1: Charla Nash akiwa kwenye banda alilokuwa sokwe huyo kabla ya shambulio. 2: Sokwe-mtu Travis. 3: Sura bandia zikionesha uharibifu uliotokea na nyingine ikionesha inavyotakiwa kuwa. 4: Sura mbili za Charla, moja baada ya kushambuliwa na nyingine kabla. 5: Charla anavyoonekana sasa akiwa amejifunika kuepuka kuwatisha watu kama anavyosema mwenyewe.
Licha ya kupoteza uwezo wake wa kuona, midomo, pua na mikono kwenye tukio lisilosahaulika la kushambuliwa na sokwe mtu mwaka 2009, Charla Nash ambaye amepandikiziwa sura mpya anasema anajisikia vizuri tu na sura yake hiyo mpya.
Mwanamke huyo jasiri kwenye miaka 58, ambaye alikaribia kifo wakati aliraruriwa na sokwe ameeleza kuwa anajisikia hana tofauti na alivyokuwa kabla ya shambulio hilo.
"Najihisi kama ni sura yangu ya kawaida," anasema Charla. "Ina tofauti ndogo sana na nilivyokuwa awali."
Charla, mwanamke anayeishi Stamford, mjini Connecticut, amesema anaendelea kubadilika na sasa anaweza kuonesha ishara zote zinazopatikana usoni.
"Kila siku misuli yangu inaendelea kulainika vizuri," ameeleza.
Sandra Herold, mmiliki wa sokwe huyo anayejulikana kama Travis mwenye uzito wa kilo 200, alifariki mwaka 2010 kwa ugonjwa wa anaemia.
Charla anasema kama angepata nafasi ya kusema kitu kwa bosi wake huyo wa zamani na marafiki angesema, "samahani kwa hili lililotokea. Hakuna tunachoweza kubadili sasa."
Hata hivyo, aliongeza kuwa Herold alikuwa 'mtu wa mikosi' ambaye alikuwa akimhofia sana sokwe wake huyo ambaye alipigwa risasi na kufa katika shambulio hilo dhidi ya Charla.
Katika mahojiano ya yaliyopita siku za nyuma, Charla alibainisha kwamba kuwekewa sura yake mpya kumemuwezesha kurejesha hadhi yake ya ubinadamu na sasa anaweza tena kunusa na kula.
Pia ameweza kupata tena hisia sehemu yake ya mbele kwenye fizi, kope na pua.
Lakini kubwa kuliko yote ni kwamba ameanza kujifunza kutabasamu. "Imefikia hapa sasa," anasimulia Charla huku akionyeshea kidole chake mdomoni.
Katika mahojiano, Charla amesimulia miaka mingi ya ukarabati na matumaini ya kupata uhuru machoni pa watu.
"Sifahamu hatima yangu (ugonjwa) itakuwa vipi…hivyo sitaki kujipa sana matumaini," anasema Charla.
Aliongeza kwamba anataka aendelee kupata nafuu kiasi cha kuweza kuendesha farasi na kuishi kwenye nyumba yake mwenyewe.
Anasema anakosa kufanya mambo mengi madogo madogo kama kuwinda, kuota jua na pengine kumtazama binti yake, Brianna.
"Ninalazimika kutegemea zaidi msaada," anasema. "Maisha yangu yanategemea zaidi kutokuwa peke yangu. Nimekuwa nikiishi peke yangu hapo kabla."
Charla amekuwa akisikia maumivu kwenye mkono wake, licha ya ukweli kwamba ulilazimika kukatwa baada ya shambulio la mwaka 2009.
Upandikizaji sura mpya uliofanywa wakati wa upasuaji uliofanyika baadaye ulilazimika kuondolewa kutokana na sababu mbalimbali kuepusha madhara zaidi.
Upasuaji kwa ajili ya kupandikiza sura umefanyika chini ya timu ya madaktari na wataalamu wa upasuaji wapatao 30.
“Sihitaji mtu yeyote kunionea huruma,” anasema Charla. “Nataka nichukuliwe kama mtu mwingine yeyote.”
Hakika kuna gharama kubwa zimetumika na zinaendelea kutumika kwa ajili ya upasuaji, uangalizi na ukarabati ambao umegharimu mamilioni ya dola mpaka sasa.
Kwa mujibu wa ofisa mmoja wa serikali, kuna kesi za madai ya tahamani inayofikia dola milioni 150 ambazo zinasubiri kutolewa hukumu dhidi ya serikali kwa kushindwa kuwalinda wananchi dhidi ya viumbe hatari.
Mwajiriwa mmoja wa serikali ameripotiwa kuandika ujumbe kuwa shambulio hilo la sokwe Travis lilikuwa ni ‘ajali iliyokuwa ikingojewa kutokea.’
Charla ambaye amepata upofu mwaka 2009 kutokana na shambulio hilo, amewekewa vioo maalumu vya rangi ya kahawia na anatarajia kuongezewa vioo vingine baada ya kimoja alichowekewa kuharibika.
Matibabu hayo ya kupandikiziwa sura aliyapata katika Hospitali ya Brigham and Women’s mjini Boston takribani miaka miwili baada ya shambulio hilo.
Baada ya kupandikiziwa sura yake mpya, amelazimika kujifunika akisema amechagua njia hiyo kwakuwa ‘sitaki kuwatisha watu.’
Hakika hujafa hujaumbika, hayo ndio yaliyomsibu mwanamama Charla.

No comments:
Post a Comment