HAYA NDIO MAWASILIANO YA RUBANI WA PRECISION AIR...

Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), imesema mawasiliano ya mwisho kati ya rubani wa ndege iliyopata ajali Jumapili, Buruhani Rugaba na mwongoza ndege wa eneo hilo, ni kwamba hali ya hewa ya Bukoba ilikuwa mbaya na angeweza kurudi Mwanza.
Hayo yamebainishwa jana Dar es Salaam kwa waandishi wa habari na Mwongoza Ndege Mkuu wa TCAA, Mathias Maige akifafanua iwapo ndege hiyo ilikuwa na mawasiliano kati ya rubani na mwongoza ndege Bukoba.
“Katika sheria za usafiri wa anga rubani anawasiliana na waongoza ndege ambao ndio wanampa taarifa za mruko na vitu vingine. Kwa kifupi tu, rubani alishapewa taarifa yeye ndiye mwenye maamuzi ya mwisho,” alisema Maige.
Alisema kwa utaratibu wa uongozaji ndege, kwenye taarifa za ndege ya Precision, rubani alishuka kwenda Bukoba na waongoza ndege walimueleza hali ya hewa ya Bukoba kwa sababu wana mitambo na rada ya kuona ndege na rubani alisema anauona uwanja wa Bukoba ingawa hali ya hewa ilikuwa mbaya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari alisema rubani Rugaba aliyekuwa akirusha ndege aina ya ATR-42-500 iliyopata ajali katika Ziwa Victoria Bukoba mkoani Kagera, alikuwa na uzoefu wa kutosha.
“Alikuwa mwanzilishi wa ile ruti (safari), mwaka 1998 tunawaita pioneers (waanzilishi), ni mwalimu wa walimu na mmoja wa marubani bora nchini, Mungu amlaze mahali pema, ajali ile ilikuwa bahati mbaya tu,” alisema.
Johari alisema wakati Precision Air ikianza utaratibu wa kwenda Bukoba, Rugaba na mwenzake Sanare (marehemu pia), walianzisha safari hiyo na waliwafundisha marubani wengine.
“Hadi mauti inamkuta rubani Rugaba alikuwa amekusanya saa 23,515 za kuruka na kwa aina ile ya ndege aina ya ATR-42-500 alikuwa amekusanya saa 11, 929,” alisema Johari.
Aliongeza, “ndiye aliyeanzisha ruti za kwenda na ndege kubwa Bukoba aina ya Let L-410 inayobeba abiria 18 na hadi umauti unamfika alikuwa akirusha aina ya ndege ATR 42-500.”
Kwa mujibu wa Johari, viwanja havifanani, kuna vilivyo tambarare, vingine kuna milima pembeni na akasema Rugaba alikuwa anakijua vizuri kiwanja cha Bukoba.
Aidha, alisema msaidizi wake, Omondi hadi mauti inamfika alikuwa  amekusanya jumla ya saa 2,109 na kwa aina ile ya ndege ATR-42-500 alikuwa amekusanya saa 1,700 hivyo wote ni wazoefu wa safari hiyo.
Ndege hiyo ya Precision Air iliyokuwa na namba za usajili H5W-PWF ilianguka katika ziwa hilo kubwa barani Afrika ikiwa na abiria 44, ikaua abiria 19 na wengine 24 kujeruhiwa.

No comments: