FAINALI MABINGWA ULAYA:
NI CHELSEA vs BAYERN MUNICH
Bayern Munich ya Ujerumani usiku wa kuamkia leo imefanikiwa kufanya kile kilichotarajiwa na wengi pale ilipoweza kuibana Real Madrid ya Hispania na kuing'oa mashindanoni kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 3-1 ndani ya dimba la Santiago Bernabeum mjini Madrid. Haikuwa kazi rahisi kwani hadi dakika 120, Real Madrid walikuwa wakiongoza 2-1 na hivyo kufanya matokeo ya jumla kuwa sare ya 2-2 kufuatia ushindi wa Bayern wa 2-1 mjini Munich wiki iliyopita. Licha ya kufunga mabao yote mawili, Cristiano Ronaldo na mwenzake Ricardo Kaka penalti zao kwa upande wa Madrid zilipznguliwa na kipa wa Bayern Manuel Neur. Sasa Bayern itavaana na Chelsea ya England ambayo juzi iliwavua ubingwa Wahispania wengine, Barcelona kwa kulazimisha sare ya 2-2 kwenye Uwanja wa Camp Nou, mjini Barcelona na kufanya matokeo ya jumla kuwa mabao 3-2, baada ya kuwa wameshinda 1-0 kwenye mechi yao ya kwanza Uwanja wao wa Stamford Bridge, mjini London wiki iliyopita. Mechi ya kwanza ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya timu hizo itapigwa kwenye dimba la Allianz-Arena, mjini Munich Mei 19 mwaka huu.

No comments:
Post a Comment