Sunday, April 15, 2012

BIBI AIVIMBIA SERIKALI KUHUSU BOMOA-BOMOA...

Bibi mmoja ameng'ang'ania ndani ya jumba lake wakati matingatinga yakiendelea na kazi ya kuvunja nyumba za jirani katika zoezi la bomoabomoa ufukweni.
Bryony Nierop-Reading mwenye miaka 66 alimwaga machozi alipotazama majengo yaliyolizunguka jumba lake eneo la Norfolk lililoko futi 80 kutoka baharini.
Bibi huyo Nierop-Reading ni mmoja wa wamiliki wa mwisho waliosalia kuvunjiwa nyumba kuepuka mmomonyoko mkubwa ufukweni mjini Happisburgh.
Bibi huyo mwenye wajukuu sita amekataa kata-kata kuhama kwenye jumba lake lenye vyumba vitatu vya kulala, alilolinunua mwaka 2008.
Amesema: "Nimezimwa kabisa. Nilifahamu kuwa itatokea, lakini huu ni mwanzo tu wa mwisho wa Barabara ya Ufukweni kama tulivyokuwa tukiifahamu."
Bibi Nierop-Reading, ambaye anaishi na paka wake wanne, amesema alikataa ofa ya pesa za serikali kumhamisha eneo hilo kwakuwa ameshazoea kuishi kando ya bahari.
"Kila siku namshukuru Mungu kwa kuniweka hapa," amesema. "Sitaondoka hapa hadi nipende mwenyewe. Tazama mandhari niliyonayo."
Wakazi wa Barabara ya Ufukweni wamekuwa wakifuatiliwa kwa zaidi ya miaka 20 sasa wakipambana kunusuru nyumba zao zisimezwe na mmomonyoko wa mwamba wa bahari.
Majira ya saa 8:05 mchana juzi, wafanyakazi wa mamlaka husika walianza rasmi bomoabomoa ya nyumba tisa ambazo zitasambaratishwa kabisa katika miezi mitatu ijayo.
Nyumba ya mapumziko ya David na Jill Gilbert, ambayo wamekuwa wakiimiliki kwa miaka 36, ilichukua dakika zipatazo 30 tu kusambaratishwa.
Wanandoa hao kutoka Nottingham, walirejea Norfolk kutazama uvunjwaji wa nyumba yao hiyo iliyo kando ya bahari, Saltwood, inayopakana na bustani ya Bibi Nierop-Reading.
Bwana na Bi Gilbert walitumia pesa walizolipwa na serikali kwa ajili ya kusaidia waathirika wa mmomonyoko, kununua gofu lililo kwenye kiwanja cha jirani na hapo.
Bwana Gilbert anasema: "Inatia uchungu kusikia vioo vikivunjika na kutazama samani zilizomo ndani zikiharibiwa kabisa.
"Nimeumizwa kidogo, japo ni vizuri kuona hatimaye imetoweka kabisa maana tumekuwa tukiona inavyoelekea kuyeyuka miaka michache ijayo tangu tulipoitelekeza."
Kwa miaka kadhaa sasa, imeshuhudiwa nyumba zipatazo 20 zikimezwa na maji kutokana na mmomonyoko huo.
Kati ya nyumba 12 zilizotajwa kuwa kwenye hatari kubwa ya kumezwa na bahari, tisa zilinunuliwa na halmashauri mwaka jana.
Wamiliki wa nyumba tatu zilizosalia walichagua kuendelea kuishi kwenye nyumba zao.
Pindi nyumba hizo tisa zitakapovunjwa, mpango uliopo ni kutengeneza eneo la wazi ambapo watu wataweza kupunga upepo kutokea juu ya mwamba wakitazama maua ya asili.
Ng'ambo ya pili ya barabara kutokea kwenye nyumba, maegesho mapya ya magari yatatengenezwa na tayari vyoo vya muda vimeshasimikwa lengo likiwa ni kama mmomonyoko utaendelea basi iwe rahisi kuvihamisha.

No comments: