Monday, May 14, 2012

MASIKINI SIMBA WAMEAGA MICHUANO YA AFRKA...

Ni wazi kuwa haya ndio mambo matatu yaliyoigharimu Simba! Kwanza ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Wasudani hao katika mechi ya kwanza kwenye Uwanja wa Taifa wiki mbili zilizopita. Pili, kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka huu kutoka kwa mtani wake wa jadi. Na tatu, ushindi wa kihistoria walioupata katika mechi ya mwisho ya Ligi Kuu dhidi ya Yanga! Lakini yote tisa, kumi ni kwamba Simba SC imetolewa katika Michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mikwaju ya penalti 9-8 mbele ya El Ahly Shandy katika jiji la Shandy, baada ya kuruhusu mabao 3-0.
Katika mchezo huo uliopigwa usiku wa kuamkia leo, Emmanuel Okwi alishindwa kuonyesha cheche zake huku Simba SC wakianza vyema kwa kumudu mashambulizi ya Shandykatika kipindi cha kwanza cha mchezo.
Katika dakika ya 31 nusura Simba SC wapate bao la kuongoza baada ya Uhuru Selemani kushindwa kutumia nafasi aliyopewa, ambapo kipa wa Shandy aliyekuwa katika kiwango chake kupangua shuti la Uhuru na mpira kugonga mwamba wa juu na kuzalisha kona ambayo nusura Mafisango aiandikie goli Simba lakini kipa huyo alikuwa kizingiti kwa Simba.
Kipindi cha kwanza safu ya ulinzi ya Simba ilifanya kazi kubwa kuokoa hatari zote na kupelekea timu hizo kwenda mapumziko bila kufungana, huku mchezo ukionekana ku-balance kwa timu zote kushambuliana kwa zamu.
Kipindi cha pili kilikuwa kibaya kwa Simba SC kwa kuruhusu bao katika dakika ya 46 lililofungwa na Farid Mohammed na dakika ya tatu mbele Shandy wakaongeza bao la pili. Tangu hapo 'bundi' akahamia langoni mwa Mnyama huku Shandy wakilisakama lango la Simba.
Dakika ya 59 kujiamini kwa Victor Costa kulipelekea kwa Shandy kunasa mpira uliotumwa kwa Farid Mohammed na bila ajizi akaifungia Shandy goli la tatu na kupelekea dakika 90 kumalizika kwa Al Ahly Shandy kushinda mabao 3-0 hivyo kufanya matokeo ya jumla kuwa mabao 3-3..
Changamoto ya mikwaju ya penati ikachukua nafasi na Simba wakapoteza penalti mbili kati ya 10 walizopiga. Waliokosa penati kwa upande wa Simba ni Patrick Mutesa Mafisango penalti ya pili na Juma Kaseja penalti ya 10. Kwa Shandy aliokoa penalti hizo mbili wakati Juma Kaseja yeye aliokoa penalti moja.
Waliopata penalti za Simba ni Victor Costa, Kelvin Yondani, Amir Maftah, Salum Machaku, Shomari Kapombe, Emmanuel Okwi, Felix Sunzu na Mwinyi Kazimoto.
Simba iliwakilishwa na: Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Amir Maftah, Victor Costa, Kelvin Yondani, Mwinyi Kazimoto, Uhuru Selemani/Salum Machaku, Patrick Mafisango, Felix Sunzu, Haruna Moshi na Emmanuel Okwi

No comments: