Mkazi Faisal Kahamba.
Alidaiwa kuwa kati ya Mei 30 na Juni 2 mwaka huu katika maeneo tofauti tofauti Dar es Salaam, Badwel akiwa mjumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), alimshawishi Mkurugenzi wa Wilaya ya Mkuranga, Sipora Liana kutoka rushwa.
Alidai kuwa Badwel alimshawishi Sipora ampe rushwa ya Sh milioni nane ili awashawishi wajumbe wa kamati hiyo kupitisha bajeti ya mwaka 2011/2012 ya halmashauri hiyo kazi ambayo inafanywa na muajiri wake.
Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa Juni 2 mwaka huu katika Hoteli ya Peacock iliyopo katika Wilaya ya Ilala Dar es Salaam Badwel alipokea Sh milioni moja za rushwa.
Inadaiwa alipokea fedha hizo kutoka kwa Sipora kwa lengo la kwenda kuwashawishi wajumbe wa LAAC ili wapitisha bajeti ya halmashauri hiyo.
Upande wa Mashitaka ulidai kuwa, upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuomba tarehe ya kutajwa ili wapange tarehe ya kumsomea mshitakiwa maelezo ya awali.
Wakili anayemtete Badwel, Mpare Mpoki aliiomba Mahakama kumpa mshitakiwa dhamana kwa kuwa kosa analoshitakiwa nalo lina dhamana na anawadhamini wa kuaminika watakaomfikisha mahakamani kila anapohitajika.
Hakimu Kahamba alisema dhamana ya mshitakiwa ipo wazi endapo atatimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika watakaosaini hati ya Sh milioni nne kila mmoja na kuwasilisha mahakamani hati zao za kusafiria.
Hata hivyo mshitakiwa alirudishwa rumande na kubakia huko saa 1:30 kwa kuwa wadhamini wake walishindwa kutoa hati za kusafiria kwa madai kuwa hawana.
Kutokana na wadhamini hao kushindwa kutimiza masharti ya dhamana, ilibidi asubiri rumande kwa muda huo mpaka alipopata wadhamini wengine ambao walitimiza masharti hayo.
Hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 18 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena na mshitakiwa atakuwa nje kwa dhamana.
Kwa mujibu wa sheria endapo mshitakiwa huyo akikutwa na hatia ya kutenda kosa hilo, adhabu yake itakuwa ni faini au kifungo cha zaidi ya miaka mitatu jela ambacho kinaweza kumuondolea ubunge wake.
No comments:
Post a Comment