Sunday, April 1, 2012

ABAMIZA MTOTO WA DADAKE CHINI, AFA

 HABARI ILIYOSISIMUA GAZETINI LEO  
Mwanamke mkazi wa kijiji cha Nyabirongo, kata ya Susuni wilayani Tarime, Wankuru Mkami (25) ameangukia mikononi mwa Polisi kwa tuhuma za kusababisha kifo cha mtoto wa miezi 18, wakati akimgombea na mama wa mtoto huyo.
Imedaiwa kuwa siku ya tukio,  Machi 26, Wankuru akiwa na hasira, alimvuta kwa nguvu mtoto huyo, Matonge Mkami, alitekuwa amebebwa na mama yake, Nchagwa Mkami na kumbamiza chini.
Kaimu Kamanda wa Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Sebastian Zakaria jana alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
"Siku ya tukio Machi 26 saa nane mchana Wankuru na Nchagwa ambao ni ndugu, waligombana, Wankuru akamvuta kwa nguvu Matonge kutoka kwa mama yake na kumbamiza chini akitanguliza kichwa.
"Kwa kweli mtoto alipoteza fahamu. Wazazi wa mtoto na majirani walimkimbiza hospitali ya wilaya akiwa mahututi, lakini siku mbili baadaye aliaga dunia," alisema Kamanda Zakaria na kuongeza kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa kwenye mochari ya hospitali ya wilaya.
Kutokana na tukio hilo, Kamanda aliwaasa watu wa jamii ya kabila la Wakurya kuacha tabia iliyopitwa na wakati ya hasira zinazosababisha maafa katika jamii.
Mtuhumiwa aliyesababisha mauaji ya mtoto huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kujibu mashitaka ya mauaji. -HABARILEO, Jumapili Aprili 01, 2012

No comments: