Picha iliyotumwa kwenye mtandao wa Twitter ikimuonesha Bobbi Kristina Brown akiwa amekumbatiana na Nick Gordon.
Juzi usiku watazamaji runinga walipata fursa ya kufuatilia mahojiano ya Bobbi Kristina Brown kwenye kipindi cha Oprah Winfrey Show akielezea machungu anayokabiliana nayo kwa kumpoteza mama yake kipenzi Whitney Houston.
Masaa kadhaa baada ya mahojiano hayo, jana zimezuka taarifa za kushitua kwamba binti huyo mwenye miaka 19 ana mahusiano ya kimapenzi na Nick Gordon.
Bobbi na kijana huyo mwenye miaka 22 walinaswa Ijumaa iliyopita wakibusiana, kukumbatiana na kushikana mikono jirani na duka moja Johns Creek, mjini Georgia kama ilivyofichuliwa na mtandao wa hollywoodlife.com.
Jana Nick, kijana ambaye amekuwa akiishi kwa Whitney Houston tangu akiwa na miaka 12, amethibitisha mahusiano hayo na Bobbi.
Katika taarifa yake aliyoituma kwenye mtandao wa Twitter, Nick amesema, “Ni kweli niko karibu mno na Bobbi.”
Kama haitoshi, Ijumaa iliyopita Nick pia ametuma picha kwenye ukurasa wake wa Twitter ikimuonesha akiwa na Bobbi.
Kijana huyo ambaye hakupata bahati ya kuasiliwa rasmi na Whitney, aliwalekea mashabiki wake kufuatilia taarifa zaidi kwenye akaunti sahihi ya Bobbi Kristina.
“Unajua kuna matapeli wengi wameibuka na kujifanya ni Bobbi kwa kusambaza akaunti za uongo wakijifanya ni MY Krissi. Lakini ukweli ni kwamba akaunti sahihi ni @REALblBrown. Kinyume cha hapo akaunti hizo feki zipotezeeni tu.
Bobbi amekuwa mbali na mitandao ya kijamii tangu Desemba mwaka jana lakini amekuwa akiwasiliana mara kwa mara na ‘mpenzi’ wake Nick kupitia mtandao wa Twitter katika miezi ya mwishoni mwa mwaka jana.
Japo wamekuwa wakichukuliwa kama dada na kaka, ujumbe aliotuma Nick kwenye mtandao huo hivi karibu umefichua mengi kwamba kuna kitu kinaendelea kati ya wawili hao.
Kwenye mahojiano na Oprah yaliyoonyeshwa Marekani, Bobbi kwa mara ya kwanza alipata fursa ya kuelezea kifo cha mama yake.
Bobbi hakusita kuweka wazi nia yake ya kufuata nyayo za mama yake katika kazi ya kuimba na kuigiza.
Pamoja na yote yaliyozungumzwa kwenye kipindi hicho, si Bobbi wala mama yake mdogo, Patricia Houston waliomtaja Nick.
Msemaji wa Bobbi hakuweza kupatikana mara moja hiyo jana kukiri ama kukanusha tuhuma hizi.

No comments:
Post a Comment