Saturday, April 21, 2012

HUYU NDIYE ALIYEFANYA MAUAJI YA HALAIKI YA WATU 77...

KULIA: Muuaji Anders Behring Breivik mara baada ya kukamatwa. KUSHOTO: Jengo alilotega bomu na kuua watu wanane (juu). Ndugu wa marehemu wakiweka maua kwenye moja ya eneo walilozikwa ndugu zao (chini).
Leo, kama ilivyozoea kufanya kwa miezi minane iliyopita, Anders Behring Breivik atakaa chini na kupata kifungua kinywa cha chapati ama mkate wa kahawia kilichopakwa jibini ama siagi akishushia na kikombe cha kahawa nyeusi.
Na, amekuwa akila hivyo tangu alipokamatwa, atakula akiwa peke yake.
Mwanaume huyu anayetuhumiwa kuhusika katika mauaji ya kutisha ya halaiki nchini Norway, ametengwa kutoka kwa wenzake katika mji wa Ila, kambi ya wafuasi wa zamani wa kundi la Nazi ambayo sasa imekuwa gereza lenye ulinzi wa hali ya juu. Sababu ya kumtenga ni kuhofia kuwa endapo wanamfikia lazima watamuua.
Hivi karibuni, Breivik, ambaye aliua watu 77 Julai 22, mwaka jana, atapelekwa kujibu mashitaka katika mji mkuu wa Norway, Oslo.
Mwanaume huyo mwenye miaka 33, alitega bomu katikati ya mji mkuu huo na kuua watu wanane na kisha masaa mawili baadaye alimimina risasi kwenye kisiwa cha Utoya na kuua watu wengine 69, wengi wao wakiwa ni vijana wafuasi wa Chama cha Labour ambao walikuwa wamepiga kambi kisiwani humo.
Breivik hakukanusha tuhuma hizo za mauaji hayo mabaya zaidi ya halaiki kutokea kipindi hiki cha amani katika historia mpya ya Norway. Pia hakuonesha kujutia kitendo hicho.
Akilini mwake, mauaji hayo yalikuwa muhimu katika zoezi la kujijengea uhalali, yaliyopanga kuvuta hisia za mitazamo ya wapinzani wake kuhusu alichodai ni mapinduzi makubwa ya Kiislamu katika Ulaya.
Makamani, amesisitiza kudai hana hatia. Wanasheria wake wamesema anakusudia kudai kufanya mauaji hayo katika harakati za kujilinda.
Ila, maili saba nje ya Oslo, ni mji ambao mashujaa wa kundi la wanaharakati wa mapinduzi ya Norway ambako walifungwa, kuteswa na hatimaye kuuawa na askari wa kundi la Nazi. Hakuna shaka Breivik, ambaye anaonekana kujiona kiasi fulani kama mpigania uhuru, alifanya hivyo wakati muafaka.
Mfungwa hatari kama yeye kwa kawaida hupelekwa Ringerike, gereza lenye ulinzi mkali wa hali ya juu nchini Norway, lakini kwa kesi hii iliamriwa kufuatia eneo yalipotokea mauaji hayo kuwa jirani na Utoya.
Ila limewekezwa vifaa vya kisasa likiwa na selo 124 huku walinzi kati ya wawili ama watatu wakipiga doria ya uhakika katika kila selo 12.
Mapema asubuhi baada ya kupata kifungua kinywa, anafanya mazoezi yake ya kawaida kwenye gym, ambako kuna mashine ya mazoezi ya kukimbia.
Breivik anafurahia chumba alimowekwa chenye futi za mraba 86 kilichogawanywa vijichumba vidogo vitatu. Kimoja ni chumba cha kulala, gym na kingine kina kompyuta bila huduma ya intaneti ambacho anakitumia kwa kujisomea.
Randi Rosenqvist, mtaalamu wa magonjwa ya akili wa mahakama ambaye alimpima akili Breivik, amesema anayafananisha maisha ya yake na yale ya chekechea.
Kwa ujumla anafanyiwa yote hayo kufuatana na utaratibu wa sheria za Norway ambazo zina lengo la kurekebisha zaidi kuliko kuadhibu.
Baada ya kazi za hapa na pale, Breivik hukaa chini na kujisomea magazeti. Wakati mwingine anaposongwa na mawazo kuhusu mashitaka dhidi yake hutumia muda mwingi kucheza michezo ya kwenye kompyuta, lakini ni michezo ile tu isiyohusisha mapigano ndio inaruhusiwa. Wakati mwingine kutazama sinema mbalimbali ama kutazama vipindi vya televisheni.
Amewekewa kifurushi cha familia chenye chaneli 15 za televisheni. Mwaka 2009 wafungwa walifanya kampeni na kuruhusiwa kuwa na picha za ngono kwenye selo zao. Pia Breivik amewekewa kengele chumbani mwake ambapo amekuwa akiitumia pale anapohitaji sigara.
Baada ya chakula cha mchana, muuaji huyo anaruhusiwa kupunga hewa kwenye eneo lililozungushiwa uzio. Uzio huo ni kwa sababu za kiusalama.
Kwa siku zote hizo Breivik amekuwa akihojiwa na wapelelezi, hadi hivi karibuni alipohojiwa na mtaalamu wa magonjwa ya akili. Kwa kawaida amekuwa akipewa nafasi ya kukutana na wanasheria wake.
Pia amekuwa akiruhusiwa kuandika barua, fursa aliyoitumia kwa mwezi mzima uliopita katika barua ya wazi yenye kurasa 38 aliyoandika kwa tovuti tatu za habari za Norway.
"Kuchunguzwa akili kulikofanywa na wataalamu wawili waliochaguliwa na mahakama, Synne Sorheim na Torgeir Husby, 'ilikuwa ni pigo la papo kwa hapo", aliandika.
Vyombo vya habari Norway na familia za waathirika wa mauaji hayo zimeshinikiza kutolewa tena kwa mara ya pili ripoti ya vipimo.
Uchunguzi mpya uliokabidhiwa hivi karibuni umethibitisha kwamba Breivik amechanganyikiwa lakini anaweza kabisa kurudia kufanya mauaji kama hayo akipatia nafasi.
Dalili kuu za mtu mwenye uchanganyikiwaji kama huo ni mtu kujiona wa kipekee aliyechaguliwa na kuonesha wazi hamu ya kutenda kitu fulani.
Katika barua yake, Breivik amedai mafunzo ya Kijapani ya 'Bushido' yamemfanya apoteze hisia zote na amefanyia kazi mafunzo hayo kwa miaka mingi.
Baada ya chakula cha usiku, Breivik huzungumza na wanasheria wake ama kuandika. Wale waliobahatika kumwuona wamesema huwa anakoroma kwa sauti usiku akilala.
Pia amekuwa akiruhusiwa kutembelewa na wagezi wawili lakini mpaka sasa hajatokea hata mmoja. Baba yake ambaye ni mwanadiplomasia wa Norway aliyetengana na mkewe wakati Breivik akiwa mtoto, amedai kuwa hajawasiliana na kijana wake kwa miaka kumi na amesikitishwa na mabadiliko ya tabia yake.
Muda mfupi kabla ya mashambulio hayo, Breivik alikuwa akiishi katika nyumba moja na mama yake, Wence Behring.
Tangu mauaji hayo ya halaiki, mama huyo amekuwa akipatiwa matibabu kutokana na mshituko. Amedaiwa kusema hataki tena kumuona kijana wake na amekataa kabisa kumtembelea gerezani.
Kesi hiyo inatarajiwa kuunguruma kwa wiki kumi. Breivik anatetewa na Geir Lippestad. Muuaji alitamka wazi kutaka kutetewa na Geir ambaye aliwahi kumtetea mfuasi wa Nazi aliyetuhumiwa kwa mauaji siku za nyuma, Ole Nicolai Kvisler.
Lippestad alisema kuwa uamuzi wake wa kwanza aliofikia mara baada ya kuombwa kumtetea Breivik ilikuwa kukataa, lakini akakubaliana na kaulimbiu ya 'haki sawa kwa wote kwamba ni msingi mkuu katika ujenzi wa demokrasia'.
Hata hivyo, hivi karibuni aliliambia gazeti la Le Monde la Ufaransa: "Najihisi nimepoteza utu wangu katika hii kesi. Natarajia kuurejesha mara itakapomalizika kesi hii na nitakuwa na msimamo uleule kama ilivyokuwa hapo kabla."
Kuna tetesi kuwa Breivik anaweza kutumikia kifungo katika gereza la Halden, ambalo ni la pili kwa ukubwa nchini Norway.
Kuna kila sababu kuamini kwamba Breivik atakata rufaa mahakama za juu kupinga utaratibu wa kisheria uliotumika.
Muuaji huyo anataka uangalizi wa karibu kadri iwezekanavyo. Na hilo angalau anaonekana kupatiwa.

No comments: