PICHA YA JUU: Fabrice Muamba akiwa amekaa kitandani hospitalini. CHINI: Ujumbe mbalimbali wa kumtakia afya njema Muamba. Ujumbe wa kushoto unasomeka "Tunashukutu kwa msaada wako kwa Fabrice" na ule wa kulia inasomeka "Tunaungana kwa ajili ya Fabrice"
Ni picha ambayo dunia nzima ilikuwa ikingoja kwa hamu kuiona.
Fabrice Muamba ameketi kwenye kitanda chake hospitalini akiwa ameachia tabasamu tamu takribani wiki mbili tangu aanguke uwanjani muda mfupi kabla ya mapumziko.
Mchumba wa mchezaji huyo, Shauna Magunda ametuma picha kwenye mtandao wa Twitter jana kuwashukuru mamilioni ya mashabiki ambao waliungana naye kumwombea Muamba ambaye moyo wake ulikuwa ukikaribia kuacha kufanya kazi.
Picha inamuonesha nyota huyo wa Bolton akiwa amevalia jaketi la bluu huku akiwa ameegemea kitanda chake hospitalini hapo. Tabasamu lake linaashiria maendeleo mazuri ya afya yake tangu siku ya mechi Machi 17.
Shauna aliandika pembeni ya picha: “Fab amenitaka niwatumie wote picha hii na kwa niaba yake nawashukuru sana kwa msaada wenu.”
Picha hiyo imevuta hisia kali kutoka kwa mashabiki kwenye mtandao huo wa kijamii.
Shabiki mmoja aliandika: “Mungu akubariki Fabrice. Endelea kupambana, kijana. Nakuombea upone haraka.”
Moyo wa Muamba ulisimama kufanya kazi kwa zaidi ya saa moja wakati madaktari akiwamo mtaalamu wa magonjwa ya moyo aliyeingia uwanjani kujitahidi kupigania uhai wa mchezaji huyo.
Alikimbizwa Hospitali ya Kifua ya mjini London, ambako alitembelewa na wachezaji wenzake wa Bolton na makundi ya wapenzi wa soka.
Baadaye ilibainika kuwa baada ya kushituliwa kwa mashine maalumu mara 15, mchezaji huyo ndipo akaanza kuonesha dalili za uhai.
Tukio hilo limeistusha jamii ya wapenda soka na wengineo ambao wameonesha kuguswa yaliyomsibu mchezaji huyo mwenye miaka 23, huku familia yake ikiwaomba mashabiki wamuombee.
Picha hiyo itakuwa faraja kubwa kwa jamii ya wapenda soka ambao wamekuwa wakifuatia kwa ukaribu maendeleo ya afya ya kijana huyo. Anaonekana atachukua muda mrefu kuwa nje ya uwanja kwa ajili ya matibabu kabla hajarudi kucheza tena.
Wakati huohuo, mwanafunzi aliyetuma ujumbe wa kuchekelea ‘kifo’ cha Muamba kwenye mtandaio wa Twitter, ameshindwa rufani yake na hivyo anakwenda lupango kutumikia adhabu yake ya kifungo cha siku 56 jela.
Liam Stacey mwenye miaka 21, pia anakabiliwa na adhabu ya kufukuzwa chuo kutokana na ubaguzi wake huo aliofanya dhidi ya Muamba. Alikuwa mwaka wa mwisho Chuo Kikuu cha Swansea akisomea digrii ya baiolojia.
No comments:
Post a Comment